1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUganda

Uganda yatuma wanajeshi mashariki mwa Kongo

22 Novemba 2022

Msemaji wa jeshi Uganda amethibitisha kuwa kikosi cha majeshi kutoka nchi hiyo kinaelekea mashariki mwa Kongo kushiriki katika operesheni ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kukomesha harakati za makundi ya wapiganaji.

DR Kongo | kongolesische Soldaten auf dem Weg zur Front im Kampf gegen die M23-Rebellen
Picha: Arlette Bashizi/AFP/Getty Images

Mnamo mwezi Septemba, serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ilitoa idhini kwa majeshi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuingia ndani ya mipaka yake na tangu hapo Burundi, Kenya na Uganda zimeitikia mwaliko huo kwa kushiriki katika operesheni maalum inayolenga kuleta amani mashariki mwa Kongo, hasa baada ya kundi la wapiganaji wa M23 kujiimarisha zaidi na kudhibiti sehemu kadhaa nchini humo. 

Msemaji wa majeshi wa Uganda, Brigedia Felix Kulayigye, alifafanua siku ya Jumanne (22 Novemba) kwamba majeshi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki hayalengi tu kumaliza mapigano kati ya waasi wa M23 na wale wa serikali, bali "yatashughulikia pia makundi mengine ya waasi na wapiganaji yaliyomo Kongo" yanayodaiwa kutatiza amani na utulivu katika mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. 

Brigedia Kulayigye alisema kuwa operesheni hiyo ni tofauti kabisa na inayoanza na hata sasa wamepata mafanikio makubwa kuwatokomeza waasi hao.

Msemaji huyo wa majeshi ya Uganda alisisitiza kuwa jukumu la wanajeshi wake ni kumaliza mgogoro kwa njia ya amani, lakini aliwaambia waandishi wa habari kwamba "mazungumzo yatafanyika tu baada ya wapiganaji kusalimisha silaha zao."

Muelekeo mpya wa kusaka amani ya Kongo

Safari hii, juhudi za muda mrefu za kutatua mizozo ya wapiganaji mashariki mwa Kongo zimechukuwa mkondo mwingine, ambapo mchakato wa kisiasa na kidiplomasia unakwenda sambamba na mipango ya kijeshi.

Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (kushoto), Rais João Lourenço wa Angola (katikati) na Rais Paul Kagame wa Rwanda wamo kwenye mazungumzo ya kurejesha amani mashariki mwa Kongo.

Rais Mstaafu wa Kenya Uhuru Kenyatta pamoja na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dkt. Peter Mathuki, wameshuhudiwa wakishauriana na viongozi wa kikanda, hasa marais wa Rwanda na Kongo, kukubali mchakato wa kuleta amani kuanza kwa mazungumzo na makundi ya wapiganaji.

Hata hivyo, wadadisi wa masuala ya kisiasa wana mtazamo kuwa haitakuwa rahisi kwa makundi hayo kusalimisha silaha zao ikiwa hayatashawishika kwamba maslahi yao yatatiliwa maanani na serikali ya Kongo.

Wanatoa mfano kwamba kwa sasa Uganda inashirikiana na Kongo katika operesheni nyingine ya kutokomeza kundi la waasi la ADF na hapajakuwa na muundo wowote wa kuwataka waasi hao kusalimisha silaha zao wala kushiriki mazungumzo.

Kulingana na takwimu za mizozo na siasa eneo la Maziwa Makuu, kuna makundi 120 ya wapiganaji mashariki mwa Kongo, ambapo miongoni mwao ni waasi wanaopinga tawala za Rwanda na Burundi.

Imetayarishwa na Lubega Emmanuel/DW Kampala

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW