Uhispania yachukua hatua kuvunja serikali ya Catalonia
21 Oktoba 2017Rajoy amesema serikali yake haina budi bali kuchukua hatua hiyo ya kuipokonya Catalonia uhuru wa kujitawala baada ya kiongozi wake Carles Puigdemont kujiendesha kwa njia isiyo stahili na kujichukulia maamumzi ambayo ni kinyume na katiba ya nchi.
Msemaji wa Puigdemont amesema atatoa tamko kuhusiana na hatua hiyo ya serikali kuu ya kutaka kulipokonya jimbo la Catalonia uhuru wa kujitawala leo saa tatu usiku.
Catalonia kupokonywa uhuru
Baraza la mawaziri limekutana kujadili upana wa hatua ambazo serikali itapanga kuchukua chini ya Ibara ya 155 ya Katiba ya Uhispania. Kipengele hicho cha katiba kinaipa mamlaka serikali kuu kuingilia kati wakati moja ya majimbo 17 ya Uhispania yenye uhuru litakaposhindwa kuzingatia sheria.
Rajoy amesema ataliomba baraza la seneti kumpa idhini ya kulivunja bunge la Catalonia na kuitisha chaguzi katika kipindi kisichozidi miezi sita. Pia anaomba idhini ya kuipokonya serikali ya jimbo la Catalonia majukumu yake yote.
Uamuzi wa baraza la seneti unatarajiwa kuchukuliwa katika kipindi cha juma moja lijalo kuhusu hatma ya jimbo hilo tajiri. Chama cha kihafidhina cha Rajoy ndicho kilicho na idadi kubwa ya wawakilishi katika baraza hilo la seneti na pia anaungwa mkono na chama kikuu cha upinzani cha kisosholisti pamoja na chama cha kuegemea siasa za wastani cha Ciudadanos.
Iwapo baraza la seneti litaridhia mapendekezo ya Rahoy, bunge la Catalonia litaendelea na shughuli zake za kawaida hadi litakapovunjwa lakini halitakuwa na mamlaka ya kumchagua kiongozi mpya wa serikali ya Catalonia kuchukua mahala pa Puigdemont au kupiga kura yoyote kuhusu kupitisha sheria zinazoendana kinyume na katiba ya Uhispania.
Viongozi wa Catalonia wapingwa kila upande
Kura ya maoni ya Wacatalonia kutaka kujitenga na kujitawala iliyofanyika Oktoba mosi, imechochea mzozo mkubwa wa kisiasa Uhispania ambao haujashuhudiwa katika kipindi cha miongo mingi.
Ibara ya 155 ya Katiba ya Uhispania, itapelekea serikali kuu ya Uhispania kuchukua mara moja wizara ya uchumi ya Catalonia, polisi, vyombo vya habari na mitandao rasmi. Lengo kuu ni kuuvunja utawala wa jimbo hilo linaloongozwa na Puigdemont na kufanya chaguzi mpya jimboni humo.
Wachambuzi wanadokeza kuwa Puigdemont anaweza kuzuia ibara hiyo ya katiba kutotumika iwapo ataitisha chaguzi. Kulingana na chunguzi za utafiti wa maoni ya wapiga kura, asilimia 68 ya Wacatonia wanataka chaguzi mpya kufanyika ili kuutatua mzozo huo wa kisiasa.
Asilimia 55.6 ya Wacatolonia wanaamini kuwa hakuna msingi wa kisheria kwa jimbo hilo tajiri kujitenga na Uhispania. Wanaotaka kujitenga wanahoji kuwa kura ya maoni iliyofanyika mapema mwezi huu, ambapo asilimia 90 ya wapiga kura walitaka kujitenga kwa Catalonia iliwapa mamlaka ya kutangaza uhuru wa kujitawala.
Mwandishi: Caro Robi/afp/AP
Mhariri: Yusra Buwahyid