1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uganda yawafunga jela askari waliowapiga wanahabari

18 Februari 2021

Jeshi la Uganda limetoa adhabu ya kifungo gerezani kwa askari wake waliowapiga na kuwajeruhi waandishi habari siku ya Jumatano, baada ya shinikizo na shutma kutoka kwa wadau mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Afrika Uganda Soldaten verurteilt für Gewalt an Journalisten
Picha: Lubega Emmanuel/DW

Aidha, mkuu wa majeshi ameomba radhi kwa jumuiya ya waandishi habari kuhusu kisa hicho akiahidi kuwa serikali itagharamia matibabu ya wote waliojeruhiwa.

Tofauti na visa vya awali ambapo majeshi na polisi wamewashambulia wanahabari na kutochukuliwa hatua zozote, safari hii wakuu katika jeshi hilo wameitikia malalamiko ya umma kwa kuwaadhibu mara moja askari waliohusika.

Soma zaidi: Polisi Uganda wawapiga waandishi habari

Kundi la askari waliokuwa wamejihami kwa bunduki, rungu na viboko walishuhudiwa waziwazi wakiwapiga wandishi habari waliokuwa wakifuatilia tukio la mwenyekiti wa chama cha upinzani cha NUP, Robert Kyagulanyi akiwasilisha malalamiko katika ofisi za shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia haki za binadamu. Naibu Msemaji wa majeshi Luteni kanali Deo Akiiki amesema saba kati yao wamehukumiwa kifungo cha siku tisini huku wengine watatu wakipata adhabu ya kifungo cha miezi sita na onyo kali.

Mkuu wa majeshi Uganda, Jenerali David MuhooziPicha: DW/E. Lubega

Awali, katika kikao cha waandishi habari alichoitisha asubuhi ya Alhamisi, mkuu wa majeshi Jenerali David Muhoozi alitangulia kwa kuiomba radhi jumuiya ya wanahabari, vyombo vya habari na umma kwa jumla kufuatia kitendo hicho ambacho kimeendelea kulaaniwa ndani na nje ya nchi hata kwenye vikao vya Umoja wa Mataifa na mikutano mbalimbali ambayo imekuwa ikifanyika sehemu zingine za dunia.

Pigo kwa utawala wa Rais Museveni

Lakini kulingana na wadadisi wa mambo ya kisiasa na kijamii, kisa hicho kimekuwa pigo kubwa kwa utawala wa Rais Yoweri Museveni ambaye mara kadhaa amekanusha kuwa vyombo vya usalama vinakiuka haki za binadamu kwa kuwatesa raia wasio na hatia ikiwemo waandishi habari na yeyote ambaye anaukosoa utawala wake.

Wanaelezea kuwa huu ni ushahidi halisi ambao siku zote utatumiwa kushtumu vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu nchini Uganda. Wakati huo huo, fundi mitambo wa aliyekuwa mgombea urais wa upinzani Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, Selector Davie amesimulia jinsi alivyoteswa baada ya kutekwa nyara na kuzuiliwa sehemu mbalimbali kwa zaidi ya mwezi mmoja. Hayo ameyaeleza wakati akihojiwa na DW.

Kulingana na malalamiko yaliyowasilishwa na Bobi Wine katika Umoja wa Mataifa, wengi wa watu waliokatekwa nyara na kuzuiliwa bila kufikishwa mahakamani ni wafuasi wake.