1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uganda yalazimika kuwapokea wakimbizi 4000 wa DRC

Admin.WagnerD22 Juni 2020

Licha ya maamuzi ya awali ya kutowaruhusu wakimbizi wengine kuingia nchini mwake kutokana na janga la COVID-19, Uganda imelazimika kuwapa hifadhi wakimbizi 4,000 waliokimbia mapigano ya hivi karibuni nchini Congo.

Symbolbild Kongo Flüchtlinge
Picha: Reuters/J. Akena

Waziri wa majanga wa Uganda amefafanua kuwa wamechukua hatua hiyo kwa msingi ya kibinadamu. Haya yanajiri wakati shirika la umoja mataifa linalowashughulikia wakimbizi UNHCR likionya kuwa halitaweza kuendelea na shughuli zake kuanzia mwezi Septemba ikiwa hawatapata ufadhili zaidi kwa wakimbizi zaidi ya milioni moja nukta nne walioko Uganda. 

Tishio la maambukizi ya virusi vya Corona liliilazimu Uganda kufunga mipaka yake kwa raia wa kigeni mwezi Machi mwaka huu. Lakini nchi hiyo imezidi kukabiliwa na shinikizo la idadi kubwa ya wakimbizi wanaotokea nchi za Jamhuri Ya Kidemokrasia ya Congo pamoja na Sudan Kusini.

Awali idadi ya wakimbizi 4,000 waliotokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo walizuiliwa kwenye vituo vya mpakani kule Kaskazini Mashariki. Viongozi wa eneo hilo waliitaka serikali iwaruhusu wakimbizi kutoka nchi hizo kuendelea kuingia nchini kwani ingekuwa vigumu kuwadhibiti kama wangeamua kupitia njia zisizo rasmi.

Kundi la wakimbizi nchini Uganda mwaka 2017Picha: Getty Images/D. Kitwood

Huku idadi ya wakimbizi ikiongezeka Uganda, Shirika la Umoja Mataifa linalowashuhulikia wakimbizi UNHCR limeelezea wasiwasi kuwa halitakuwa na fedha za kuwahudumia wakimbizi kufikia mwezi Septemba.

Kulingana na mwakilishi wa UNHCR nchini Uganda Joel Boutrout, wana upungufu wa dola milioni 250. Wanahitaji angalau dola milioni 50 za dharura ili angalau kukidhi mahitaji ya wakimbizi yasiyohusiana na chakula.

Kwa sasa, mataifa kadhaa yameelekeza ufadhili wao kwa janga la COVID-19 katika nchi zao. Hii imewasababisha kutotimiza ahadi zao za kufadhili shughuli za kuwahudumia wakimbizi. Hata hivyo waziri wa majanga wa Uganda Hillary Onek ameyakososa baadhi ya mataifa kwa kusababisha migogoro ya kisiasa inayolazimu watu kuwa wakimbizi. Kwa hiyo anayataka yazingatie pia kufadhili shughuli za kuwahudumia wakimbizi hata katika kipindi hiki.

Serikali ya Uganda na shirika la UNHCR wameelezea kuridhishwa mpaka sasa na ukweli kwamba angalau COVID-19 haijawa tishio kwa wakimbizi walioko Uganda. Wakimbizi wengi wanazingatia mwongozo wa kuepusha maambukizi licha ya kuishi katika kambi zenze mazingira ya mikusanyiko ya watu.

Na Lubega Emmanuel DW Kampala.