1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uganda yatishia kuwafukuza wafanyakazi wa afya wanaogoma

27 Mei 2022

Serikali ya Uganda imetisha kuwafuta kazi wafanyakazi wote wa afya ambao wanashiriki mgomo ikiwa hawatarudi kazini kufikia siku ya Jumatatu.Hata hivyo watumishi hao wameendelea kushikilia msimamo wao.

EAC Staaten Video-Konferenz | Yoweri Museveni
Picha: Philbert Rweyemamu/EAC

Licha ya onyo hilo la serikali viongozi wa makundi ya wafanyakazi hao ikiwemo wauguzi na wataalamu mbalimbali wamesisitiza kuwa hawababaishwi na tishio hilo kwani wanadai haki yao waliyoahidiwa mwaka 2017.

Kinyume na matarajio kuwa serikaliingejitokeza na njia ya kuwashawishi wafanyakazi wa afya kukomesha mgomo huo warudi kazini, waziri wa utumishi wa umma amekariri  tamko  la awali la waziri mkuu kwamba watafutwa kazi wasipositisha mgomo huo kufikia siku ya Jumatatu.

Waziri wa Utumishi wa Umma Wilson Muruli Aliwasisitiza watumishi hao kuwa endapo hawatabadili mawazo juu mgomo huo itawafuta kazi.

Watumishi:Hatubabaishwi na kitisho cha kufutwa kazi

Mgomo wa wataalamu mbalimbali wa afya ulianza tarehe 16 mwezi huu lakini athari zake hazikuhisika ipasavyo hadi hapo jana wenzao wauguzi na wakunga walipojiunga nao siku ya Jumatano.

Kwa sasa madaktari wanapata shida kuwashughulikia wagonjwa bila usaidizi wa wataalamu hao na ndicho chanzo cha wagonjwa waliokwenda kwenye vituo vya afya vya serikali kutopata huduma stahiki.

Soma zaidi:Mgomo wa madaktari Uganda wasababisha maafa

Wengi wamelazimika kurudi makwao na wale walio na uwezo kifedha kuamua kwenda kwenye vituo binafsi. Viongozi wa makundi hayo ya wafanyakazi wa afya wamesisitiza kuwa hawatababaishwa na vitisho vya kufutwa kazi kwani wanadai haki yao walioahidiwa tangu mwaka 2017.

Waziri mkuu Robinah Nabbanja alinukuliwa siku ya Jumatano akisema kuwa serikali inapanga kuwaita wataalamu wa afya ambao hawana ajira kujitolea kuziba pengo ambalo limesababishwa na wanaoshiriki mgomo.

 Miongoni mwa hao ni wale wataalamu waliajiriwa na jeshi. Lakini wataalamu wanaogoma wamesema kuwa itakuwa kazi bure kwani idadi iliyopo haiwezi kukidhi mahitaji ya wagonjwa wengi wanaotegemea huduma za serikali.

Mgomo wawaathiri raia wa kawaida

Baadhi ya  raia wamekosoa pande zote mbili kwa kutojali dhiki ya wagonjwa na kukataa kukubaliana kwamba la muhimu ni utaoji huduma ili kuokoa maisha.

MMoja wa wauguzi akiwa katika majukumu yake kabla ya mgomo.Picha: Badru Katumba/AFP/Getty Images

Baadhi ya raia wamekuwa wakienda katika vituo vya afya kwa ajili ya kupata huduma lakini hakuna huduma inayotolewa, kutokana na watumishi hao kuendesha mgomo wakidai maslahi yao.

Soma zaidi:Museveni: Kupunguza ushuru kutavuruga mipango ya serikali

Wiki iliyopita serikali ilifanikiwa kushauriana na walimu wa sayansi waliokuwa katika mgomo wakidai nyongeza ya mishahara. Mgomo huo uliathiri pakubwa masomo katika shule za umma.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW