1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhamiaji Umoja wa Ulaya bado suala tete

29 Septemba 2023

Licha ya mawaziri wa uhamiaji wa Umoja wa Ulaya kupata aina fulani ya makubaliano baada ya Ujerumani kuacha upinzani wake dhidi ya sehemu ya mkataba mpya wa wahamiaji, lakini kumesalia masuali kadhaa yaliyokosa majibu

Brüssel EU-Innenminister-Treffen
Picha: KENZO TRIBOUILLARD/AFP

Ingawa majadiliano yalikuwa makali, mawaziri wa mambo ya ndani wa Umoja wa Ulaya walishindwa kukamilisha kutatuwa mkwamo kwenye kile kiitwacho "Mkataba Mpya wa Wahamiaji". 

Kigingi cha mwisho kwenye mkwamo huo, yaani mfumo wa kutangaza janga la wahamiaji, hakikupatiwa ufumbuzi hadi mkutano unamalizika jioni ya Alkhamis (28 Septemba).

Soma zaidi: Ujerumani iko tayari kuridhia mageuzi ya uombaji hifadhi Ulaya
UN: Zaidi ya wahamiaji 180,000 wamevuka bahari ya Mediterania na kuingia Ulaya mwaka 2023

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa baraza la mawaziri wa ndani wa Umoja huo, Fernando Grande-Malarska wa Uhispania, "kigingi hicho kitajadiliwa siku chache zijazo."

Hata hivyo, kulikuwa na idadi kubwa ya wajumbe waliokubaliana kwa mengi katika mkutano huo, isipokuwa Poland na Hungary zilizosema zinapingana na mkataba huo mpya.

Italia ilitaja baadhi ya mambo yenye mashaka nayo na sasa inataka mkataba huo upitiwe kwa kina zaidi.

Ujerumani yabadili msimamo

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Ujerumani, Nancy Faeser, alilazimika kuachana na msimamo wa awali wa nchi yake kupingana na mkataba huo, na badala yake alikubaliana nao ingawa baada ya kuwasilisha marekebisho kadhaa mapya.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani, Nancy Faeser.Picha: KENZO TRIBOUILLARD/AFP

Muhimu katika hayo, ni kuyazuwia mataifa kama Italia na Ugiriki, ambayo ndiyo yanayowapokea kwanza wakimbizi wanaoingia Ulaya, kutangaza peke yao kuwepo kwa mgogoro wa wakimbizi.

Soma zaidi: Ujerumani kulegeza msimamo kuhusu mageuzi ya uombaji hifadhi

Mwaziri wa Uhamiaji wakutana Brussels kujadili mustakabali wa waomba hifadhi
“La muhimu kwetu ni kwamba hata kunapokuwa na hali ya mgogoro, tuhakikishiwe kwamba serikali moja peke yake haiwezi kutangaza hivi hivi tu madai ya kushusha viwango. Tumeandaa masharti mengine ya ziada kwa hilo kutokea.“ Alisema waziri huyo.

Hiyo inamaanisha, mchakato wa utangazaji wa hali mbaya ya uhamiaji utatangazwa, kuongezewa muda ama kutekelezwa pale tu idadi kubwa ya mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya itakapoidhinisha. 

Sharti hili kwa sasa linaihusu zaidi Italia, ambayo ingelipendelea kuwaruhusu wahamiaji wengi zaidi kadiri iwezekanayo kuelekea mataifa ya kaskazini haraka mno ili kujipunguzia mzigo kwenye vituo vya kuwahifadhia.

Mkataba si suluhisho kwa hali ya sasa

Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Ndani wa Austria, Gerhard Karner, uamuzi uliopitishwa jana mjini Brussels ni muhimu zaidi kwa ajili ya kuwapa nafasi wakimbizi ambao wana haki kweli ya kuingia UIaya.

''Tumekuwa wakali zaidi, tumekuwa wawazi zaidi, tumekuwa wagumu zaidi, ili kwa upande mwengine mfumo huu uweze kufanya kazi kwa wale hasa wanaohitaji msaada wetu.'' Alisema Karner.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Austria, Gerhard Karner.Picha: GEORG HOCHMUTH/APA/picturedesk/picture alliance

Soma zaidi: Mawaziri wa EU kujadili tena mageuzi ya uombaji hifadhi
Ujerumani: Watu wahama kutoka mijini kwenda vijijini

Mkataba huu wa wahamiaji ambao bado unangojea kujadiliwa kwenye Bunge la Ulaya unatowa nafasi ya moja kwa moja kwa watu zaidi ya 30,000 walio kwenye vituo vya kuwapokea wahamiaji nje ya mipaka ya Umoja wa Ulaya, lakini pia unatowa uwezekano wa wahamiaji kurejeshwa walikotoka wakiwa hapo hapo mpakani. 

Muhimu zaidi ni kuwa kwa mara ya kwanza, unajumuisha kipengele cha kugawana waomba hifadhi miongoni mwa mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya, ingawa Poland na Hungary zimesema wazi kwamba hazitautekeleza mkataba huo, na badala yake zitatumia kura zao za veto kuupinga. 

Hata hivyo, mkataba huu utachukuwa angalau miaka miwili kabla ya utekelezaji wake kuanza na hivyo sio suluhisho kwa mgogoro wa sasa wa wahimiaji, kama wale wanaoingia kwenye kisiwa cha Lampedusa nchini Italia.