1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uganda yatakiwa kuheshimu haki za binadamu

2 Aprili 2020

Shirika la kutetea haki za binadamu Human Rights Watch limeitaka serikali ya Uganda kuhakikisha kuwa vikosi vyake vya usalama vinajiepusha kutumia nguvu wakati wa kutekeleza hatua za kukabiliana na janga la COVID-19.

Askari polisi Uganda
Picha: picture-alliance/AP Photo/R. Kabuubi

Shirika la kutetea haki za binadamu Human Rights Watch katika ripoti yake limevitaka vikosi vya kulinda usalama nchini Uganda kujiepusha kutenda vitendo vya ukatili dhidi ya raia wa Uganda.

Kulingana na mtafiti wa Uganda kwenye shirika la Human Rights Watch Oryem Nyeko, vikosi vya usalama vimekuwa vikitumia nguvu nyingi kutekeleza hatua za serikali zilizowekwa kwa ajili ya kupambana na maambukizi ya virusi vya corona. Nyeko amesema wakati ambapo Uganda pia inapokabiliwa na changamoto ya kiafya ni muhimu zaidi kwa serikali kuhakikisha kuwa haisababishi visa vya kukiukwa haki za binadamu.

Hadi kufikia sasa watu 44 wamethibitishwa kuambukizwa na virusi vya corona na hakuna mtu yeyote aliyefariki mpaka sasa. Serikali ya Uganda imeongeza hatua zaidi kwa ajili ya kuzuia kuenea kwa virusi hivyo.

Kuanza kwa marufuku

Mnamo Machi 25 serikali ya Uganda ilipiga marufuku shughuli za usafiri wa umma na masoko yasiyokuwa ya chakula. Kabla ya hapo ilianzisha hatua za lazima za kuwaweka watu karantini walioingia nchini humo kutokea nje katika hoteli ambazo walitakiwa kujilipia gharama zote.

Watu 44 wamepatikana na virusi vya corona UgandaPicha: AFP/S. Sadurni

Wiki moja baadae Rais Yoweri Museveni alitangaza hatua kadhaa za nyongeza, ikiwa ni pamoja na marufuku ya kutembea nyakati za usiku kwa muda wa siku 14.

Siku iliyofuata, Richard Karemire, msemaji wa jeshi la Uganda, alitangaza kwamba jeshi, na polisi wenye silaha wa Kitengo cha Ulinzi wa Mitaa (LDU), kinachoshirikiana na jeshi la Uganda, kitafanya doria na kusaidia kutekeleza maelekezo yaliyotolewa na serikali.

Mawakili wa kutetea haki za binadamu

Mawakili wa Jukwaa la Haki za Binadamu na Ulinzi (HRAPF), ambalo ni shirika linalotoa misaada ya kisheria nchini Uganda, limeripoti juu ya matukio ya polisi kuwanyanasa watu na kutolea mfano wa polisi kuvamia makao ya watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja nje ya jiji la Kampala, na kuwapiga na kuwakamata watu 23.

Mawakili hao wanaamini vijana hao walilengwa kimakusudi ingawa polisi waliwashtaki watu hao kwa kufanya uzembe unaoweza kueneza maambukizi na kutotii maagizo ya serikali kwa kukusanyana mahala pamoja.

Mtafiti wa Uganda kwenye shirika la Human Rights Watch Oryem Nyeko ameeleza kwamba jukumu la serikali ni kuhakikisha kwamba haki za kimsingi za watu zinapewa kipaumbele katika janga hili, haswa wale ambao wako katika hatari kubwa kama wachuuzi wa mitaani, na watu wasio na makazi. Ameitaka serikali ya Uganda kuwaamuru maafisa wote wasitumie nguvu wanapotekeleza hatua zilizowekwa. Oryem Nyeko pia ametoa wito wa kuwajibishwa wale wote wanaofanya vitendo vya dhuluma.

Chanzo: Human Rights Watch

Mhariri: Iddi Ssessanga