1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uganda:Maagizo ya kudhibiti corona yachanganya umma

Admin.WagnerD7 Juni 2021

Maagizo ya Rais Yoweri Museveni wa Uganda ya kusitisha baadhi ya shughuli za umma kwa siku 42 ili kukabiliana na kasi ya kusambaa kwa ugonjwa wa COVID-19 yamepokelewa kwa maoni mbalimbali nchini humo.

Tansania Chato 2020 | Yoweri Museveni, Präsident Uganda
Picha: Tanzania State House/Xinhua News Agency/picture alliance

Maagizo ya Rais Yoweri Museveni wa Uganda ya kusitisha baadhi ya shughuli za umma kwa siku 42 ili kukabiliana na kasi ya kusambaa kwa ugonjwa wa COVID-19 yamepokelewa kwa maoni mbalimbali nchini humo. Miongoni kwa maagizo aliyotangaza jana usiku ni kufungwa kwa shule na taasisi za elimu pamoja na usafiri wa umma kutoruhusiwa kuvuuka mipaka ya wilaya. 

Baada ya kushauriana na wanasayansi na wakuu katika wizara ya afya kwa siku kadhaa kufuatia wimbi jipya la mripuko wa COVID-19, hatimaye Rais Museveni ametangaza maagizo ya kudhibiti kasi ya maambukizo ya ugonjwa huo. Maagizo hayo ambayo yanatakiwa kufuatwa kwa muda wa siku 42 yanalenga kuzuia mikusanyiko ya watu pamoja na matembezi kutoka wilaya moja hadi nyingine.

Alisema "Hii leo shule zingewapokea wanafunzi wa madarasa ya chini ambao wamekuwa nyumbani kwa muda wa zaidi ya miezi 14, lakini badala yake wanafunzi wote wa shule na taasisi za elimu watatakiwa kurudi makwao na kusubiri kwa muda huo wa siku 42 kurejea masomoni." 

Hatua hiyo inamaanisha kwamba wanafunzi wa taasisi zote za elimu watalazimika kusubiri kwa siku nyingine 42, na kuibua malalamiko mengi.Picha: Imago/Zuma Press

Baadhi ya wanafunzi wa vyuo vikuu pamoja na walimu wa shule ambao wameathirika kutokana na agizo hilo linalolenga kudhibiti kusambaa kwa COVID-19. Miongoni mwao wamesema "Mimi mwenyewe naona tayari nimekata tamaa", lakini hakuwa peke yake aliyelalama bali huyu hapa naye alikuwa na haya "Kwanza kabisa kuna wanafunzi ambao tayari wamelipa ada za shule ambazo hawataweza kurudishiwa. Tukienda kijijini hao watu watakuwa wanapata shida, wataambukizwa virusi vya COVID-19". 

Soma Zaidi: Corona: Uganda yaanza zoezi la utoaji chanjo

Baada ya kushughulika kuwarudisha wanafunzi makwao, usafiri wa umma kutoka wilaya moja hadi nyingine utasitishwa siku ya Alhamisi. Hii  ina maana kuwa hata usafiri wa abiria kutoka mataifa jirani ambao ulikuwa umeanza tena umeathirika kufuatia agizo hilo. 

Kwa mujibu wa kanuni hizo, ni watu 20 tu watakaoruhusiwa kuhudhuria shughuli za kijamii kama vile harusi, maziko na kadhalika. Shughuli za viwanda, masoko, uchukuzi wa bidhaa pamoja kilimo zitaendelea lakini kwa kufuata kanuni za kudhibiti maambukizo ya virusi vya Corona, ila maduka yatatakiwa kufunga saa moja jioni.

Huku makanisa na misikiti ikiagizwa kufunga milango yao, nyumba za wageni na madanguro yameruhusiwa kuendelea na biashara. Rais Museveni ameongezea kuwa safari hii, atakayevunja sheria hizo atatozwa faini ya papo kwa papo badala ya kukamatwa na kufungwa. Kwa namna hii wataepusha msongamano katika magereza na mahabusu.

Lubega Emmanuel/DW Kampala