1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uganda: Viongozi wa upinzani wahangaishwa na polisi

27 Novemba 2020

Mgombea wa urais wa NUP katika uchaguzi ujao nchini Uganda, Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine amelazimika kulala ndani ya gari baada ya hoteli zote katika eneo alilokuwa akifanya kampeni kukataa kumpokea.

Robert Kyagulanyi
Picha: Emmanuel Lubega/DW

Hayo yalijiri baada ya hiyo jana mwanasiasa huyo kutimuliwa na polisi kutoka studio za redio moja, wakati kipindi alichokilipia kilipokuwa kikirushwa hewani. 

Mgombea  urais wa chama cha NUP Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine pamoja na msafara wake ikiwemo wanahabari wamekesha wakiwa katika magari yao kando ya barabara. Hii ni baada ya polisi na vyombo vingine vya usalama kuzikataza hoteli zote magharibi mwa Uganda kuwapokea.

Katika jaribio la mgombea huyo kutafuta sehemu nyingine alisafiri umbali wa kilomita 200 hivi usiku wote wakitafuta pa kujibanza. Na hata alfajiri ya saa tisa, polisi wamefika eneo hilo na kuwapa dakika tano tu kuondoka.

Maafisa wa polisi wakifanya doria nje ya makao makuu ya chama chake Bobi WinePicha: Ronald Kabuubi/AP Photo/picture-alliance

Mgombea huyo ambaye hapo jana Alhamisi aliondolewa kwa lazima kutoka kituo kimoja cha redio dakika tatu tu baada ya kuanza kipindi

alichokuwa amelipia amewahimiza wafuasi wake wabaki watulivu na wasishiriki katika makabiliano yoyote na vyombo vya usalama licha ya

madhila hayo yote. Wagombea wengine nao wamekumbwa na unyanyasaji sawa na huo wakitatizwa na vyombo vya usalama katika kampeni zao.

Hata kijana John Katumba mwenye umri wa miaka 25 alikatakazwa kula chakula mji wa Jinja hapo jana.

Kufuatia malalamiko kutoka kwa wagombea wa urais, mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi Simon Byabakama amemwandikia mkuu wa jeshi la polisi kuamuru maafisa wake wakomeshe mienendo hiyo.

Robert Kyagulani akiwa ndani ya gari la polisiPicha: REUTERS

Wakati huohuo, Umoja wa Ulaya umetoa taarifa ukihimiza utulivu na fursa sawa katika kuwashughulikia wagombea katika kampeni zao. Aidha

ujumbe wa Umoja wa ulaya umeitaka serikali kuanzisha uchunguzi huru kuhusiana na vifo vya watu zaidi ya 50 kufuatia ghasia za kampeni

zilizozuka wiki iliyopita.

Mwandishi: Lubega Emmanuel