1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ugonjwa wa Malaria waongezeka kwa kasi Rwanda

8 Januari 2025

Watu 67 wamefariki dunia nchini Rwanda kwa nyakati tofauti kutokana na ugonjwa wa malaria ambao umeonekana kuongezeka nchini humo.

Utoaji chanjo ya Malaria Cameroon
Utoaji chanjo ya Malaria CameroonPicha: Desire Danga Essigue/REUTERS

Serikali imewatahadharisha wananchi kuhusu kusambaa kwa malaria kunakosababishwa  na mazalia ya mbu  katika sehemu zao za makazi. Ugonjwa wa malaria umetajwa kuongezeka kwa kasi katika wilaya 15 kati ya wilaya 30 nchini Rwanda hii ikiwa na maana kwamba nusu ya nchi inakabiliwa na ugonjwa huo.

Soma: Ongezeko la aina mpya ya mbu sugu Afrika mashariki latishia vita dhidi ya Malaria

Kwa miaka kadhaa sasa ugonjwa wa malaria ulikuwa umefubazwa kwa kiasi kikubwa kutokana na hatua zilizokuwa zimechukuliwa na serikali ikiwa ni pamoja na kuwagawia wananchi vyandarua vilivyonyunyiziwa dawa ya kuua mbu pamoja na kuwahamasisha wananchi kusafisha maeneo yao kwa kuharibu sehemu zenye mazalia ya mbu.

Lakini sasa wizara ya afya inasema ni kama hatua hizo hazipo tena. Huyu ni waziri wa afya Dr Sabin Nsanzimana akionya kuhusu ugonjwa huu.

Utoaji chanjo ya Malaria washika kasi Cameroon

02:11

This browser does not support the video element.

"Ugonjwa wa malaria ni ugonjwa ambao kwa kawaida tunaujua unasababishwa na mbu lakini kwa siku za hivi karibuni tumeshuhudia ongezeko lake katika baadhi ya wilaya na kutishia kuwa janga na ndipo tulipofanya haraka kuchukua mikakati,maana tunaamini bila kuchukua hatua za maksudi ugonjwa huu utasabisha vifo zaidi vya watu."Niger yazindua kampeni ya chanjo dhidi ya Malaria

Katika baadhi ya vituo vya afya mjini Kigali wagonjwa wanakwenda kupata matibabu baadhi yao wanaumwa malaria. Igihozo Hycenthe yeye ni mara yake ya tatu kwenda hopitali kupata matibabu dhidi ya malaria katika kipindi cha miezi mitatu mfululizo.

"Mwezi wa kumi na moja niliugua ugonjwa huu, mwezi wa kumi na mbili nikaugua tena, na sasa mwezi huu wa kwanza ni mara ya tatu, na tena sina chandarua", alisema Hycenthe.

Hali ilivyo Uganda: Mbinu zinazotumiwa kutokomeza Malaria Uganda

Baadhi ya wahudumu wa afya katika hospitali na vituo vya afya wanathibitisha  kwamba kiwango cha maambukizi ya malaria kimeongezeka maradufu ndani ya kipindi cha miaka mitatu iliyopita. Bi Beatrice Magnifique ni mhudumu wa afya mjini Kigali, akizungumza na DW alisema kwamba; "Kati ya mwaka 2021 na 2022 nilikuwa nawapokea wagonjwa kumi kwa siku moja, kati ya hao kumi nilikuwa nikipata wagonjwa wa malaria tano au sita,lakini mwezi huu wa kumi na mbili uliopita niliwapokea wagonjwa 134 na wagonjwa 128 kati ya hao walikuwa na ugonjwa wa malaria."

Soma kwa kina kuhusu: Siku ya Malaria Duniani

Kiwango hiki cha ongezeko la wagonjwa kimesababisha ngazi za afya kupaza sauti na kuwakumbusha wananchi kuzingatia maangalizo ambayo yanatolewa na wataalam wa afya. Dr Mbituyumuremyi Aimable ni mkuu wa idara ya kupambana na malaria katika taasisi ya taifa ya magonjwa na tiba RBC anasema.

Chandarua ya kuzuia mbu TogoPicha: picture alliance/Photononstop

"Tunawaomba wananchi hasa wakati huu malaria imeongezeka  kuhakikisha wanatumia vyandarua vyenye dawa, pamoja na kuondoa mazalia ya mbu lakini pia kutumia kunyunyizia dawa ya kuua mbu katika makazi yao, hasa katika maimbo ya mashariki na kusini ambako kunashuhudia ongezeko kubwa la malaria."

Mafanikio ya kupambana na Malaria: Cape Verde yatangazwa kutokomeza ugonjwa wa Malaria

Wizara ya afya imesema kwamba hadi mwezi wa kumi na mbili mwaka jana wa 2024 watu 67 tayari walikuwa wamepoteza maisha kutokana na malaria na serikali imetangaza matumizi ya dawa mpya ya malaria kama hatua ya kukabiliana na ugonjwa huu.

Wataalam wa afya wanasema kasi ya ongezeko la  malaria imeshuhudiwa sana mwishoni mwa mwaka jana wa 2024 na kuwataka wananchi kuchukua hatua kali kuepuka ongezeko la kupata ugonjwa huu.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW