Uganda yawashtaki watano jaribio la mauaji ya waziri
8 Julai 2021Wanaume waliopanda pikipiki walifyatrua risasi kadhaa kwenye gari lililombeba waziri, Katumba Wamala, wakati akiendesha kupitia kitongoji cha mji mkuu Kampala mapema asubuhi Juni 1.
Shambulio hilo lilimuua binti yake Katumba ambaye alikuwa naye katika gari pamoja na dereva wake. Katumba aliumia wakati mlinzi wake alitoka bila kujeruhiwa na alisifiwa kwa kuokoa maisha yake.
Waraka wa mashtaka uliyotolewa na mahakama mnamo Alhamisi ulionyesha wanaume wengine watano walikuwa wameshtakiwa kwa makosa mengi yaliyotokana na shambulio hilo. Wanaume wawili walikuwa tayari wameshtakiwa kuhusiana na shambulio hilo.
Lengo la shambulio hilo lilikuwa "kutisha umma au sehemu ya umma na ya kisiasa, kidini, kijamii na sababu za kiuchumi, kulingana na waraka huo wa mashtaka.
Wiki iliyopita polisi walisema wanaume hao walipata mafunzo katika kambi katika jimbo la Kivu Kaskazini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inayoendeshwa na kundi la waasi wa Allied Democratic Forces (ADF).
ADF inadai uhusiano na kundi linalojiita Dola la Kiislamu (IS). Kundi hilo la waasi awali lilianzia Uganda lakini sasa linaendesha operesehni zake katika misitu ya mashariki mwa DRC.
Polisi wamesema wakati wa upekuzi wa nyumba ya mmoja wa washukiwa, kwamba vifaa vilivyotumika kutengeneza vilipuzi vilipatikana, na vile vile miongozo ya mafunzo ya al-Qaeda juu ya jinsi ya kutengeneza na kulipua mabomu.
Kumekuwa na mauaji zaidi ya dazeni ya watu mashuhuri katika nchi hiyo ya Afrika mashariki katika muongo mmoja uliopita na mengi yake, ambayo kawaida hufanywa na wanaume wanaoendesha pikipiki, hayajawahi kutatuliwa.