Uhamiaji, Urusi changamoto kwa usalama wa kimataifa
14 Februari 2024Hata hivyo watu pia wana wasiwasi kuhusu mashambulizi ya mtandaoni na athari za akili ya kubuni. Kuanzia Februari 16 hadi 18, maafisa wa jeshi, wataalamu wa ulinzi na wanasiasa wa haiba kubwa kutoka kote ulimwenguni kwa mara nyingine tena watakutana mjini Munich, kusini mwa Ujerumani kwa mkutano wa masuala ya usalama huku rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy pia akitarajiwa kuhudhuria.
Ulimwengu utashuhudia kupwaya kwa siasa za kimataifa katika mwaka huu wa 2024, kutakakoandamana na misuguano katika maeneo mbalimbali kijiografia na kukosekana uhakika wa kiuchumi. Ndivyo alivyoandika Christoph Heusgen, mwenyekiti wa mkutano wa kimataifa wa usalama wa Munich, MSC, katika ripoti kuhusu mkutano huo ya mwaka 2024, ambayo ilitolewa siku ya Jumatatu kabla kufanyika mkutano huo mwishoni mwa wiki katika jimbo la Bavaria, kusini mwa Ujerumani.
Soma pia: NATO yajiandaa kwa hatari ya vita na Urusi
Katika faharasa ya mkutano wa usalama wa Munich iliyochapishwa kabla ya kufanyika mkutano wa mwaka huu, vita vya Urusi dhidi ya Ukraine viliorodheshwa kuwa kitisho kikubwa nambari moja kwa usalama, hususan katika nchi wanachama wa kundi la nchi zilizostawi kiviwanda la G7, zinazojumuisha dola zilizostawi zaidi kiuchumi duniani.
Katika matokeo ya utafiti wa sasa, ambapo watu 12,000 katika nchi za G7 walihojiwa, pamoja na Brazil, India, China na Afrika Kusini, uhamiaji kutokana na vita na mabadiliko ya tabia nchi, sasa vinaonekana kuwa muhimu zaidi kuliko uwezekano wa Urusi kuongeza zaidi uchokozi wake. Inaonekana wale waliohojiwa mwezi Oktoba na Novemba mwaka uliopita wamevizowea vita vinavyoendelea nchini Ukraine.
Utafiti wa mkutano wa Munich pia uliwahoji raia wa Ukraine kuhusu hali zisizokubalika za usitishwaji mapigano, huku asilimia 92 wakitaka vikosi vya Urusi viondoke kabisa kutoka Ukraine, pamoja na rasi ya Crimea. Ni asilimia 12 pekee ambao walisema wangeona inakubalika ikiwa Crimea ingebaki himaya ya Urusi. Zaidi ya thuluthi mbili wangependelea Ukraine ijiunge haraka na Umoja wa Ulaya na jumuiya ya kujihami ya NATO.
Kambi ya Magharibi yapoteza ushindani na China
Ripoti hiyo mpya ya utafiti iliyopewa jina "Lose-Lose" inadai kila mtu anapoteza ushawishi katika hali ya sasa ya ulimwengu. Nchi za magharibi zinapoteza ushawishi wake katika ushindani na China. Kwa mujibu wa utafiti huo, uelewa wa hofu kuhusu kuzuka kwa mzozo kwenye kanda ya Bahari ya Hindi na Pasifiki kati ya China na Taiwan umeongezeka kwa kasi kubwa.
Soma pia: Rais Putin asema hawana maslahi nchini Poland wala Latvia
Heusgen ameandika kuwa hofu ya China inayojiamini zaidi imeongezeka kwa kiwango kikubwa - hasa nchini Japan, ikifuatiwa na India, Marekani, Ujerumani na Ufaransa. Miongozi mwa nchi za G7, idadi kubwa ya wakazi wanaamini nchi zao zitakuwa na usalama mdogo na utajiri utapungua katika kipindi cha miaka 10 ijayo.
Uchanganuzi wa utafiti huo unaonesha kwamba watu katika nchi za G7 wanatarajia China na nchi za kusini mwa dunia kuongeza nguvu na mamlaka, huku China ikinufaika kuliko dola nyingine.
Utandawazi warudi nyuma
Ripoti inasema kutoridhishwa na hali ya kiuchumi duniani kunaongezeka. Kwa ujumla utandawazi unarudi nyuma. Ushindani na kuongezeka kwa mahitaji ya usalama kunatawala waziwazi katika ulimwengu wa leo. Kimataifa, mtaji mdogo uliopungua unaelekea China, na kuongezeka kwa uhasama baina ya maeneo ya kijiografia kumeizika ile imani kwamba utandawazi unaosukumwa na masoko unasaidia kupelekea ugavi wa haki wa faida. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, nchi zinawekeza zaidi katika uthabiti na usalama kuliko ufanisi.
Machafuko zaidi baada ya kila mapinduzi Sahel
Kuongezeka kwa ushawishi wa Urusi katika eneo la Sahel barani Afrika pia kulizingatiwa katika ripoti ya uchambuzi ya mkutano wa Munich. Kufukuzwa kwa vikosi vya Ufaransa na utawala wa kijeshi wa Niger mwaka uliopita ni mfano mmojawapo wa kupungua kwa ushawishi wa Ufaransa katika eneo hilo, huku Urusi ikionekana inajaribu kuzitenganisha nchi za ukanda wa Sahel na Ulaya na Marekani. Hapa pia waandishi wa ripoti hiyo wanaona watu walioshindwa tu. Watu wa eneo la Sahel wanapoteza fursa ya amani na maendeleo ya kidemokrasia, kwa kuwa kila mapinduzi tangu mwaka 2000 yamefuatiwa na viwango vya juu vya machafuko.
Soma pia: EU watasisitiza kuendelea kuisaidia Ukraine
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kuongezeka kwa hali ya kutoaminiana kote ulimwenguni pia kulidhihirisha uelewa wa hatari iliyopo kutokana na mashambulizi ya mtandaoni na athari hasi za matumizi ya akili ya kubuni.
Ripoti inadai licha ya maendeleo ya kiteknolojia kuwahi kuwa kichocheao muhimu cha utandawazi, sasa yamegeuka kuwa mashindano makubwa ya udhibiti wa siasa za dunia.
Hali hii inaungwa mkono na matokeo ya utafiti wa faharasa ya mkutano wa Munich, ambapo waliohojiwa kutoka Marekani wanakiorodhesha kitisho hiki kuwa juu sana, wakifuatiwa na wale wa kutoka India.
Kiujumla, inaonekana watu wanaendelea kuwa waoga kutokana na kampeni za kusambaza taarifa za uongo katika ulimwengu wa kidigitali.