Wahamiaji 500,000 kupata hadhi ya kisheria Uhispania
29 Januari 2026
Hatua hii ya kipekee itatekelezwa kwa kuharakisha kutolewa kwa amri ya serikali ili kurekebisha sheria za uhamiaji, kwa mujibu wa Waziri wa Uhamiaji wa Uhispania, Elma Saiz, hatua inayoweka kando muswada sawa ambao umekwama bungeni. Wahamiaji watakaostahili watapewa hadi mwaka mmoja wa ukaazi wa kisheria pamoja na kibali cha kufanya kazi.
Tofauti na mataifa mengine yaliyochukua hatua za kuzuia uhamiaji na hifadhi ya wakimbizi—mengi yakichochewa na sera za utawala wa Trump—Uhispania imechukua mwelekeo tofauti chini ya Waziri Mkuu Pedro Sánchez, huku yeye na mawaziri wake wakisisitiza mara kwa mara faida za uhamiaji wa kisheria kwa uchumi na nguvu kazi inayozeeka ya nchi hiyo.
Uhispania "haitageuka na kuangalia pembeni,” Saiz aliwaambia waandishi wa habari katika mkutano na vyombo vya habari. Serikali inafanya hivyo ili "kuwapa heshima na kutambua watu ambao tayari wako katika nchi yetu,” alisema.
Hatua hiyo inaweza kunufaisha takribani watu 500,000 wanaoishi Uhispania bila vibali, kwa mujibu wa Saiz. Mashirika mengine yanakadiria kuwa hadi watu 800,000 wanaishi gizani katika jamii ya Uhispania. Wengi wao ni wahamiaji kutoka Amerika ya Kusini au Afrika wanaofanya kazi katika sekta za kilimo, utalii au huduma—nguzo kuu za uchumi unaokua kwa kasi wa Uhispania.
Raia wa kigeni waliowasili Uhispania kabla ya tarehe 31 Desemba 2025 na wanaoweza kuthibitisha kuwa wameishi nchini humo kwa angalau miezi mitano watastahili. Pia watahitajika kuthibitisha kuwa hawana rekodi ya uhalifu.
Saiz alisema anatarajia waombaji wanaostahili kuanza kuwasilisha maombi yao kuanzia Aprili hadi mwisho wa Juni. Aliongeza kuwa rasilimali zitapatikana kuhakikisha mchakato unaendeshwa kwa ufanisi, baada ya chama cha wafanyakazi wa polisi wa kitaifa kuonya kuhusu uwezekano wa mfumo kulemewa.
'Ushindi katika mazingira ya chuki dhidi ya wahamiaji'
Hatua ya serikali ya Uhispania iliwashangaza wengi baada ya makubaliano ya dakika za mwisho kati ya Chama cha Kisoshalisti kinachotawala na chama cha mrengo wa kushoto cha Podemos, kama sehemu ya kubadilishana uungwaji mkono wa bunge kwa serikali dhaifu ya Sánchez.
Irene Montero, mbunge wa Bunge la Ulaya kutoka Podemos, ambaye alitangaza makubaliano hayo Jumatatu, alilinganisha hatua ya Uhispania na utekelezaji mkali wa sheria za uhamiaji nchini Marekani, ambako utawala wa Trump umekosolewa vikali kwa operesheni zake, hususan katika jimbo la Minnesota.
"Iwapo wao wanateka watoto, kuua na kutisha watu, sisi tunawapa nyaraka,” alisema Montero wakati wa mkutano wa hadhara akiwa pamoja na wanaharakati wa haki za wahamiaji.
Habari hiyo ilishangiliwa na mamia ya mashirika ya kutetea haki za wahamiaji pamoja na mashirika mashuhuri ya Kanisa Katoliki, ambayo yalifanya kampeni na kukusanya saini 700,000 kwa ajili ya mpango kama huo.
"Hatuzoei ushindi wa aina hii,” alisema Silvana Cabrera, msemaji wa kundi la wanaharakati la RegularizaciónYa, huku akizuia machozi. Harakati hiyo ilizaliwa wakati wa janga la COVID-19, ambapo wahamiaji wengi walio hatarini walifanya kazi muhimu bila haki wala ulinzi wa kutosha.
Katika taarifa yake Jumanne, Baraza la Maaskofu Katoliki la Uhispania liliita hatua hiyo "kitendo cha haki ya kijamii na utambuzi wa wahamiaji wengi ambao, kupitia kazi zao, wamechangia kwa muda mrefu maendeleo ya” Uhispania.
Faida kwa wahamiaji na uchumi wa Uhispania
"Katika wakati ambapo mazingira ya chuki dhidi ya wahamiaji yanaenea pande zote za Atlantiki, hatua hii inaonyesha ubinadamu na busara,” alisema Laetitia Van der Vennet, afisa mwandamizi wa utetezi kutoka PICUM, mtandao wa Ulaya wa mashirika ya haki za wahamiaji.
Sio mara ya kwanza Uhispania kutoa msamaha kwa wahamiaji walioko nchini humo kinyume cha sheria: ilifanya hivyo mara sita kati ya mwaka 1986 na 2005.
"Kulikuwa na athari kubwa katika soko la ajira, si tu kwa kuhalalisha hadhi ya wafanyakazi bali pia kwa kuunda ajira rasmi,” alisema Anna Terrón Cusi, mtafiti mwandamizi katika taasisi ya Migration Policy Institute, ambaye awali alifanya kazi katika sera za uhamiaji kwa serikali kadhaa za Uhispania, ikiwemo ya Sánchez.
Hatua hiyo itaiwezesha Uhispania "kuanza upya” kabla ya kuanza kutekelezwa mwezi Juni kwa mkataba mpya wa Ulaya kuhusu uhamiaji na hifadhi ya wakimbizi, ambao unategemea zaidi kurejeshwa kwa wahamiaji kama suluhu ya uhamiaji usio fuata sheria, alisema Terrón.
Aliongeza kuwa kwa kuwapa hadhi ya kisheria wahamiaji wasio na vibali, Sánchez anatoa haki na ulinzi kwa wafanyakazi wasio na nyaraka huku pia akiunufaisha uchumi wa Uhispania. "Mwisho wa siku, kuwaambia watu kwamba uhamiaji ni mbaya kunaweza kuwavutia, lakini kumfukuza mwanamke anayesafisha nyumba yao ni jambo tofauti,” alisema.
Upinzani wakosoa vikali hatua hiyo
Vyama vya siasa vya mrengo wa kati-kulia na mrengo mkali wa kulia vilikosoa vikali tangazo la serikali.
Alberto Núñez Feijóo, kiongozi wa Chama cha Popular Party, alimshutumu Sánchez kwa kujaribu kuficha ajali mbaya ya treni mapema mwezi huu iliyosababisha vifo vya watu 46.
Kwa upande wake, Santiago Abascal, kiongozi wa chama cha mrengo wa kulia kinachopinga uhamiaji cha Vox, aliandika kwenye mitandao ya kijamii kwamba Sánchez "anawachukia Wahispania” na kwamba "anaharakisha uvamizi,” kauli inayorudia nadharia ya kibaguzi inayotumiwa mara nyingi na makundi ya msimamo mkali wa mrengo wa kulia.
Uhispania—nchi iliyoshuhudia mamilioni ya raia wake wakiondoka wakati na baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe—imepokea mamilioni ya watu kutoka Amerika Kusini na Afrika katika miaka ya karibuni. Idadi kubwa waliingia nchini humo kwa njia halali.
Saiz alisema Uhispania itaendelea kuwa "taa ya mwongozo” katika mapambano dhidi ya wimbi la kimataifa la siasa za kupinga uhamiaji zinazoongozwa na mrengo mkali wa kulia.
"Tutafanya kila lililo ndani ya uwezo wetu kulizuia,” alisema. "Ninaamini kuwa leo ni siku njema kwa nchi yetu.”