Uganda yaanza kampeni ya chanjo dhidi ya homa ya manjano
28 Mei 2024Uganda imeanza tena kampeni ya kutoa chanjo ya homa ya manjano ili kuulinda umma dhidi ya ugonjwa huo unaosambazwa na mbu.
Afisa anayesimamia zoezi hilo kutoka wizara ya afya daktari Michael Baganizi amesema kufikia mwishoni mwa mwezi Aprili, nchi hiyo ilikuwa imetoa chanjo kwa watu milioni 12.2 kati ya watu milioni 14 waliokusudiwa kupokea chanjo huo.
Daktari Baganizi ameeleza kuwa Uganda sasa itahitaji kila mtu anayeingia na kutoka nchini humo kuwa na cheti cha kuthibitisha kuwa amepokea chanjo ya homa ya manjano kama sehemu ya kanuni za kimataifa.
Dosi hiyo moja inatolewa bila malipo kwa raia wa Uganda wa kati ya umri wa mwaka mmoja hadi miaka 60. Serikali imesema imeweka vituo vya kutoa chanjo katika mji mkuu Kampala na pamoja na sehemu nyengine za umma ikiwemo shule, vyuo vikuu na hospitali.
Awali, raia wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki walilipa dola 27 ili kupokea chanjo ya homa ya manjano katika hospitali za kibinafsi.