Ugiriki iko hatarini
8 Septemba 2011Waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang Schäuble amesema leo hii hali nchini Ugiriki ni mbaya sana na kwamba nchi hiyo haitopatiwa msaada mpya hadi hapo itakapotimiza masharti ya kifedha iliowekewa na taasisi za mikopo za kimataifa.
Schäuble amekuwa mmojawapo wa mawaziri waandamizi wa serikali ya Ujerumani kuhoji uwanachama wa Ugiriki kwa kanda inayotumia sarafu ya euro barani Ulaya kwa kusema kwamba nchi hiyo lazima itimize masharti yanayohitajika kwa nchi kuwa mwanachama wa kanda ya euro.
Waziri huyo wa fedha wa Ujerumani amesema Ujerumani iko tayari kuisaidia Ugiriki lakini iwapo nchi hiyo haitotimiza masharti yalioyowekwa na Umoja wa Ulaya,Benki Kuu ya Ulaya na Shirika la Fedha la Kimataifa IMF haitopewa mikopo zaidi ya kuisaidia nchi hiyo.
Akizungumza na radio ya Ujerumani ya Deutschland Funk Schäuble amesema anafahamu kwamba kuna upinzani miongoni mwa wananchi wa Ugiriki juu ya hatua za kubana matumizi lakini hatimaye Ugiriki itakuwa inawajibika kutimiza masharti ambayo yanahitajika kwa nchi kuwa mwanachana wa kanda inayotumia sarafu ya euro katika Umoja wa Ulaya.
Schäuble ameongeza kusema kwamba hawawezi kuiregezea masharti nchi hiyo.
Kushindwa kutimiza masharti kwa serikali ya Ugiriki kumeuweka hatarini mpango mpya wa msaada wa mkopo kutoka kwa taasisi za mikopo za kimataifa.
Jambo hilo limewakasirisha baadhi ya wabunge wa Ujerumani wakiwemo wahafidhina wa serikali ya Kansela Angela Merkel ambao wameanza kutowa wito wa kutimuliwa kwa Ugiriki kutoka kanda hiyo ya nchi wanachama 17 wa Umoja wa Ulaya wanaotumia sarafu hiyo ya pamoja ya euro.
Mkuu wa chama cha Christian Social Union mojawapo ya vyama vitatu vinavyounda serikali ya mseto ya Merkel ameongezea sauti yake katika mdahalo huo hapo jana kwa kusema kwamba hafuti uwezekano kwa Ugiriki kuondoka katika kanda hiyo inayotumia sarafu ya euro.
Duru za kanda ya Euro zimeliambia shirika la habari la Uingereza Reuters kwamba Ugiriki inabidi ilipe fidia kwa nakisi yake ya bajeti ya mwaka 2012 na katika maeneo mengine ya mageuzi iliyokubaliana na mashirika ya mikopo ya kimataifa ili kuweza kupatiwa mkopo mpya wa msaada wa kuinusuru nchi hiyo na madeni.
Waziri wa fedha wa Ujerumani pia ameitaka Italia kuchukuwa hatua zaidi kupunguza nakisi yake ya bajeti.
Wakati huo huo Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Manuel Barosso amesema sarafu ya euro itaibuka katika mzozo wa hivi sasa ikiwa imara zaidi na kwamba wale wanaofikiri kwamba sarafu ya euro itasambaratika hawafahamu juu ya uimara wa umoja wao.
Akihutubia katika chuo kikuu cha Auckland nchini New Zealand Barosso amesema sarafu ya euro sio tu inahusika na ujenzi wa kifedha bali ni mradi wa kisiasa unaojumuisha takwa la wananchi wa Ulaya kushirikiana mustakabali wao.
Mwandishi: Mohamed Dahman/RTRE/dpa
Mhariri:Josephat Charo