1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uganda yarejesha mawasiliano ya inteneti

Saleh Mwanamilongo
18 Januari 2021

Mawasiliano ya mtandao yalirejeshwa Jumatatu nchini Uganda siku tano baada ya kusitishwa kote nchini kabla ya uchaguzi ambao upinzani umesema ulijawa na udanganyifu.

Uganda Kampala | Präsidentschaftswahl: Wahlplakate
Picha: Sumy Sadurni/AFP/Getty Images

Kasi ya mawasiliano hayo ingali ya chini na wakati mwingine mawasiliano hayo yanakatikakatika.Hatua hiyo imekuja  baada ya polisi kutangaza kwamba makumi ya watu walikamatwa kutokana na machafuko ya uchaguzi. Polisi imezingira makao makuu ya chama kikuu cha upinzani ambacho kiongozi wake yuko katika kizuwizi cha nyumbani.

 Rais wa mda mrefu Yoweri Museveni alitangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi huo akiwa na asilimia 58.6 ya kura, kwa muhula wa sita baada ya kuiongoza Uganda kwa miaka 35.

 Mpinzani wake mkuu, mwanamuziki aliegeuka kuwa mbunge Bobi Wine alishika nafasi ya pili akiwa na asilimia 34.8. Alitupilia matokeo hayo na kuita uchaguzi huo kuwa ni aibu.

Kasi ya mawasiliano bado chini sana

Msemaji wa serikali amesema hatua ambayo haijawahi kutokea ya kusitisha mawasiliano ya inteneti kwa mashahi za kiusalama ,iliochukuliwa Januarai 13, imeondolewa.

 ''Inteneti imerejeshwa. Hatua kuhusu mitandao mingine zimekuwa zikichunguzwa. Tutarejelea hali ya kawaida endapo hatua ya hivi sasa ya kufungua mawasiliano itakwenda vizuri. Tunawashauri watumiaji wa mawasiliano ya inteneti,hasa wale kutoka upinzani, kutoyatumia kwa ajili ya kueneza ujumbe wa chuki, na vitisho''. alisema  Ofwono Opondo msemaji wa serikali.

Kasi ya mawasiliano ya mitandao ya kijamii ilikuwa ya chini kwenye baadhi ya maeneo kwenye Mji Mkuu Kampala, ambako mamilioni ya watumiaji wake hawakuweza kutuma ujumbe,kuendesha utafiti au kutumia mitandao ya Facebook,Whatsapp na mitandao nyingine muda mrefu toka wiki iliopita.

Shirika lisilo la serikali la NetBlocks,linalofuatilia kukatwa kwa mawasiliano ya inteneti,lilisema kwamba data za mtandao ziliongezeka kwa asilimia 37 baada ya kukatwa kwa inteneti nchini Uganda. Shirika hilo limeliambia shirika la habari la AFP kwamba utaratibu wa kukatwa kwa mawasiliano ya inteneti nchini humo kumeonyesha kuwa kulipangwa.

Kiongozi wa upinzani wa chama cha NUP, Bobi WinePicha: Sumy Sadurni/AFP

Jumatatu, makao makuu ya chama cha Bobi Wine, NUP, mjini Kampala yalizingirwa na polisi,katika kile kiongozi wake alisema kwamba ni uvamizi wa polisi.

 ''Museveni baada ya kuiba kura kwa njia chafu kabisa katika historia,ametumia vitisho kwa njia ya kudharaulika'',aliandika kwenye mtandao wake wa twitter,Bobi Wine.

Upinzani wapinga matokeo ya uchaguzi

Tangu kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi, Bobi Wine na viongozi wa chama chake cha NUP wamepinga hatua ya tume ya uchaguzi kumtangaza rais Yoweri Museveni kuwa mshindi. Chama hicho kinahoji kwa nini matokeo kutoka vituo 1,257 hayakujumuishwi kwenye matokeo hayo huku vituo 271 kati ya hivyo vikiwa katika wilaya ya Wakiso ambayo ni ngome kuu ya Bobi Wine.

Chama hicho sasa kinaandaa ushahidi kuwasilisha rufaa mahakamani kupinga matokeo hayo. Lakini kisa cha majeshi na polisi kuvamia makao makuu ya chama hicho asubuhi ya leo na kuwazuia watu kuingia wala kutoka kimetajwa kuwa kitakwaza shughuli ya kukusanya ushahidi wanahitaji kuwasilisha mahakamani.

Picha: Abubaker Lubowa/REUTERS

Msemaji wa polisi ya Uganda, Fred Enanga alisema kwamba watu 55 walikamatwa wakati wa uchaguzi kutokana na visa vya utumiaji nguvu, ikiwemo kufunga barabara na uharibifu.

 Kipindi cha kabla ya uchaguzi kilighubikwa na umwagikaji wa damu na kunyanyaswa kwa wapinzani wa Museveni.

Watu wasiopunguwa 54 waliuliwa mwezi Novemba kufuatia siku mbili ya maandamano ya kupinga kukamtwa kwa Bobi Wine. Kiongozi huyo wa upinzani alikamatwa mara kadhaa.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW