1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uganda yakanusha madai ya Rwanda kuhusu kundi la M23

Lubega Emmanuel10 Novemba 2021

Uganda imekaunusha vikali madai ya Rwanda kwamba wapiganaji wa kundi la M23 wanaodaiwa ndio walikabiliana na majeshi ya Congo mwishoni mwa wiki iliyopita walitokea Uganda.

zum Thema - Friedensvertrag mit der M23 geplatzt - Kongo
Picha: Getty Images/Afp/Phil Moore

Hata hivyo, msemaji wa majeshi Uganda amethibitisha kwamba kuna kundi la waliokuwa wapiganaji wa M23 walioko Uganda kama wakimbizi, akasisitiza kuwa waliondolewa  kutoka eneo la mzozo kwenye mpaka na Congo wakapelekwa kambi za wakimbizi Kasikazini mwa Uganda mwaka 2017.

Kulingana na taarifa rasmi iliyotolewa na jeshi la ulinzi la Rwanda RDF, wapiganaji waliokabiliana na majeshi  ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo hawakutokea Rwanda kama ilivyodaiwa.

Taarifa hiyo imezidi kudai kuwa  kundi hilo linajumuisha waliokuwa wapiganaji wa M23 waliopata hifadhi Uganda mwaka 2013.

Hao ndio  walishindwa katika uvamizi huo walipojaribu kuviteka vijiji vya Tshanzu na Runyoni jirani na mji wa Bunagana kwa upande wa Uganda na wamerudi walikotokea.

Jeshi la Rwanda limetaja madai kuwa walitokea Rwanda na wamerudi huko kuwa propaganda inayolenga kuharibu mahusiano mazuri kati ya Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Viongozi wa kundi la M23 ndio walikuwa wa kwanza kukanusha madai kwamba wao ndio walihusika katika makabiliano na majeshi ya Congo eneo hilo mwishoni mwa wiki.Picha: Phil Moore/AFP/Getty Images

DW ilipomtaka Waziri wa mahusiano ya kimataifa wa Uganda Okello Oryem ajibu madai hayo kwa kuyakanusha vikali.

"Upuuzi… Upuuzi…. upuuzi…. Na ukitaka nirudie ….upuuzi," alisema Orwenyo

Kwa upande wake, msemaji wa majeshi ya Uganda Birgedia Flavia Byekwaso amefafanua kuwa kuna kundi la waliokuwa wapiganaji wa M23 waliokataa kurudi kwao baada ya viongozi wao kuafikiana na serikali ya Congo mwaka 2017.

Msemaji huyo ameongeza kuwa madai ya Rwanda hayana msingi wowote kwani hata waliokuwa wapiganaji wa M23 walioko Uganda wanaisha mbali kabisa na eneo la mzozo. Walipelekwa kaskazini mwa Uganda.

Angalau raia 5,000 kutoka Congo walikimbilia Uganda wakivuka mpaka eneo la Bunagana mapigano hayo yalipozuka mkesha wa Jumapili tarehe 7 mwezi huu.

Lakini wengi wao wameshawishiwa kurudi makwao baada ya majeshi ya Congo kuwazidi nguvu wapiganaji hao.