1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

FBI:Hakuna Mashitaka dhidi ya Hillary Clinton

7 Novemba 2016

Shirika la Upelelezi la Marekani, FBI limesema mgombea wa urais wa chama cha Democratic, Hillary Clinton hawezi kushtakiwa kutokana na kutumia anuani binafsi ya barua pepe.

USA Cleveland Präsidentschaftswahl Hillary Clinton
Picha: picture-alliance/AP Photo/P. Long

Kauli hiyo imetolewa katika dakika za lala salama, ikiwa imebakia siku moja kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu nchini Marekani, huku mpinzani wa Clinton katika kinyang'anyiro hicho, Donald Trump akiiita hatua ya FBI, uthibitisho wa kuwepo uchakachuaji.

Mkurugenzi wa FBI, James Comey, amewaambia wabunge wa Marekani kwamba ugunduzi mpya wa hivi karibuni kuhusu matumizi ya anuani binafsi ya barua pepe, wakati Clinton akiwa waziri wa mambo ya nje, hautasababisha mgombea huyo kufunguliwa mashtaka.

Mwezi uliopita, Comey aliwaarifu wabunge wa Baraza la Congress kwamba ofisi yake imegundua barua pepe mpya ambazo zinaweza kusababisha kuanzisha upya uchunguzi wa hitimisho lilitolewa Julai. 

Mkurugenzi wa FBI, James ComeyPicha: picture alliance/AP Photo/J. Scott Applewhite

Mbunge wa Republican, Jason Chaffetz, ambaye aliongoza uchunguzi wa bunge katika kesi hiyo, amesema Comey amemuarifu yeye pamoja na wabunge wengine kuhusu hitimisho la FBI.

Duru za karibu na uchunguzi huo, zililiambia gazeti la Marekani, ''The New York Times,'' kwamba barua pepe hizo ziligunduliwa katika uchunguzi tofauti katika kompyuta ya mbunge wa zamani, Anthony Weiner, mume wa msaidizi mwandamizi wa Hillary, Huma Abedin.

Kambi ya Clinton yafurahishwa na uamuzi wa FBI

Mkurugenzi mkuu wa mawasiliano wa kampeni ya Clinton, Jennifer Palmieri amewaambia waandishi wa habari kwamba wamefurahishwa na uamuzi huo wa FBI. ''Tumefurahi kuona hivyo, kama tulivyokuwa na uhakika kwamba atathibitisha hitimisho alilolifikia mwezi Julai na tunafurahi kuona kwamba suala hili limepatiwa ufumbuzi,'' alisema Palmieri.

Wakati upande wa Hillary wakiufurahia uamuzi huo, mgombea urais wa chama cha Republican, Donald Trump ameikosoa FBI, akisema shirika hilo linafahamu fika kwamba Clinton ana hatia. Akizungumza jana katika kampeni kwenye vitongoji vya Detroit, Trump amesema Clinton analindwa na mfumo wa uchaguzi ambao una njama ya kufanya udanganyifu wa kura. Amesema Clinton atachunguzwa kama rais, na hivyo kusababisha mzozo wa kikatiba.

Mgombea urais wa chama cha Republican, Donald TrumpPicha: Getty Images/J.J. Mitchell

Trump amesema, ''Kwa sasa analindwa na mfumo wa wizi wa kura. Ni mfumo wa wizi kabisa, nimekuwa nikisema hivi kwa muda mrefu. Huwezi kuzichunguza barua pepe mpya 650,000 ndani ya siku nane, huwezi kufanya hivyo. Hillary Clinton ana hatia. Anajua hivyo, FBI inajua, watu wanajua na sasa ni juu ya watu wa Marekani kuchagua haki kupitia masanduku ya kura tarehe 8 Novemba.''

Katika kukamilisha kampeni leo, Clinton atakuwa North Carolina, Michigan na Pennsylvania, ambako ataongozana na mumewe, Bill Clinton na mtoto wao, Chelsea, pamoja na Rais Barack Obama na mkewe Michelle Obama.

Utafiti wa maoni wa nchi nzima uliotolewa jana na kituo cha televisheni cha ABC na Washington Post, unaonyesha kuwa Clinton anaongoza kwa asilimia 5, huku utafiti mwingine wa shirika la utangazaji NBC na Jarida la Wall Street, ukionyesha kuwa Clinton anaongoza nchi nzima kwa asilimia 4.


Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DPA, AP, AFP
Mhariri: Daniel Gakuba

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW