Uganda yatimiza miaka 50 ya Uhuru
9 Oktoba 2012"Ni Lulu ya Afrika". Hivyo ndivyo Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Winston Churchill, alivyowahi kuitaja Uganda. Hata hivyo, lulu hiyo imepoteza thamani yake. Baada ya utawala wa kikatili wa Milton Obote, Rais wa sasa Yoweri Museveni naye yuko madarakani kwa miaka 26.
Uchaguzi uliopita ulitajwa na waangalizi kuwa huru lakini si wa haki. Chama tawala NRM kiliendesha kampeni kubwa ya uchaguzi iliyogharimu fedha nyingi za umma. Baadhi ya wachambuzi wa siasa za Uganda hawatiwi moyo sana na hali ilivyo Uganda.
"Ni muhimu kufahamu kwamba mfumo wa kisiasa nchioni Uganda si wa kidemokrasia, bali ni sura ya kidemokrasia yenye kuendeshwa kidikteta. Polisi wamegeuzwa wanajeshi na ni wenye ukatili. Wanailinda serikali na sio umma. Pia wamejaa rushwa na kuangaliwa vibaya na raia. Kuna makundi kadhaa ya wanamgambo ambayo hayadhibitiwi kikatiba." Anasema Sarah Tangen, mkuu wa tawi la wakfu wa Friedrich-Ebert mjini Kampala.
Kauli inayomsuta Museveni
Mwaka 1986, Yoweri Museveni alitamka kwamba tatizo la Afrika ni la viongozi kubakia muda mrefu madarakani na hivyo kutumbukia kwenye rushwa na kuuvuruga uchumi. Lakini katika mkutano mmoja na waandishi habari aliulizwa kuhusu yeye mwenyewe na jibu lake liliwashangaza wengi, kwani sasa sio tu kwamba amebakia madarakani muda mrefu, bali tayari anaanza kuozea madarakani.
Kubakia madarakani kwa Museveni kunatokana pia na upande wa upinzani kukosa muelekeo. Maandamano na kampeni ya kwenda "Kazini kwa Kutembea" ikiwa ni kususia usafiri kwa sababu ya ughali wa maisha, rushwa na ukosefu wa haki za kijamii, hayakuweza kuwavutia watu wengi.
Kizza Besigye aliyewahi kuwa sahibu mkubwa wa Museveni na tangu miaka kadhaa sasa kiongozi wa chama kikuu cha upinzani Forum for Democratic Change, anasema miaka 50 iliopita imeshuhudia maendeleo ya miundo mbinu na kiuchumi lakini sio ya kisiasa .
"Miaka 50 baada ya uhuru bahati mbaya Uganda ingali kwenye njia panda. Miaka 50 kwetu haijaleta demokrasia wala utulivu wa jamii. Katika miaka yote 50 hakuna hata mtawala mmoja aliyefuata njia nyengine." Anasema Kiza Besigye, kiongozi wa upinzani.
Hakuna demokrasia
Licha ya haki ya kidemokrasia kusisitizawa katika katiba, lakini ukweli wa mambo ni mwengine. Haki ya kukusanyika na kuandamana imekuwa ikikandamizwa, kwa kutumiwa vyombo vya dola ambavyo huchukuwa hata hatua za kikatili. Agnes Kabajuni, msemaji wa Shirika la Haki za Binaadamu Amnesty International mjini Kampala anasema wao wana "wasiwasi sana na hali ya haki za binaadamu" ilivyo nchini Uganda.
Serikali inayakosoa mashirika yasiyo ya kiserikali kama Amnesty International na hasa panapohusika na misimamo yao kuhusu kuwatetea wanaharakati wanaopigania haki za mashoga. Mmoja wa mashoga hao ni David Kato ambaye mwaka uliopita aliuawa kikatili . Bunge limejaribu kuwasilisha sheria kutaka adhabu ya kifo kwa kosa la ushoga, huku jumuiya ya kimataifa ikijaribu kuishinikiza serikali kuzuwia sheria hiyo.
Wengi miongoni mwa vijana nchini Uganda ni wa umri wa chini ya miaka 20. Hawamjuwi rais mwengine isipokuwa Yoweri Museveni na wanapigania haki zao za kidemokrasia. Wabunge vijana wameanaza kuikosoa serikali na hiyo ni ishara ya matumaini katika kupigania demokrasia zaidi kwa lulu ya Afrika - Uganda .
Mwandishi: Andrea Schmidt/Saumu Mwasimba
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman