1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhispania yaingia robofainali

30 Juni 2010

Mabingwa Ulaya Uhispania imekuwa nchi ya mwisho kufuzu kwa robofainali ya michuano hiyo ya kombe la dunia baada ya kuichapa Ureno bao 1-0 katika mechi iliyokuwa kali na ngumu.

David Villa akishangilia bao aliloifungia Uhispania dhidi ya UrenoPicha: AP

Alikuwa ni mshambuliaji hatari wa timu hiyo David Villa aliyewarejesha nyumbani Ronaldo na wenzake, kwa bao la dakika ya 63 na kufufua matumaini kwa Uhispania kuweza kutwaa ubingwa huo.Uhispania ni miongoni mwa timu ambazo zinapigiwa sana upatu kushinda taji hilo, hata mfalme wa kandanda duniani Pele ni miongoni mwa wale wanapiga upatu huo.

Timu nyingine zilizofuzu kwa robofainali ni pamoja na Paraguay, Ujerumani, Ghana, Brazil, Argentina, Uholanzi na Uruguay.

Paruguay ilifanikiwa kuingia hatua hiyo kwa mara ya kwanza katika historia ya kabumbu la nchi hiyo baada ya kuitoa Japan kwa changamoto ya mikwaju ya penalti, kufuatia kila mtu kutoweza kuufumania mlango wa mwenzie hata pale mpambano uliporefushwa muda.

Mshambuliaji nyota wa timu hiyo Santa Cruz alisema kuwa kufuzu kwa hatua hiyo, ni ndoto aliyokuwa akiiota na kwamba sasa imekuwa kweli.Amesema kwa kipindi cha miaka minne iliyopita wamekuwa wakiota fainali za mwaka huu kufanya vyema.

Mechi mbili za kwanza za robofainali zitakuwa Ijumaa ijayo kwa pambano kati ya Brazil na Uholanzi na baadaye Ghana na Uruguay. Jumamosi itakuwa zamu ya Ujerumani kuumana na Argentina na hatimaye Uhispania kucheza na Paraguay.

Wachezaji wa UjerumaniPicha: AP

Baada ya kukuru kakara ya mechi 48 katika makundi na nane katika hatua ya mtoano hatimaye timu hizo 8 zimechomoza kuwa na mbinu mujarabu dimbani, lakini ilikuwa ni mbinu ya kujilinda na kushambulia kwa kushtukiza iliyoonekana kutumika na majogoo wa kabumbu waliyofuzu miongoni mwao Ujerumani na Brazil.

Katika hatua ya makundi wastani wa mabao yaliyopachikwa ulikuwa ni mabao mawili kwa kila mechi ambapo hatua hii ya kufuzu kwa robofainali, wastani ulikuwa ni mabao matatu kwa mechi huku timu zikionesha kabumbu la kuvutia.

Brazil ikionekana kuwa na hamu kubwa ya kutwaa ubingwa huo wa dunia kwa mara ya sita, ilipata ushindi wa kusisimua wa mabao 3-0 dhidi ya Chile huku soka lake likivutia.

Luis Fabiano akishangilia baoPicha: AP

Huku mabeki wake wa pembeni wakiwa na uwezo wa kunyang´anya mipira na kushambulia, ilitumia vyema mbinu ya kushambulia kwa kushtukiza.Mfano bao la pili lililofungwa na Luis Fabiano lilitokana na ushirikiano wa pasi za haraka haraka kati ya Robinho na Kaka kabla ya kumfikia mfungaji.

Jogoo wa zamani wa Brazil aliyekuwemo katika kikosi cha timu hiyo kilichotwaa ubingwa wa dunia mwaka 1970, Tostao, amesema Brazil miaka yote ni timu ya kushambulia zaidi, lakini mbinu za safari hii ni kuzuia zaidi na kushambulia kwa kushtukiza.

Lakini mbinu za kocha wa Ujerumani Joachim Loew za kushambulia kwa kushtukiza ndizo ambazo zimezaa mabao mengi zaidi katika hatua hiyo ya mtoano, kwa ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Uingereza.

Hatua hiyo ya mtoano pia ilishuhudia maamuzi yenye utata, ambapo Uingereza ilikataliwa bao lake la kusawazisha dhidi ya Ujerumani, pamoja na bao la Argentina dhidi ya Mexico mfungaji akionekana kuwa aliotea.Rais wa FIFA Sepp Blater alikiri kuwa wakati sasa umefika wa kujadili kutumika kwa teknolojia katika kuwasaidia waamuzi dimbani.Bunge la Ujerumani limetaka bao hilo la Uingereza likubaliwe.

Kansela Angela MerkelPicha: AP

Katika hatua nyingine Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ambaye ni mshabiki mkubwa wa kabumbu anatarajiwa kuelekea Afrika Kusini kuishangilia timu yake katika robofainali dhidi ya Argentina hapo siku ya Jumamosi.

Mwandishi:Aboubakary Liongo/Reuters/AFP