Ugiriki yaadhimisha miaka 50 ya demokrasia
24 Julai 2024Wakati eneo la kusini mwa ulaya likikabiliwa na wimbi la joto kali, Ugiriki iliadhimisha kumbukumbu ya miaka 50 ya kurejeshwa kwa demokrasia yake kwa kuandaa sherehe rasmi, maonyesho, matamasha na kuchapisha sarafu ya euro 2 ya ukumbusho.
Ugiriki ilikuwa na sababu zote za kusherehekea siku hiyo kwa sababu demokrasia haijawahi kuwa imara kwa muda mrefu katika historia ya hivi karibuni ya taifa hilo.
Walakini, huo ulikuwa ni wakati wa kutafakari kwa sababu kurejeshwa kwa demokrasia mnamo mwaka 1974 kufuatia kuanguka kwa utawala wa kijeshi, kunahusishwa pia na mgawanyiko wa kisiwa cha Cyprus ambao unaendelea hadi leo hii.
Soma: Serikali ya Ugiriki yakabiliwa na shinikizo la kuondolewa
Mnamo Julai 15, 1974, kundi la makanali wa kijeshi lililonyakua mamlaka huko Ugiriki miaka saba iliyopita, lilifanya mapinduzi katika kisiwa cha Cyprus, na kuipindua serikali ya Askofu Mkuu Makarios III, aliyekuwa rais wa Cyprus wakati huo.
Kwa kuhofia kwamba Ugiriki ingeliweza kutanua udhibiti wake kwenye kisiwa hicho, Uturuki iliivamia Cyprus na hatimaye kuchukua udhibiti wa karibu asilimia 36 ya kisiwa hicho na kusababisha mgawanyiko unaoshuhudiwa hii leo hadi katika mji mkuu wa Cyprus Nicosia.Jaji Ugiriki awaachia huru watuhumiwa wa kuzamisha meli
Kufuatia kushindwa kwa jeshi huko Cyprus, jeshi la Ugiriki lilisambaratika huku jeshi la wanamaji ambalo lilikuwa muhimu kwa utawala wa kijeshi lilimwondoa madarakani kiongozi wao, Dimitrios Ioannidis.
Mwanzo mpya wa iutawala wa kidemokrasia
Mnamo Julai 23, 1974, wanajeshi walikabidhi mamlaka kwa serikali ya kiraia, na siku moja baadaye yaani Julai 24, Waziri Mkuu wa zamani Konstantine Karamanlis alirejea kutoka uhamishoni nchini Ufaransa na kuwasilisha baraza lake jipya la mawaziri.
Ingawa matukio ya Cyprus ndiyo kwa kiasi fulani yalisababisha kuanguka kwa utawala wa kijeshi huko Ugiriki, kulikuwa tayari kumeshuhudiwa matukio kadhaa ya kuupinga utawala wa kidikteta wa jeshi.Ugiriki yaahidi msaada zaidi kwa visiwa vya Crete na Gavdos
Upinzani huo ulifikia kilele chake wakati wa ghasia za wanafunzi katika mji mkuu wa Ugiriki, Athens ambazo zilizimwa kikatili na jeshi mnamo Novemba 17, 1973. Wagiriki wengi walilazimika kukimbilia uhamishoni nje ya nchi. Idhaa ya Ugiriki ya Deutsche Welle ilikuwa ndio chombo kinachowapa kauli vuguvugu la upinzani dhidi ya utawala wa kijeshi.
Ugiriki: Demokrasia yenye nguvu na thabiti
Wiki hii, Ugiriki inaaadhimisha kumbukumbu ya kuangushwa kwa utawala wa udikteta wa kijeshi na kusherehekea kwa fahari miaka hiyo 50 ya kurejeshwa kwa demokrasia.
Soma pia: Waandishi habari Ugiriki wagoma kwa saa 24 kulalamikia mishahara duni
Kwa wiki kadhaa sasa, wanasiasa, wataalamu wa masuala ya sheria, wanahistoria, wataalam wa kisiasa, wasanii na waandishi wa habari wamekuwa wakielezea kile wanachokiona kama mafanikio na changamoto za taifa hilo kwa miongo mitano iliyopita.
Hadi sasa watu bado wanazungumza jambo linalofahamika kama "Metapolitefsi," inayomaanisha "kipindi cha mpito", kana kwamba uimara wa demokrasia ya Ugiriki bado upo mashakani. Lakini nchi hiyo ni tulivu, yenye nguvu na thabiti licha ya misukosuko mingi ya kisiasa na kiuchumi iliyoshuhudiwa katika kipindi cha miaka 50 iliyopita.Waziri mkuu wa Ugiriki Mitsotakis aapishwa muhula wa pili
Mambo muhimu ya kuzingatia ni kwamba jeshi limeondolewa na halijihusishi kabisa katika siasa. Mfalme aliondolewa madarakani na jeshi mnamo Desemba 1967 na hakurudi tena hata baada ya utawala wa kijeshi kuondolewa.
Makovu ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vya mwaka 1944 hadi 1949 yameanza kupona, huku mfumo wa bunge ukiwa unafanya kazi vizuri kwa zaidi ya nusu karne. Pia, mabadiliko ya serikali yatokanayo na uchaguzi wa kidemokrasia ni kielelezo cha uimara wa demokrasia nchini Ugiriki.