1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uganda yakataa kuwahifadhi wakimbizi wa Sudan Kusini

8 Oktoba 2020

Serikali ya Uganda imesema haitawaruhusu kuingia nchini humo wakimbizi zaidi ya 1,000 waliokwama kwenye mpaka wake na nchi ya Sudan Kusini.

Uganda Flüchtlingslager Palorinya Südsudan
Picha: DW/L. Emmanuel

Waziri wa majanga wa Uganda Hillary Onek ameelezea kuwa kwa sasa wanazingatia kanuni za kudhibiti ugonjwa wa COVID-19 na pia hawana uwezo wa kukidhi mahitaji ya wakimbizi hao kutokana na kupungua kwa misaada kutoka kwa wahisani katika kipindi hiki.

Shirika la Umoja wa Mataifa linalowashughulikia Wakimbizi, UNHCR, lilikuwa limetoa limetoa mwito kwa Uganda kuwaruhusu wakimbizi zaidi ya elfu moja waliokwama kwenye mpaka wa nchi hiyo na Sudan Kusini kwa wiki kadhaa kuingia ndani ya mipaka yake. Wakimbizi hao wanadai kuwa wanakimbia hali ngumu ya maisha sambamba na misukosuko ya kivita. Hata hivyo, waziri wa majanga Uganda, Hillary Onek, amesisitiza kuwa Uganda haijaondoa marufuku ya kuwaruhusu wakimbizi na kwa hiyo hakuna mkimbizi ataruhusiwa.

Ijapokuwa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji, IOM, limetaja kuwa lilikuwa tayari kufadhili misaada ya dharura kwa wakimbizi hao, serikali ya Uganda imeyataka mataifa wanakotoka wakimbizi kushughulikia raia wake kwa kuwahakikishia mazingira ya amani. Mwakilishi wa shirika hilo nchini Uganda, Sanusi Tegan Sacage, amesema inatanguliza haki za binadamu katika kuhakikisha kuwa watu ambao wangependa kukimbilia usalama sehemu nyingine wanasaidiwa:

Mwezi Juni mwaka huu, Uganda ililegeza kanuni za kudhibiti COVID-19 kwa kuwaruhusu wakimbizi 3,000 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuingia ndani ya nchi baada ya kundi hilo kukwama katika misitu kwenye mpaka wa nchi hiyo. Waziri Onek anafafanua kuwa kwa sasa hawawezi kukiuka kanuni za kulinda usalama wa raia wake huku wakizidi kulemewa na mzigo wa kuwatunza wakimbizi zaidi ya milioni moja laki nne walio nchini humo kwa sasa. Hii ni kufuatia kushuka kwa kiwango cha misaada kutoka kwa wafadhili:

Wakati huo huo, shirika la IOM limetoa mwito kwa jamii ya kimataifa kuchangia juhudi za kuwalinda watu wote katika kipindi hiki cha janga la COVID-19. Shirika hilo limesema litaendelea kuwasaidia raia wa nchi mbalimbali waliokwama nje ya mataifa yao kurudi makwao.

Lubega Emmanuel/DW Kampala

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW