Uganda yaripoti kifo cha kwanza cha ugonjwa wa Mpox
24 Oktoba 2024Waziri wa afya wa nchi hiyo Jane Ruth Aceng amefahamisha kuwa kifo hicho ni kielelezo kinachoonesha, hatua madhubuti zinastahili kuchukuliwa katika kukabiliana na kasi ya maambukizi ambayo kwa sasa idadi ya watu 153 wamekutwa na virusi vya ugonjwa huo.
Soma pia: Chanjo ya mpox kuchukuwa muda mrefu zaidi Kongo
Waziri huyo ameagiza majopo yaliyohusika katika kupambana na UVIKO-19 kwenye ngazi za wilaya kuitwa tena kushiriki kwenye juhudi za kupambana kuzuia kusambaa kwa ugonjwa huo.
Soma pia:Mripuko wa Mpox umeshaua watu 1,100 kote Afrika: CDC
Waziri Aceng, ameongezea kuwa katika kipindi cha wiki moja tu watu 42 waligundulika kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo, idadi kubwa ikiwa katika mji wa Kampala na viunga vyake. Wanasayansi wanasema ni rahisi kwa watu katika maeneo yenye misongamano kuambukizwa na wametowa ushauri, watu wajiepushe na maeneo kama hayo ikiwemo masokoni na vituo vya magari ya abiria.
Wiki mbili zilizopita serikali ya Uiengereza ilitangaza kutoa msaada wa pauni milioni moja kwa Uganda kuisaidia nchi hiyo kupambana na Mpox. Tangu shirika la afya duniani WHO lilipotangaza mripuko wa ugonjwa huo, juhudi za kupata chanjo miongoni mwa mataifa ya Afrika hazijaonekana kufanikiwa.