1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ugiriki yapata mkopo mpya

Josephat Nyiro Charo21 Februari 2012

Baada ya zaidi ya muda wa masaa 12 ya mazungumzo mjini Brussels, Ubelgiji, nchi zinazotumia sarafu ya euro zimekubaliana mapema leo kuipa Ugiriki mkopo mpya wa Euro bilioni 130 ili kuiepusha isifilisike mwezi ujao.

Greek Prime Minister Lucas Papademos, left, and European Commission President Jose Manuel Barroso participate in a media conference at EU headquarters in Brussels, on Monday, Nov. 21, 2011. Papademos is on a one day visit to meet with EU officials. (Foto:Virginia Mayo/AP/dapd)
Waziri mkuu wa Ugiriki, Lukas Papademos, kushoto, na rais wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya, Jose Manuel BarrosoPicha: dapd

Kanda ya Euro na shirika la fedha la kimataifa, IMF, zina matumaini mkopo huo mpya utaiwezesha Ugiriki kurudi katika nafasi ambapo itaweza kuhimili hali ngumu ya kiuchumi bila ya msaada kutoka nje na kuhakikisha inalinda nafasi yake katika kanda hiyo. Mawaziri wa fedha kutoka Ugiriki na mataifa mengine 16 ya eneo linalotumia sarafu ya Euro wamefanya mazungumzo marefu hadi leo alfajiri kuhusu vipi lengo hilo litakavyofikiwa.

Makubaliano yaliyopatikana yananuia kupunguza deni kubwa la Ugiriki katika kila nyanja, huku wakopeshaji binafsi na wale rasmi wakifanya kazi ya ziada kuliko yale waliyokuwa wakisema yanawezekana.

Mkuu wa shirika la IMF, Christine Lagarde, amesema mpango huo si rahisi na malengo yake ni makubwa. Lagarde aidha amesema kuna uwezekano ulio dhahiri kwamba uchumi wa Ugiriki huenda usikue sana ikilinganishwa na vile wakopeshaji wa kimataifa wanavyotumai. Hata hivyo ameeleza matumaini yake kwamba sasa Ugiriki inaweza kunyanyuka tena kiuchumi.

"Tunaianza siku hii leo na deni la pato jumla la kitaifa la asilimia 120.5. Kwa hiyo mafanikio makubwa yamepatikana usiku kucha yatakayoiweka Ugiriki katika nafasi nzuri ya kutekeleza mpango ambao imeufanyia mashauriano kwa wiki kadhaa zilizopita."

Shirika la IMF na kanda ya Euro zimesema mkopo huo unatarajiwa kupunguza deni la Ugiriki hadi asilimia 120.5 ya pato jumla la kitaifa kufikia mwaka 2020, kiwango ambacho zinaweza kukihimili. IMF inasubiriwa kuamua kiwango itakachotoa katika mkopo huo kwa Ugiriki. Lagarde amesema bodi ya shirika hilo itaamua mchango wake wiki ya pili ya mwezi ujao.

Hisia zajitokeza

Wakati huo huo, wanasiasa wa Ugiriki wameupongeza mkopo mpya uliotolewa wakisema ni wa msaada mkubwa wa nchi yao iliyoathiriwa vibaya na mdororo wa kiuchumi. Waziri mkuu wa Ugiriki, Lucas Papademos, amesema ni siku ya kihistoria kwa uchumi wa Ugiriki.

"Ni makubaliano mazuri. Wagiriki wamefanya kila walichoweza. Viongozi wa Ulaya wanatimiza jukumu lao la kuwasaidia kama wakopeshaji," amesema Francois Baroin," waziri wa fedha wa Ufaransa.

Kanda ya Euro pamoja na Ugiriki zilikabiliwa na shinikizo la kufikia makubaliano ya haraka kuiepusha Ugiriki isishindwe kulipa deni lake la dhamana za thamani ya Euro bilioni 14.5 kufikia tarehe 20 mwezi ujao. Sarafu ya Euro imeimarika leo dhidi ya dola ya Marekani

Kwa upande mwingine mawaziri wa fedha wa Umoja wa Ulaya wanakutana leo kujadili kuziongezea makali sheria za masuala ya fedha kufuatia uamuzi wa kuipa Ugiriki mkopo mpya. Bunge la Ugiriki nalo linaanza leo mjadala wa kuongeza hatua za kufunga mikaja zinazohitajika kuziba pengo katika bajeti ya mwaka 2012.

Mwandishi: Josephat Charo/APE

Mhariri: Mohammed Abdulrahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW