1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ugiriki yapambana na mioto mikubwa ya msituni

26 Julai 2023

Ugiriki inakabiliwa na kitisho cha joto la kupindukia hii leo wakati mioto za msituni ikizidi kushika kasi, huku marubani wawili wakiripotiwa kufariki, baada za ndege waliyokuwa wakitumia kuzima moto kuanguka.

Satellitenaufnahme Griechenland Waldbrände | Korfu
Picha: MAXAR TECHNOLOGIES/REUTERS

Vikosi vza wazima moto vimeendelea kupambana kuidhibiti mioto hiyo ambayo pia imeleta athari kwenye mataifa mengine ya ukanda wa Mediterania. 

Maelfu ya watu tayari wamehamishwa, wakati Mamlaka nchini Ugiriki zikihangaika kukabiliana na mioto mikubwa katika maeneo matatu nchini humo ambayo ni visiwa vya Rhodes na Corfu na Evia. Mioto pia imeshuhudiwa nchini Croatia na Italia na tayari imesababisha vifo vya watu kadhaa nchini Algeria mapema wiki hii.

Viwango vya joto vinatarajiwa kufikia nyuzi joto 43 hadi 45 katikati na kusini mwa Ugiriki, hii ikiwa ni kulingana na shirika la kitaifa la masuala ya hali ya hewa nchini humo. Licha ya taifa hilo kukabiliwa na mawimbi ya kila mara ya joto kali, lakini kwa sasa linashuhudia moja ya hali mbaya kabisa na ya muda mrefu kuwahi kushuhudiwa katika miaka ya karibuni, wataalamu wanasema.

Soma Zaidi: Waziri mkuu wa Ugiriki aunda kikosi maalum kukabili moto

Ndege ya kikosi cha zimamoto ikimwaga maji katika kijiji cha Gennadi kinachoungua, kufuatia moto mkubwa kwenye kisiwa cha RhodesPicha: Nicolas Economou/REUTERS

Wizara ya ulinzi wa raia imeonya juu ya kitisho kikubwa cha moto katika mataifa sita kati ya 13 ya ukanda huo, huku wanasayansi kutoka taasisi ya kimataifa ya hali ya hewa ya World Attribution Group wakisema shughuli ya binaadamu ndizo zimechangia pakubwa kutokea kwa hali hiyo iliyochochewa na joto kali, ambalo pia limeyakumba baadhi ya maeneo ya Ulaya na Amerika ya Kaskazini.

Baadhi ya wakazi katika visiwa vya Corfu na Rhodes ambako kumeshuhudiwa madhara makubwa, wanasema sio rahisi hata kidogo wakati huu wanapoangalia namna ya kuanza tena kusimamisha biashara zao. Miongoni mwao ni Vasilis Sofitsis aliyekuwa anamiliki biashara ya ujenzi katika kisiwa cha Corfu ambaye amesema, "Ni janga. Kwa sababu chanzo kikuu cha mapato katika kisiwa hiki ni utalii. Lakini kwa kuwa sasa hivi shughuli za kitalii zimesitishwa na watu wanaogopa kuja kutembea, kwa hakika litakuwa janga kwenye kisiwa hiki na kila kisiwa cha Ugiriki."

Msemaji wa kikosi cha zimamoto amesema kulishuhudiwa mioto mikali kabisa hapo jana ikiharibu visiwa vya Corfu na Rhodes ambavyo vyote ni maarufu kwa utalii.

Maelfu ya watu wamehamishwa katika baadhi ya maeneo nchini Algeria, kutokana na kitisho kinacholetwa na moto mkubwa wa nyikaniPicha: FETHI BELAID/AFP/Getty Images

Karibu wazimamoto 100 sasa wapo katika kisiwa cha Evia wakipambana kutwa kucha kuuzima moto. Huko ndiko kulikotokea ajali ya ndege ya wazima moto na kusababisha vifo vya marubani wawili baada ya ndege hiyo kuanguka wakati ilipogongana na ndege nyingine iliyokuwa inamwaga maji. Mwili wa muhanga wa tatu pia uliokotwa kwenye kisiwa hicho.

Tayari mamlaka zimewahamisha maelfu ya raia na watalii. Nchini Algeria ambako pia kumeshuhudiwa athari za moto, watu 34 wamefariki dunia baada za makazi yao kuungua na maelfu pia wamehamishwa.

Huko Italia, wazima moto wamekuwa wakipambana kwa usiku mzima kuuzima moto unaoshika kasi katika eneo la Sicily, linalopakana kwa karibu na uwanja wa ndege wa Palermo ambao ulisimamisha shughuli zake jana asubuhi. Eneo la kusini mwa taifa hilo ndio hasa limeshuhudia janga hilo, hii ikiwa ni kulingana na wizara ya ulinzi wa raia. Msichana mmoja wa miaka 16 amefariki katika eneo la kaskazini baada ya kuangukiwa na mti kutokana na upepo mkali.

Mamia ya wazima moto pia wanahangaika na kuudhibiti moto katika mji wa kusini mwa Croatia wa Dubrovnik, na mamlaka zimesema mapema leo kwamba tayari wametuma ndege na mabomba ya maji kusaidia kuuzima.

Soma Zaidi: Joto kali lasababisha maafa ya moto kwenye nchi kadhaa Ulaya