Ugiriki kuwasilisha orodha mpya ya mageuzi
20 Machi 2015Hii ni baada ya Waziri Mkuu Alexis Tsipras kufanya mazungumzo ya dharura na viongozi wakuu wa Ulaya pembezoni mwa Mkutano wa Kilele wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels. Bruce Amani ana ripoti kamili.
Taarifa iliyotolewa punde baada ya mkutano huo wa jana usiku imesema Ugiriki imekubali kumalizia haraka iwezekanavyo kazi ya kuukamilisha mpango wa uokozi wa Umoja wa Ulaya na Shirika la Fedha Ulimwenguni – IMF, ili kuiwezesha serikali yake kupewa fedha hizo muhimu za kuiepusha kufilisika na uwezekano wa kuondoka katika kanda ya sarafu ya euro.
Kiongozi wa Ugiriki wa siasa kali za mrengo wa kushoto Alexis Tsipras alikaa meza moja kwa karibu saa tatu, na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, Rais wa Ufaransa Francois Hollande na viongozi wakuu wa Umoja wa Ulaya pembezoni mwa mkutano wa kilele mjini Brussels. "Tuna matumaini zaidi baada ya mazungumzo haya. Nadhani pande zote zimethibitisha nia yao ya kujaribu zinavyoweza kuyatatua matatizo ya uchumi wa Ugiriki haraka iwezekanavyo".
Merkel – akiwa kiongozi wa taifa kubwa kiuchumi barani Ulaya ameongoza juhudi za kuifanya Ugiriki kuheshimu majukumu yake – amesema yeye na Hollande “wamekubaliana kikamilifu” na muafaka huo. "Kwa mara nyingine serikali ya Ugiriki itajitwika jukumu la kufanya mageuzi na katika siku chache zijazo itatukabidhi orodha kamili ya hatua maalum. Tumejitolea katika mchakato huu wa tathmini na hiyo ni kusema kuwa mazungumzo ya kisiasa ya taasisi yatafanyika Brussels na ujumbe wa ukaguzi utaendelea Athens".
Wakopeshaji wa Ugiriki walikubaliana mwezi Februari kurefusha mpango wake wa uokozi wa euro bilioni 240, baada ya serikali mpya ya Tsipras kutoa ahadi za kutekeleza mageuzi ya kupunguza gharama za matumizi nchini humo.
Serikali ya Ugiriki inataka ipewe kitita cha fedha zizosalia cha euro bilioni saba ili iendelee kujikimu, lakini Umoja wa Ulaya unataka kuona utekelezwaji wa ahadi za mageuzi.
Mkutano huo wa Ugiriki pia ulihudhuriwa na Rais wa Umoja wa Ulaya Donald Tusk, Mkuu wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Juncker, Mkuu wa Benki Kuu ya Ulaya Mario Draghi na Jeroen Dijsselbloem, waziri wa fedha wa Uhilanzi ambaye ni mwenyekiti wa kundi la nchi zinazotumia sarafu ya euro
Viongozi hao wa UIaya wakati huo huo walikubaliana kuwa vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Urusi kuhusiana na mgogoro wa Ukraine vinapaswa kuendelea kutekelezwa mpaka mwisho wa mwaka huu.
Tusk amesema muda huo utahusishwa wazi na utekelezwaji kamili wa mikataba ya amani iliyosainiwa mjini Minsk mwezi Februari. Uamuzi wa mwisho halali wa kisheria kuhusu kama vikwazo hivyo vitarefushwa au la utafanyika katika mkutano ujao wa kilele mwezi Juni.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Gakuba Daniel