1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhispania yadhibiti hatamu za uongozi Catalonia

Oumilkheir Hamidou
28 Oktoba 2017

Serikali kuu ya Uhispania imedhibiti hatamu za uongozi wa jimbo la Catalonia, imewapokonya nyadhifa zao viongozi wa serikali iliyoasi, siku moja baada ya wabunge kutangaza uhuru wa jimbo hilo tajiri,

Kundgebung für die Einheit Spaniens in Madrid
Picha: Imago/Agencia EFE

Hakuna bado ishara yoyote hadi sasa inayoonyesha kama maafisa wa Catalonia watauheshimu au wataupinga uamuzi wa serikali ya mjini Madrid wa kuwafukuza kazi na kulitumbukiza jimbo hilo katika  janga la misuko suko na kwa namna hiyo kuzidisha makali ya mvutano wa mwezi mzima dhidi ya viongozi wa serikali kuu ya Uhispania.

Uamuzi huo umetangazwa baada ya siku kadhaa za vurugu kubwa kabisa kuwahi kushuhudiwa katika historia ya karibuni ya nchi hiyo, pale bunge la taifa mjini Madrid lilipoidhinisha hatua zisizokuwa na mfano, kuzuwia juhudi za kujitenga za bunge la jimbo la Catalonia mjini Barcelona.

Uhispania imeweka uamuzi wa kudhibiti madaraka mjini Barcelona kwa kutangaza hatua maalum mapema hii leo mtandaoni.

Waziri mkuu Mariano Rajoy anaedhibiti  hivi sasa majukumu ya rais wa jimbo hilo Carles Puigdemont ,amelivunja pia bunge la mjini Barcelona  na kuitisha uchaguzi mpya decemba 21 inayokuja.

Wakaazi walio wengi wa Catalonia wanaafuatilizia magazetini na mitandaoni kinachojiri nchini humPicha: Reuters/Y. Herman

 Matokeo ya uchaguzi mpya yatabadilisha nini?

Bado haijulikani kama uchaguzi huo mpya utaupatia ufumbuzi mzozo wa kujitenga jimbo la Catalonia au la. Utafiti wa maoni  ya wananchi unaashiria vyama vinavyopigania uhuru vitaendelea kudhibiti wingi mdogo wa viti katika bunge hilo, lakini havitajikingia zaidi ya asilimia 50 ya kura.

Rajoy anasema tangazo la uhuru sio tu ni kinyume na katiba bali pia ni uhalifu. Kuanzia sasa Puigdemont na wanachama 12 wa baraza lake la mawaziri hawatokuwa tena wakilipwa na wanaweza kushitakiwa kwa madai ya kutwaa kwa nguvu madaraka, pindi wakiupinga uamuzi uliopitishwa. Na mpaka sasa hakuna dalili kama wataheshimu amri iliyotolewa na serikali kuu mjini Madrid.

Polisi ya Catalonia yalinda bunge baada ya tangazo la uhuruPicha: Reuters/Y. Herman

Mkuu  wa kikosi maalum cha polisi ya jimbo la Catalonia-Mossos apokonywa wadhifa wake

Makamo wa rais Soraya Saenez de Santamaria ndie aliyeteuliwa kumwakilisha Rajoy na kusimamia shughuli za utawala katika jimbo la Catalonia hadi Desemba 21, uchaguzi mpya wa bunge utakapoitishwa. Anasimamia shughuli za wizara mbadala zilizoundwa katika jimbo hilo, ikiwa ni pamoja na wizara ya fedha na usalama pamoja na kuwateuwa maafisa watakaofuata amri kutoka Madrid.

Mojawapo ya hatua za mwanzo zilizopitishwa; Wizara ya mambo ya ndani ya Uhispania imetangaza amri ya kumshusha cheo Josep Lluis Trapero aliyekuwa hadi wakati huu mkuu wa kikosi maalum cha polisi ya mjini ya Catalonia-Mossos. Ataruhusiwa kuendelea na kazi yake lakini kama kamishna wa polisi tu. Mkuu wa Trapero, mkurugenzi wa polisi ya jimbo la Catalonia Pere Soler amesema katika taarifa yake ameridhia uamuzi wa serikali kuu ya mjini Madrid wa kumshusha cheo Trapero.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AP

Mhariri: Yusra Buwayhid

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW