1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ugonjwa wa Ebola wazua taharuki Uganda

Josephat Charo
14 Oktoba 2022

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wamejishughulisha na mlipuko wa ugonjwa wa ebola nchini Uganda, vifo vya watoto nchini Gambia kutokana na dawa za mafua kutoka India na uasi wa kundi la M3 mashariki mwa Congo.

Uganda Ausbruch von Ebola
Picha: Nicholas Kajoba/AA/picture alliance

Gazeti la Süddeutsche liliandika kuhusu ugonjwa wa ebola nchini Uganda. Mhariri alisema aina ya kirusi cha ebola ambacho ni nadra kimesababisha mrupuko na kuenea nchini Uganda. Wakati wanasayansi walipokuwa wakifanya utafiti na kugundua kirusi cha ebola mnamo 1976 katikati ya msitu wa kitropiki wa Jamhuri ya zamani ya Zaire ambayo sasa ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, waligundua pia aina ya kirusi ambacho kimesababisha asilimia takriban 80 ya milipuko yote ya ugonjwa huo. Pia janga baya la mlipuko wa ebola lililotokea Afrika Magharibi kati ya 2014 na 2016 na lililosababisha vifo 10,000, lilitokana na aina hii ya kirusi cha ebola. Kutokana na janga hilo aina mbili za chanjo na aina mbili za dawa dhidi ya kirusi hicho cha Zaire zilivumbuliwa.

Pia mnamo 1976, watafiti nchini Sudan waligundua aina nyingine ya kirusi cha ebola. Aina hii ya kirusi cha Sudan ni nadra sana, kilikuja kutokea miaka kumi baadaye na mpaka sasa hakuna chanjo wala dawa ya kupambana nacho. Na sasa aina hii ya kirusi cha ebola imerudi tena na kinaenea nchini Uganda. Shirika la Afrika duniani WHO lilitambua kitisho kwamba mlipuko wa ebola unageuka kuwa tatizo kubwa kwa taifa hilo la Afrika Mashariki na unaongezeka. Kitisho cha kusambaa kwa mataifa mengine kwa upande mwingine kiko chini. Hata hivyo Marekani tayari ilikuwa ikiwashauri raia wake wanaorejea nyumbani wapitia viwanja maalumu vya ndege ambako watapimwa kubaini ikiwa wana dalili za ebola.

Madaktari wasio na mipaka wa Uganda wakitengeneza kituo cha kuwatenga wagonjwa wa ebolaPicha: BADRU KATUMBA/AFP via Getty Images

Gazeti la Frankfurter Allgemeine liliandika kuhusu dawa ya mafua kutoka India ambayo inaripotiwa imeua watoto barani Afrika. Kutokana na madai hayo maafisa nchini India wanafanya juhudi kuiokoa sifa ya makampuni yanayotengeneza na kusafirisha dawa katika nchi za kigeni. Vifo vya watoto 66 nchini Gambia baada ya kupewa dawa hiyo ya mafua kutoka India vinaiweka sekta ya kutengeneza dawa ya India katika shinikizo kubwa.

Watoto 66 wafa Gambia kutokana na dawa za mafua

Nalo gazeti la Die Tageszeitung kuhusu mada hii lilikuwa na kichwa cha habari kilichosema: Dawa ya mafua inayoua kutoka India kwa ajili ya watoto wa Gambia. Gazeti lilisema uchunguzi umeshaanza kufuatia vifo vya watoto 66, lakini maafisa wa Gambia wanaamini watoto hao walikufa baada ya kupewa aina nne ya dawa za mafua zilizoagizwa kutoka India. Shirika la afya duniani WHO limeonya kuhusu matumizi ya dawa hizo na yeyote ambaye ameshazitumia anatakiwa amuone daktari mara moja.

Kuzungumza au kupigana? Changamoto inayolikabili kundi la waasi la M23. Ndivyo lilivyoandika gazeti la die Tageszeitung. Nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki zinataka kulisaidia jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo dhidi ya makundi ya waasi. Lakini kwanza panatakiwa pawepo mazungumzo na waasi wa kundi la M23, ambao wanachukuliwa kuwa ni bawa la Rwanda nchini Congo. Jeshi la Congo linasuasua.

Mwandishi wa gazeti la die Tagaeszeitung Simone Schlindwein anasema muungano wa vijana wa Congo LUCHA unachapisha kila asubuhi idadi ya siku ambazo mji wa Bunagana unaopatikana katika mpaka kati ya Congo na Uganda, umeshikiliwa na kundi la M23 linaloongozwa na watutsi. Siku 120. Rais wa M23 Bertrand Bisimwa aliliambia gazeti la die Tageszeitung kwamba wanahakikisha usalama asilimia mia moja, soko na maduka yamefunguliwa, wakulima wanaleta mavuno yao. Maelfu ya wakimbizi wamerejea kutoka Uganda wiki chache zilizopita kuyalima mashamba yao.

Wakimbizi wa Congo katika mpaka wa BunaganaPicha: Guerchom Ndebo/AFP/Getty Images

Waethiopia wafa katika vita Ethiopia

Gazeti la Die Zeit liliripoti kuhusu Waethiopia waliokufa chini ya utawala wa mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed. Katika wingu la vita vya Ukraine, vita vinapiganwa nchini Ethiopia ambapo mamia kwa maelfu ya watu wamekufa, vita ambavyo hakuna anayeweza kuvishinda. Mhariri anasema vita vya Ethiopia huenda vikawa ndivyo vita vibaya kabisa duniani kwa sasa, huku waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed na washirika wake kwa miaka miwili wakipambana na wapiganaji wa chama cha ukombozi wa watu wa Tigray TPLF.

Wataalamu wanakadiria watu wapatao 50,000 wamekufa kufikia sasa kutokana na vita wakiwemo, wanajeshi na raia waliouliwa kwa risasi na mabomu na ndege zisizoendeshwa na rubani. Wengine wamekufa pia kutokana na magonjwa na njaa, silaha mbili hatari zinazosababisha maangamizi makubwa.

Gazeti la Neues Duetschland liliandika kuhusu mapinduzi nchini Burkina Faso likiwa na kichwa cha maneno kilichosema: Mapinduzi ya pili ya kijeshi katika kipindi cha miaka miwili. Rais wa mpito kapteni Ibrahim Traore ndiye nembo mpya ya matumaini. Umma wa WaBurkinabe, hususan vijana wanamuona Traore kama mtu mwenye nguvu anayeweza kuyatatua matatizo ya watu masikini wa nchi hiyo, lakini mwandishi wa gazeti la Neues Deutschland anasema mapinduzi hayo pia ni ishara ya uasi dhidi ya mkoloni wa zamani wa Burkina Faso, Ufaransa.

Inlandspresse

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW