Uhispania: Pablo Casado achaguliwa kukiongoza chama cha PP
21 Julai 2018Kwenye hotuba yake baada ya kushinda Casado amesema chama chake kinapaswa kurudi katikati jamii ya Uhispania ili kuhakikisha kazi walioifanya haiharibiwi pia ameahidi kutetea maadili ya maisha na familia. Casado alikuwa mkuu wa wafanyakazi wa Waziri Mkuu wa zamani Jose Maria Aznar aliyekuwa madarakani kutoka mwaka 2009 hadi 2012.
Mshindani wa Casado katika nafasi hiyo ya juu kwenye chama hicho cha PP Soraya Saenz de Santamaria, aliwaambia waandishi wa habari kuwa amekubali kushindwa hata kabla ya kutangazwa rasmi matokeo ya kura hiyo muda mfupi tu baada ya manaibu hao wa chama cha PP kupiga kura zao huko mjini Madrid.
Casado, alipata kura 1,701 na Soraya Saenz de Santamaria alipata kura 1,250. Wabunge na wanachama wengine wanaoshikilia nafasi za juu kwenye chama hicho cha PP walishiriki katika zoezi hilo la kupiga kura. Uteuzi wa Casado, mwanasheria ambaye ameahidi matumaini na marekebisho katika chama hicho, ni hatua inayoonekana kuegemea mrengo wa kulia kwa chama hicho.
Casado amechukua msimamo mkali kuhusu jimbo la Catalonia, akitaka kufanywa kuwa ni kosa la uhalifu na pia kinyume cha sheria nchini Uhispania kuitisha kura ya maoni ili kuongeza kasi ya kukabiliana kisheria na tishio la kujitenga.
Wiki hii, Pablo Casado alisema majadiliano hayatafanya kazi kwa wale wanaotaka kuvunja sheria. Kiongozi huyo mteule pia anapinga marufuku juu ya utoaji uhai usio na machungu au mateso kwa mgonjwa asiyekuwa na taama ya kupona au aliye kwenye koma kwa muda mrefu bila kuwepo na matumaini ya kuzinduka tena kama inavyohamasishwa na srikali ya Kisoshalisti. Zoezi hilo bado halijahalalishwa katika nchi nyingi. Casado pia nataka kupunguza mishahara na kodi ya mapato kwa makampuni.
Kiongozi huyo mpya wa chama cha PP anatarajiwa kuleta sura mpya au kukipa maisha mapya chama hicho kilichopoteza wapiga kura milioni tatu katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2011, wakati ambapo Mariano Rajoy alishinda kwa kupata kura nyingi, tofauti na uchaguzi uliopita wa mwaka 2016. Wengi wa wapiga kura wamehamia kwenye chama kinacholemea mrengo wa kati kulia cha Ciudadanos, kutokana na hasira juu ya mfululizo wa kashfa za rushwa zilizokikumba chama cha PP katika miaka ya hivi karibuni.
Rajoy aliondolewa kwa kura ya kutokuwa na imani naye mnamo mwezi Juni, katika hatua inayoonekana kama wanachama kutoridhishwa na jinsi alivyoushughulikia mgogoro wa jimbo la Catalonia lililokuwa linataka uhuru wake na pili ni kwa mtazamo kwamba alikuwa dhaifu katika kupambana na rushwa.
Mwandishi: Zainab Aziz/AFPE/APE
Mhariri: Yusra Buwayhid