Uharamia waongezeka Afrka magharibi
1 Novemba 2019Gazeti la Die welt limeandika, "Uchunguzi unaendelea" ni maneno ambayo yamekuwa yakitumika katika ripoti za hivi karibuni kuhusu matukio ya uharamia baharini. Kwa mfano, kuna habari juu ya meli kubwa ya mizigo iliyovamiwa karibu na pwani ya Afrika ya Magharibi. Maharamia waliojihami kwa silaha waliwachukua mateka wafanyakazi tisa wa meli hiyo na kutoweka kuelekea Cameroon. Jina la meli hiyo halikutajwa lakini bendera yake ni ya Liberia
Gazeti hilo linaendelea kuandika kuwa tawi la shirika la kimataifa la biashara na Umoja wa Mataifa liitwalo the International International Maritime Bureau (IMB), huchapisha taarifa za matukio kama hayo. Katika mji mkubwa zaidi wa Cameroon wa Douala wahalifu waliiteka nyara meli nyingine ya mizigo. Kipindi hiki, wafanyakazi nane wa meli hiyo walitekwa nyara na bendera ya meli hiyo ni ya Antigua. Jina la meli hiyo pia limewekwa kapuni.
Kwa upande wake gazeti la Frankfuter Allgemeine liliandika kuhusu ugunduzi wa gesi katika nchi za Mozambique na Senegal. Ugunduzi huo umesababisha ongezeko kubwa la uwekezaji. Nchi za Ulaya na Asia zimeonesha nia kwa kiasi kikubwa lakini kuna upungufu wa miundombinu na sheria mbadala.
Gazeti hilo linaandika, wiki mbili zilizopita tangu kufanyika kwa uchaguzi Kusini mashariki mwa Msumbiji, waangalizi wa uchaguzi huo walitupia macho eneo la kaskazini mwa nchi hiyo wakiwa na wasiwasi. Eneo hilo ni la mkoa wa Cabo Delgado linalopakana na Tanzania ambapo kundi la kiislamu lenye siasa kali limekuwa tishio. Wanajiita "wapiganaji wa kikhalifa” wakiharibu vijiji vyote na kuwaua wakazi. Hadi sasa takribani watu 300 wanaripotiwa kuwa waathiriwa wa ugaidi huo, na hatma ya mauaji hayo bado haijulikani.
Kwa serikali ya Msumbiji, Cabo Delgado ni zaidi ya eneo lililo mbali na mji mkuu linalokabiliwa na makundi ya kiislamu yenye siasa kali kwani, matumaini karibu yote ya mafanikio katika nchi hiyo yapo kwenye mji huo. Miaka minane iliyopita, gesi asilia iligunduliwa katika eneo hilo ulipo mto Ruvuma mpakani na Tanzania.
Die tageszeitung, liliandika juu ya uchaguzi wa hivi karibuni wa Botswana ambapo nchi hiyo imeendelea kuwa na msuguano baada ya Rais Mokgweetsi Masisi kuchaguliwa tena kutetea nafasi yake tofauti na matarajio. Gazeti hilo liliandika, chama chake kimekuwa kikiiongoza Botswana kwa zaidi ya nusu karne sasa.
Mokwgeetsi alishinda uchaguzi huo unaochukuliwa kuwa mgumu zaidi katika miaka 53 ya historia ya taifa hilo. Botswana, inayoonekana kuwa nchi thabiti katika eneo la Kusini mwa Afrika, ilikuwa imejiandaa kwa matukio baada ya Rais Masisi kujihusisha katika mgogoro wa wazi na mtangulizi wake Ian Khama.
Ian ni mtoto wa muasisi wa taifa hilo Seretse Khama alimchagua Masisi kuwa mrithi wake mwaka 2019 na kisha akakiacha chama chake cha BDP katika mgogoro. Alikiunga mkono chama kipya cha BPF. Waangalizi wengi wa uchaguzi walitegemea kuwa kuondoka kwa familia ya wanasiasa wakubwa kwenye chama tawala kungemaanisha mwisho wa chama hicho na kuwa na uchaguzi wenye matokeo yenye utata.
der Tagesspiegel linaandika juu ya kugunduliwa kwa program ya kupambana na Ebola, 'Ebola App' ambayo inatarajiwa kupunguza maambukizi ya ebola kwa kusaidia kuwapata watu walio na maambukizi ya homa hiyo.
Gazeti hio lilianza kwa kuandika, mara nyingi huanza kama mafua. Joto la mwili hupanda kidogo na maumivu ya viungo. Ndani ya siku chache, mtu hupata maumivu ya tumbo, kichefuchefu na kutapika. Wale wasiopata matibabu wanaishia kufariki. Mlipuko wa sasa wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo unaua watu wawili kati ya watatu walio na maambukizi ya ugonjwa huo.
Hata hivyo sasa kuna chanjo ambazo zimeonesha mafanikio katika kipindi cha majaribio. Kadri mtu anavyotibiwa mapema ndivyo uwezekano wa kupona unavyokuwa mkubwa. Hili linaweza kusaidiwa na program ya simu za kisasa inayotengenezwa katika jimbo la Saxony, Ujerumani. Programu hiyo, Ebola App inasaidia kuwapata watu wenye maambukizi kwa haraka, kuwapa angalizo na kuwasaidia wapate tiba.