Ugiriki kutakiwa kuamua kubakia au kutoka kwenye Euro
2 Novemba 2011Bado hakijajuilikana kitakachoamuliwa baada ya mazungumzo baina ya Kansela Angela Merkel wa Ujerumani, Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa, Mkuu wa Shirika la Fedha la Kimataifa, (IMF), Christine Lagarde na Waziri Mkuu Papandreou jioni hii.
Hata hivyo, tayari Kansela Merkel ameshadokeza kile kinachoweza kutegemewa kwenye mazungumzo hayo. Akizungumza kwenye mkutano wa pamoja kati yake na Waziri Mkuu wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, hivi leo jijini Berlin, ametaka utekelezwaji wa mpango wa kuiokoa Ugiriki kama ulivyokubaliwa kwenye mkutano wa wiki iliyopita wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels.
"Tulikubaliana mpango huo wiki iliyopita. Tunachohitaji sasa ni uwazi katika utekelezaji wake." Amesema Kansela Merkel.
Kwa upande mwengine, tayari Ujerumani imesema kuwa fedha zilizokuwa ziende Ugiriki, zitakawia kwa muda. Msemaji wa Kansela, Steffen Seibert, ameliambia shirika la habari la Ujerumani (DPA) kwamba hakutakuwa na malipo yatakayofanywa hadi baada ya mkutano wa mawaziri wa fedha wa Umoja wa Ulaya utakaofanyika Jumatatu ijayo.
Wizara ya Fedha ya Ujerumani nayo inasema kwamba taarifa walizopata kutoka Ugiriki zinasema kuwa nchi hiyo haitahitaji fedha hizo hadi mwezi ujao.
Hivi leo, bei za hisa za makampuni zimeporomoka Ulaya nzima baada ya tangazo hili, huku ikihofiwa kwamba kama Wagiriki wataukataa mpango wa uokozi wa madeni kutoka Umoja wa Ulaya, sio tu Ugiriki itafilisika, bali pia eneo zima la sarafu ya euro litaingia kwenye pata-potea, kwani itamaanisha kujiondoa Ugiriki kwenye umoja wa sarafu hiyo.
Katika mkutano wa viongozi hao wanne jioni hii, Sarkozy anatarajiwa kumuambia Papandreou waziwazi kwamba kura ya maoni ya Ugiriki iwe ni kuhusu ama Ugiriki kubakia au kujitoa kwenye sarafu ya euro.
Waziri anayeshughulikia masuala ya Ulaya nchini Ufaransa, Jean Leonetti, ameakiambia kituo cha televisheni cha LCI, kwamba ni ama Ugiriki kuukubali mpango wa uokozi na mshikamano wake na Ulaya "au kuihama euro na kurudi kwenye sarafu yake na kujitangaza muflisi."
Waziri wa Fedha wa Ujerumani, Wolfgang Schaeuble, ameliambia gazeti la leo la Hamburger Abendblatt kwamba litakuwa jambo la maana sana kama uamuzi halisi wa Ugiriki ungelijuilikana na mapema zaidi.
Nchini Ugiriki kwenyewe, ambako mapema leo Baraza la Mawaziri lililunga mkono pendekezo la Papandreu la kura ya maoni, wananchi wamegawika kuhusiana na hili, huku wengine wakisema kwamba ilikuwa waulizwe tangu mwanzo na sio leo hii, ambapo maji yameshazidi unga.
"Huu wanaoufanya ni upuuzi. Wangelituuliza mwanzo kabla hawajaenda Shirika la Fedha la Kimataifa na kuamua kututoa sadaka. Wangelifanya hivyo tangu mwanzo, leo tusingekuwa na kiwango hiki cha madeni." Amesema mkaazi mmoja mji mkuu wa Athens.
Mkaazi mwengine wa Athens amesema kwamba ni bora serikali nzima ya Papandreou ikaondoka madarakani. "Kama wataondoka mapema, ndivyo Ugiriki itakavyojikwamua mapema pia."
Pamoja na hayo, kura ya maoni iliyoendeshwa wiki hii nchini Ugiriki inaonesha kuwa Wagiriki wengi hawafurahishwi na mpango huu wa kuiokoa kutoka wimbi la madeni uliokubaliwa na Umoja wa Ulaya. Kwa wengi, mpango huu ni wa kuziokoa benki na sio maisha ya mtu wa kawaida.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AP/DPA/AFP
Mhariri: Othman Miraji