1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhispania moto wa kuotea mbali

Josephat Nyiro Charo15 Juni 2012

Mabingwa watetezi wa kombe la kandanda la mataifa ya Ulaya Uhispania, imesambaratisha ngome ya Jamhuri ya Ireland kwa mabao 4-0, katika michuano inayofanyika Ukraine na Poland.

Spain's Fernando Torres, fourth left, celebrates after scoring a goal with teammates during the Euro 2012 soccer championship Group C match between Spain and Ireland in Gdansk, Poland, Thursday, June 14, 2012. (Foto:Michael Sohn/AP/dapd)
Uhispania ikishangilia ushindiPicha: AP

Mabao mawili kati ya manne hayo yaliwekwa kimyani na mshambuliaji Fernando Torres na kuisambaratisha kabisa ndoto ya Ireland kufikia hatua ya robo fainali. Goli la pili lilifungwa na David Silva. Na goli la nne lilitundikwa nyavuni na Cesc Fabregas ambaye alichukua nafasi ya Torres katika kipindi cha pili.

Mchezaji kiungo wa Iraland, Keith Andrew alikiri kwamba kulikuwa na makosa tangu mwanzo wa mchezo huo na kusema wanajifunza kutokana na makosa. Uhispania iliutawala mchezo huo kwa asilimia 60, walitandika mikwaju 26 golini, ambapo 20 kati ya hiyo ililenga kabisa goli na kumfanya kipa wa Ireland awe katika kibano kikali. Hali kwa upande wa Ireland ilikuwa mbaya pamoja na kufanikiwa kutandika mikwaju sita katika goli la wapinzani wao lakini waliambulia patupu.

Ushindi huu sasa unaiweka Uhispania kileleni kwa tofauti ya magoli ikiwa na point nne sawa na Croatia na ambazo zitatua tena dimbani Jumatatu ijayo.

Torres akipachika bao la kwanzaPicha: Reuters

Italia yatoka sare na Croatia

Awali katika mchezo kati ya Italia na Croatia, Andrea Pirlo aliiongoza Italia katika mchuano huo pale ambapo alikunjua mkwaju mkali katika dakika ya 39 na kuifumua nyavu ya Croatia. Ama katika kipindi cha pili katika dakika ya 72 mambo yakabadilika wakati Mario Mandzukic alipowainua mashabiki wa Croatia pale alipotia kimyani bao la kusawazisha.

Katika kipindi cha kwanza Italia ilikosa nafasi kadhaa za ushindi kupitia wachezaji wake Mario Balotelli, Claudio Machisio na Anthonio Cassano. Na hasa Balotelli aliyeonekana mwenye kusitasita katika kipindi hicho cha kwanza na kufanya kukosa nafasi za wazi kabisa za ushindi. Hata hivyo mchezaji huyo aliwekwa benchi na nafasi yake kuchukuliwa na Antonio Di Natale ambaye hata hivyo naye alitoka bila kufunga goli.

Pirlo akiutikisa wavu wa CroatiaPicha: Reuters

Kutokana na hali hiyo kocha wa Italia Cesare Prandelli alisikia akisema, "Kama huwezi kumalizia bila shaka utabaki na majuto," bila shaka alikuwa akihoji kitendo cha mchezaji Balotelli kubaki mbele pasipo matunda yoyote.

Baada ya ushindi wake wa mabao 3-1 katika mechi yao ya mwanzo, Croatia ina pointi 4 katika kundi C, Na Italia ina pointi mbili baada ya kutoka sare ya 1-1 na mabingwa watetezi Uhispania katika mchezo wake wa ufunguzi. Baada ya mpambano wa jana kocha wa Croatia, Slaven Bilic alisika akisema kwamba taifa lake halikutegema matokeo ya goli moja kwa moja, kwa kujinasibu kwamba kwa hakika wana nafasi nzuri ya kusonga mbele.

Moto unawaka tena leo wakati timu za kundi "D" zitakapojimwaga viwanjani. Ukraine itakipiga na Ufaransa na Sweden kumenyana na England.

Mwandishi: Sudi Mnette/AFP

Mhariri: Josephat Charo