1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sanchez atangaza baraza la mawaziri lenye wanawake wengi

Yusra Buwayhid
7 Juni 2018

Waziri Mkuu wa Uhispania ametangaza baraza lake la mawaziri Alhamisi linalounga mkono Umoja wa Ulaya na lenye wingi wa wanawake katika historia ya nchi hiyo. Pedro Sanchez ameteua mawaziri 11 kati ya 17.

Spanien Madrid Pedro Sanchez stellt neues Kabinett vor
Picha: Getty Images/AFP/J. Soriano

Serikali ya kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 46, aliyeurithi wadhifa wa uwaziri mkuu kutoka kwa mhafidhina Mariano Rajoy Ijumaa iliyopita katika kura ya kutokuwa na imani nae, inajumuisha idadi kubwa ya mawaziri wanawake ikiwa ni pamoja na Carmen Calvo, atakaekuwa naibu waziri mkuu.

Wanawake wamepewa nafasi za kushughulikia idara za uchumi, fedha na ulinzi. Pia wataongoza mahakama ya nchi, wizara za elimu, bajeti na mazingira.

"Kuna hali ya zamani na ya leo nchini mwetu kutokana na vuguvugu la haki za wanawake, na serikali mpya inaakisi vuguvugu hilo. Kwa mara ya kwanza katika historia ya demokrasia yetu, wanawake ni wengi kuliko wanaume katika baraza la mawaziri, 11 kati ya 17 ni wanawake. Majukumu ya kiuchumi ya serikali yatabebwa na wanawake. Na serikali inazipa kipaumbele sera za usawa, na kuongozwa na Naibu Waziri Mkuu.” amesema Sanchez wakati akitangaza baraza jipya la mawaziri.

Msimamizi wa bajeti ya Umoja wa Ulaya Nadia Calvino mwenye uzoefu wa miaka 12 katika nyadhifa mbalimbali za umoja huo, ameteuliwa kuwa waziri wa uchumi na rais wa zamani wa bunge la Ulaya Josep Borrell ameteuliwa kama waziri wa mambo ya nje. Maria Jesus atakuwa waziri wa bajeti baada ya kuwa na wadhifa huo katika serikali ya jimbo la kusini mwa Andalusia.

Carmen Calvo alieteuliwa kuwa naibu waziri mkuuPicha: picture-alliance/dpa/epa/O. Labrador

Akiwa na lengo la kuendeleza utulivu nchini humo, Sanchez ameahidi kutekeleza bajeti kwa mwaka wa 2018, iliyoandaliwa na serikali iliyoondoka madarakani ya kihafidhina.

Miongoni mwa hatua muhimu za bajeti hiyo ni ongezeko la kati ya asilimi moja hadi tatu ya malipo ya kiwango cha chini cha pensheni, na ongezeko la mishahara kwa watumishi wa umma, kabla ya uchaguzi wa serikali za mitaa, uchaguzi wa majimbo na uchaguzi wa wawakilishi katika bunge la Ulaya hapo mwakani.

Serikali inayoakisi jamii ya Uhispania

Sanchez amesema serikali yake ni kioo ya jamii ya Uhispania, ambayo inajumuisha wanawake na wanaume, vizee na vijana, na yenye kufuata misingi ya Umoja wa Ulaya.

Hata hivyo serikali hiyo ya Kisoshalisti ni ya wachache kwa vile imepata viti 84 pekee katika bunge la viti 350. Sanchez ameahidi kushughulikia matatizo ya kijamii yanyolikabili taifa hilo, lakini wachumi wanasema ukosefu wake wa wingi wa viti bungeni na sheria za bajeti za Umoja wa Ulaya vitamzuia kuleta mabadiliko makubwa.

Wanawake pia wataongoza timu ya uchumi ya serikali ya Sanchez, ambayo amesema kipaumbele mbele chake itakuwa ni kuheshimu mabano ya matumizi yaliyopendekezwa na Umoja wa Ulaya.

Uhispania ni nchi yenye uchumi wa nne kwa ukubwa katika Umoja wa Ulaya. Lakini pia ni taifa la pili lenye kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira katika umoja huo, ambayo ni asilimia 16.7 ya idadi yote ya watu nchini humo. Serikali hiyo mpya ya Sanchez inatarajiwa kula kiapo mbele ya Mfalme Felipe VI baaade Alhamisi.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/afp/rtre

Mhariri: Bruce Amani

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW