1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ughali wa maisha wafikia asilimia milioni 1 Venezuela

Sekione Kitojo
26 Julai 2018

Hali ya kiuchumi Venezuela inakaribia kuwa mbaya sana. Iwapo hali hiyo inaweza kuilazimisha serikali kufungua zaidi uchumi, kitu kimoja ni hakika ughali wa maisha uliofikia asilimia milioni moja utaleta maadhila zaidi.

Venezuela Bolivar Banknote Geldschein Währung
Picha: picture-alliance/dpa/F. Batista

Mapema  wiki  hii , shirika  la  fedha  la  kimataifa  IMF limetoa viwango  vinavyotisha, likifanya  marekebisho  kwa  makadirio  yake kwamba  ughali  wa  maisha  utafikia  asilimia  14,000 katika  idadi ambayo  imeongezeka  kwa  karibu  mara  70. Tayari, umasikini unafikia  viwango  ambavyo  havivumiliki, watu  wanaokadiriwa kufikia  milioni  1.6 wameikimbia  nchi  hiyo , vurugu za  kijamii zinaongezeka  miongoni  mwa  wale  waliobakia, mishahara imekuwa  karibu  haina  thamani  tena, kuna  upungufu  wa  chakula na  madawa, na  bado  rais Nicolas Maduro  anaendelea kung'ang'ania  madarakani.

Maandamano ya kuipinga serikali mjini CaracasPicha: picture-alliance/ZUMAPRESS.com

"Hakuna  kitu  kinachonishangaza," Marcos  Salazar  aliliambia shirika  la    habari  la  afp  baada  ya  kuambiwa  kuhusu makadirio hayo  ya  IMF wakati  akila  mkate  huku  akiwa  amesimama  katika kioski  mtaani.

Mkate  huo  na  nyama  unagharimu  kiasi  cha  boliva milioni  tano sarafu  ya  Venezuela  kiasi  ya  dola  1.5  katika  soko  la  chini  kwa chini , ikiwa  na  thamani  ya  mshahara  wa  mwezi  mmoja, ambao unalipwa  kwa  kutumia vocha  za  chakula.

Kila  wiki , kila  siku , vitu  vinaongezeka  bei. Sio  kwa  taratibu , bei zinalipuka,"  aliongeza  Salazar , profesa  mwenye  umri  wa  miaka 31  anayefanyakazi   tatu, ambazo  bado  hazitoshi  kuweza kumfanya  amudu  maisha  yeye  pamoja  na mpenzi  wake.

Wanaishi kutokana  na  pesa  zinazotumwa  na  ndugu  ambao wamekimbia  nchi  hiyo.

Ughali  huo  mkubwa  wa  maisha sio  tu  umechangia  katika upungufu  wa  chakula  na  madawa  lakini  pia  kuporomoka  kwa huduma  za  umma , ikiwa  ni  pamoja  na  maji, umeme  na  usafiri.

Waandamanaji wahudumu wa afya wakipaaza sauti zao wakidai mishara bora zaidi Picha: picture-alliance/ZUMAPRESS.com

Mageuzi ya kisiasa

Mtaalamu  Henkel Garcia  wa  washauri wa  kiuchumi , Econometrica, anaamini Venezuela  inahitaji  kwa  udi  na  uvumba mageuzi  ya  kisiasa  na  kijamii  ili kuweza  kufanikisha  uthabiti wa wastani.

"Unaweza  tu  kukimbia  kutoka  katika  ughali  huu  mkubwa  wa maisha  kupitia  mageuzi  makubwa  ya  sera  za  kiuchumi," aliliambia  shirika  la  habari  la  afp, akielekeza  katika  mifano  ya Ujerumani  katika  miaka  ya  1920  na  Zimbabwe  katika  miaka  ya 2000.

Umasikini  umepanda   hadi  asilimia  87  katika  mwaka  2017 na umasikini  wa  kupindukia  umefikia  asilimia  61 , kwa  mujibu  wa kundi  la  vyuo  vikuu  vya  Venezuela.

Rais wa Venezuela Nicolas MaduroPicha: picture-alliance/epa/Miraflores Presidential Palace

Kundi  hilo  limesema  sita  kati  ya  watu 10  wanadai  wapoteza wastani  wa  kilo  11  kutokana  na  njaa. Serikali  ya  Maduro inakataa  tarakimu  hizo , ikidai kwamba  umasikini  uliokithiri  uko katika  asilimia  4.4 tu.

Venezuela,  hata  hivyo , inategemea  mauzo  ya  mafuta  ambayo yanafanya  kiasi  ya  asilimia  96  ya  mapato , lakini  uzalishaji umepungua  na  kuwa  katika  kiwango  cha  chini  kabisa  katika muda  wa  miaka  30, mapipa milioni 1.5 kwa  siku, kutoka  mapipa milioni 3.2 mwaka  2008, kwa  mujibu wa  shirika  la  mataifa yanayosafirisha  kwa  wingi  mafuta.

makamu wa rais wa Marekani Mike Pence akizungumza na wakimbizi kutoka Venezuela katika kituo cha misaada ya kiutu cha Santa catarina mjini ManausPicha: Getty Images/AFP/R. Oliveira

Hali  hii  imeizuwia  nchi  hiyo  kufaidika na  kupanda  kwa  bei  ya mafuta, wakati  uamuzi  wa  serikali  ya  rais  Maduro kuchapisha fedha  kutokana  na  ukosefu  wa  fedha  za  kigeni umesababisha kudhoofika  kwa  uchumi.

Shirika  la  IMF likihalalisha  makadiro  yake  lilisema  linatarajia serikali  kuendelea  kuchapisha  noti  zaidi , na  kutia nguvu  kasi  ya ughali  wa  maisha  wakati   mahitaji  ya  fedha  yakizidi kuporomoka."

Mwandishi: Sekione  Kitojo / afpe

Mhariri: Yusuf, Saumu

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW