Athari za kimazingira za mizozo ya kivita
2 Juni 2021Matumizi ya kemikali za kupukutisha majani ya miti msituni iliyotumiwa na jeshi la Marekani katika vita vya Vietnman, kuchoma moto visima vya mafuta wakati wa vita vya ghuba hadi uchafuzi wa vyanzo vya maji katika mashambulizi ya Israel kwenye Ukanda wa Gaza, ni baadhi ya visa vya uchafuzi mkubwa wa mazingira uliosababishwa na mizozo.
Lakini athari za vita kwa mazingira ni mada ambayo haiangaziwi sana, sababu mojawapo ikiwa kwamba udhibiti wa utoaji wa gesi chafu haujumuishwi katika mikataba ya kimataifa ya ulinzi wa mazingira, ukiwemo ule wa Kyoto wa mwaka 1997.
Soma pia: UN: Mizozo huwauwa na kuwaumiza watoto 12,000
Profesa wa sayansi ya siasa katika chuo kikuu cha Boston nchini Marekani, Neta Crawford, anasema kutojumuishwa kwa kipengele hicho kunatokana na Marekani kupinga hatua yoyote inayoweza kuweka kikomo katika uwezo wake wa kijeshi.
Crawford ambaye ni mkurugenzi mshiriki wa Mradi wa Gharama ya Vita, anasema baada ya kusambaratika kwa iliyokuwa Umoja wa Kisovieti mwaka 1990, Marekani ilihofu kuwa udhibiti wowote katika utoaji wa gesi chafu unaweza kuwa kikwazo kwa hadhi yake mpya ya kuwa taifa pekee kubwa kijeshi duniani.
Ukweli ni kwamba kamajeshi la Marekani lingekuwa taifa, lingekuwa miongoni mwa mataifa 50 yanayoongoza kwa utoaji wa gesi ya kaboni inayochafua mazingira, likija mbele ya nchi kama Sweden na Denmark, anasema profesa Crawford.
Mbali na utafiti wake, utafiti mwingine wa chuo kikuu cha Lancaster na Durham ambao ripoti yake ilichapishwa mwaka 2019, ulidhihirisha kuwa jeshi la Marekani ndiyo taasisi inayoongoza duniani kwa matumizi ya bidhaa za haidrokaboni, kama bidhaa zitokanazo na petroli.
Ncha mbili za upanga mmoja
Kulingana na profesa Neta Crawford, mizozo na mazingira ni ncha mbili za upanga mmoja. Anasema ingawa taasisi za kijeshi duniani zimetambua kwa muda mrefu kuwa athari za mabadiliko ya tabianchi zitakuwa chanzo kikubwa cha mizozo siku za usoni, hazijafanya vya kutosha katika kupunguza kasi ya mabadiliko hayo.
Anasema badala ya kupambana na sababu zinazoleta mabadiliko hayo ili kuyazuia, taasisi hizo za kijeshi zinajipanga kukabiliana na athari hizo, akitoa mfano wa jeshi la majini la Marekani, ambalo linakabiliana na ongezeko la kina cha maji ya ya bahari kwa kuzifanyia ukarabati bandari zake za Florida na Virginia ziendane na mabadiliko hayo.
Soma pia:Umoja wa Mataifa waonya athari za ujoto kwa nchi tajiri
Mtafiti mwingine, Patrick Bigger ambaye ni mhadhiri kwenye kitengo cha mazingira katika chuo kikuu cha Lancaster, anasema hata pale jeshi la Marekani linapotumia nishati mbadala kama nguvu za jua na mafuta yatokanayo na mimea, kama lilivyofanya nchini Afghanistan, ufanisi unaolengwa sio wa kimazingira,bali ni wa kijeshi.
Lakini hata kama majeshi yangeamua kuhamia katika matumizi ya nishati safi, bado mizozo itaendelea tu kuwa kitisho kwa mazingira. Mkurugenzi anayehusika na sera katika taasisi ya CEOBS inayofanya utafiti wa athari za kimazingira zitokanazo na mizozo, Doug Weir anatoa mfano wa nchini Colombia, ambako uasi wa kundi la FARC ambao umeweka ombwe kubwa la mamlaka ya serikali, umechochea ufyekaji wa misitu ambayo awali ilisaidia pakubwa kufyonza hewa chafu ya kaboni.
Benjamin Neimark, mhadhiri mwandamizi katika kitengo cha kitengo cha mazingira katika chuo kikuu cha Lancaster anapendekeza suluhisho gumu kwa mchango huu mkubwa wa taasisi za kijeshi, hususan jeshi la Marekani katika uchafuzi wa mazingira ya dunia; yaani kufungwa kwa vituo vipatavyo 800 vya jeshi la Marekani katika nchi 70 duniani.
Hata hivyo Patrick Bigger, mhadhiri mwenzake katika kitengo hicho hicho, anasema hilo kisiasa halifikiriki, ushahidi wa wazi ukiwa kwamba katika tangazo la mkakati wake wa kutunza mazingira hivi karibuni, rais wa Marekani Joe Biden hakusema chochote juu ya uchafuzi utokanao na shughuli za kijeshi.
Chanzo: DW