Ugiriki kuwafukuza wahamiaji walioingia baada ya Machi mosi
5 Machi 2020Maelfu ya wahamiaji wameelekea Ugiriki tangu Uturuki ilipotangaza hapo Februari 28 kuwa itawafungulia wahamiaji watumie mipaka yake kuelekea Ulaya licha ya taifa hilo kukubali kuwahifadhi wahamiaji hao chini ya mkataba wa mwaka 2016 na Umoja wa Ulaya
Mamima ya wahamiaji wameingia Ugiriki kupitia baharini kuelekea Lesbos na visiwa vingine vya Ugiriki. Nchi hizo mbili, Uturuki na Ugiriki zinatuhumiana kwa kutumia nguvu kubwa katika mpaka kati yao ambapo wahamiaji wamekuwa wakipambana na vikosi vya usalama katika siku za hivi karibuni. Ugiriki ilitangaza Machi mosi kuwa haitapokea maombi yoyote ya hifadhi ya ukimbizi kwa kipindi cha mwezi mmoja kutokana na kuwepo kwa mzozo wa wahamiaji walioko mpakani.
Wakimbizi kadhaa wamekwama katika mpaka huo kati ya Ugiriki na Uturuki na wanateseka kwa baridi, maraadhi na hali ya kukata tamaa kutokana na kukosa mahala pa kuishi na pia wanakabiliwa na ukosefu wa mahitaji ya msingi. Ugiriki na Umoja wa Ulaya wanailaumu Uturuki kwa kuwachochea wakimbizi kuvuka mpaka kama njia moja ya kuishinikiza jumuiya ya Umoja wa Ulaya itoe fedha zaidi au iiunge mkono Uturuki katika mzozo wa na Syria.
Utulivu umerejea kwenye eneo la mpakani la Kastanies nchini Ugiriki ingawa bado upo wasiwasi kutokana na hatua ya polisi wa Ugiriki ya hapo siku ya Jumatano, jinsi walivyotumia nguvu kukabiliana na wakimbnizi waliojaribu kuingia nchini humo kutokea Uturuki. Ugiriki inawahifadhi mamia ya wakimbizi visiwani na bara kwenye nchi hiyo.
Hali hiyo kwa jumla imeutumbukiza Umoja wa Ulaya kwenye harakati za kutafuta njia za kuzuia kuibuka tena ongezeko la wakimbizi miaka minne tangu jumuiya hiyo ilipofikia makubaliano na Uturuki.
Vyanzo:RTRE/DPA