1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhalifu na vijana barani Afrika

21 Februari 2019

Hadithi kuhusu uchunguzi katika michezo ya redio ya DW zinazungumzia changamoto zinazowakabili vijana barani Afrika.

LbE Crime Fighters Produktion Kenia 2019
Picha: DW/A. Gensbittel

Ungana na wapelelezi wetu wanaopigania ukweli na haki, huku ukipata mitazamo ya thamani katika masuala muhimu. Uhalifu wa Mtandaoni, Unyanyasaji wa Majumbani, Uchafuzi wa Mazingira na Biashara ya Binadamu – Michezo hii mipya ya hadithi zetu za Karandinga inaelezea kiini kinachowapa changamoto vijana wa Afrika. Tukiendeleza utamaduni wa mafanikio ya michezo ya kuigiza ya redio ya Noa Bongo Jenga Maisha Yako, Karandinga inatoa elimu na taarifa katika mfumo wa kuburudisha na kuwahamasisha wasikilizaji kufikiria wao wenyewe.

Bonyeza Kiunganishi

Mitandao ya kijamii imetawaliwa na picha za Zawadi, mwanafunzi kijana wa kike ambaye amekutwa amechomwa kisu kando ya barabara. Nini kimetokea kwake? Kwa mujibu wa polisi, ulikuwa uhalifu wa kimapenzi unaomfanya mpenzi wake kuwa mtuhumiwa mkuu. Lakini Kendi, rafiki wa karibu wa mtuhumiwa huyo, bado hajashawishika na ameanzisha upelelezi wake mwenyewe. Anaamini kuwa huenda Zawadi alikumbana na tapeli wa mtandaoni. Pamoja na mtaalamu wa masuala ya IT, Tembo, wanagundua siri kuhusu kijana wa kike na shughuli zake mtandaoni. Wanavyouchunguza zaidi ulimwengu wa kidigitali, baadhi ya hatari na fursa ya matumizi ya leo ya intaneti na mitandao ya kijamii zinaanza kujitokeza. Lakini je itawasaidia kupata majibu kusuhu mtu aliyemchoma kisu Zawadi? Mchezo huu umeandikwa na Wanjiku Mwaurah (Kenya)

Chozi la Mnyonge

Katika mji wa Lambu, ghafla polisi wana mambo mengi ya kufanya: Mtoto mchanga amekutwa tu nje ya kituo cha polisi. Siku inayofuata, mtu anayeheshimika sana katika jamii anakutwa amekufa mbele ya nyumba yake, huku kisu kikiwa bado kwenye kifua chake. Afisa kijana wa polisi, Amsa, anazishughulikia kesi hizo akishirikiana na mpelelezi mkuu, Bruce. Akiwa polisi pekee wa kike wa Lambu, Amsa pia anafuatwa na wanawake kadhaa wanaonyanyaswa na anajitolea kuwasaidia. Hili ni jambo gumu kwa sababu bado hakuna sheria kwenye nchi hiyo inayowaadhibu watu wanaofanya unyanyasaji wa majumbani. Ungana na Amsa, akijaribu kushughulikia kesi hizo na kuwalinda waathirika wa unyanyasaji wa majumbani.  Mchezo huu umeandikwa na Pinado Abdu Waba (Nigeria)

Unaniua Taratibu

Maisha yameimarika kwa wakaazi wa Donge la Maji tangu kampuni ya kusafisha chuma ilivyofunguliwa mjini humo na kutoa fursa za ajira. Aida Kabange, mama anayelea mtoto peke yake, hivi karibuni alihamia mjini humo na kuanza kazi kama katibu muhtasi wa kiwanda hicho. Lakini mambo yanakwenda ndivyo sivyo, baada ya mtoto wa kiume wa Aida kuumwa. Wakati huo huo, mfanyakazi wa kiwanda hicho anaanguka na kufa kutokana na ugonjwa wa Malaria, kama dokta alivyobainisha. Au kuna ukweli mwingine uliojificha nyuma ya kifo hichi? Wakati Aida anajaribu kutafuta chanzo cha ugonjwa wa mtoto wake, anagundua kitu kibaya katika kiwanda hicho. Je yuko tayari kuhatarisha kila kitu ili kufichua siri chafu kwenye kiwanda cha kusafishia chuma?  Mchezo huu umeandikwa na Chrispin Mwakideu (Kenya)

Jinamizi la Mauaji

Inspekta wa polisi George Cross amezongwa na mauaji ya mhudumu kijana wa kike aliyekatwa viungo vyake. Utambulisho wake bado ni siri. Uhalifu huu unaweza kuhusishwa na vitendo vya kishirikina? Anaposhughulikia kisa hicho, polisi huyo kijana bila kujitambua anamruhusu mdogo wake wa kike na binamu yake wa kiume kuendeleza ndoto zao kwenye nchi jirani. Melody na Kodjo wanataka kusoma nje ya nchi. Rafiki mmoja jirani amewaahidi kuwapatia mafunzo, hivyo kusisimua matarajio yao ya baadaye. Baada ya kutosikia kutoka kwao kwa muda mrefu, familia ya vijana hao, inaanza kupata wasiwasi. Wakati George anajaribu kuwasiliana na Melody na Kodjo na kushughulikia kesi ya mauaji, anagundua mtandao hatari wa wahalifu wanaofanya biashara ya binadamu.  Mchezo huu umeandikwa na Hurcyle Gnonhoué (Benin)

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW