Uhispania yaiunga mkono katiba ya umoja wa Ulaya.
21 Februari 2005Uhispania ndilo taifa la kwanza la jumuiya ya Ulaya kuiunga mkono katiba ya umoja huo kufuatia kura ya maoni iliyopigwa nchini humo hapo jana. Maafisa wa Ulaya wanatumai kwamba hatua hiyo ya Uhispania itakuwa mfano kwa mataifa mengine ya Ulaya yatakayoipigia kura ya maoni katiba hiyo siku zijazo
Afisa mkuu anayehusika na mawasiliano ya umoja wa Ulaya, Margot Wallstrom, amesema hatua ya Uhispania kuiunga mkono katiba ya Ulaya ni jambo la kuridhisha na ni ishara kwa mataifa mengine wanachama yatakayoipigia kura katiba hiyo katika miezi kumi na nane ijayo. Hata hivyo hakufurahishwa na idadi ya wapiga kura walioshiriki katika kura hiyo ya maoni.
Uingereza nayo imeipongeza Uhispania lakini ikaelezea kutoridhishwa kwake kwa idadi ndogo ya wapiga kura. Kate Hoey, mwanachama wa chama cha Labour, amesema idadi hiyo ilikuwa ndogo mno. Ameongeza kusema katiba ya Ulaya imeshinda katika hatua yake ya kwanza lakini ni wazi kwamba imejikwaa.
Idadi ya walioshiriki katika kura hiyo ya maoni nchini Uhispania, imeelezewa kuwa ya chini zaidi tangu kurejeshwa kwa maongozi ya kidemokrasi, kufuatia kifo cha dikteta wa kijeshi, jenerali Francisco Franco, mwaka wa 1975.
Katika kura ya maoni kutaka mabadiliko ya kisiasa iliyofanyika mwaka wa 1976, na ya kutaka katiba ya kidemokrasia mwaka wa 1978 na kura ya maoni ya Uhispania kuendelea kubakia katika shirika la NATO ya mwaka wa 1986, idadi ya wapiga kura waliojitokeza ilikuwa kati ya asilimia 60 na 78.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na wizara ya mambo ya ndani ya Uhispania, zaidi ya asilimia 42 ya wapiga kura walijitokeza kushiriki katika kura hiyo, huku wahispania wanne katika kila wahispania watano wakiiunga mkono katiba hiyo.
Waziri mkuu wa Uhispania, Jose Luis Rodriguez Zapatero, alisema na ninamnukulu, ´ Kura yetu ni mfano kwa raia wenzetu wa umoja wa Ulaya ambao walikuwa wakisubiri uamuzi wetu. Leo, Ulaya imeshinda, katiba ya Ulaya imeshinda na Uhispania imeshinda,´ mwisho wa kumnukulu.
Zapatero aliyatolea wito mataifa wanachama wa jumuiya ya Ulaya kuiga mfano wa Uhispania na yapige kura kuiunga mkono katiba hiyo. Wazo lake hilo liliungwa mkono na Javier Solana, waziri wa mambo ya kigeni wa jumuiya ya Ulaya.
Mataifa kumi ya umoja wa Ulaya, yakiwemo, Uhispania, Uingereza, Poland na jamhuri ya Ucheki, yameamua katiba hiyo ipigiwe kura na wananchi. Mataifa 15 yaliyosalia, ikiwemo Ujerumani, yameamua katiba hiyo iidhinishwe na bunge. Mbali na Uhispania, Slovenia, Lithunia na Hungary tayari ziliidhinisha katiba hiyo. Bunge la Itali bado halijaiidhinisha katiba hiyo.
Solana alisema matokeo hayo ya Uhispania yatachangia pakubwa kuyasaidia mataifa wanachama kufanya mashauri kuhusiana na katiba hiyo mpya. Kimsingi mataifa yote 25 wanachama yanatakiwa kuiunga mkono katiba hiyo, inayonuiwa kuyafanikisha maongozi ya jumuiya ya Ulaya, kabla kuanza kufanya kazi.
Rais wa Ufaransa, Jacques Chirac, ambaye alisafiri hadi Uhispania kuziunga mkono kampeni za kuipigia kura katiba ya umoja wa Ulaya, alimpongeza Zapatero kwa matokeo hayo. Alisema hatua ya wahispania kuiunga mkono katiba hiyo, na Ulaya yote kwa jumla, ni ishara muhimu itakayoyaongoza mataifa mengine wanachama yatakayopiga kura kuiidhinisha katiba hiyo.
Matokeo ya kura hiyo ya maoni yanatarajiwa hatimaye kuidhinishwa rasmi na bunge la Uhispania. Mfalme Juan Carlos, ambaye hapigi kura katika uchaguzi mkuu wa taifa hilo, alikuwa kati ya wahispania wa kwanza kupiga kura mjini Madrid, pamoja na malkia Sofia.
Katika eneo la kazkazini la Basque na Catalonia, katiba hiyo haikuungwa mkono kikamilifu. Vyama vitano viliipinga katiba hiyo, vikisema haina lengo la kuyaunganisha maeneo hayo na Ulaya. Usalama uliimarishwa nchini kote, huku polisi elfu 106 walishika doria. Kulikuwa na wasiwasi mkubwa kwamba wanamgambo wa kundi la ETA la chama cha Basque, walikuwa na njama ya kufanya mashambulio.