Uhispania yatwaa kombe la Ulaya katika kandanda.
30 Juni 2008Uhispania imebeba kombe la ubingwa wa Ulaya kwa mara nyingine baada ya miaka 24.
Timu hiyo iliibwaga Ujerumani bao moja kwa bila katika mechi iliyochezwa kwenye uwanja wa mji mkuu wa Austria ,Vienna. Goli la Uhispania lilifungwa na Fernando Torres katika dakika ya 33. Timu ya Uhispania ilionesha kandanda ya hali ya juu sana kiasi kwamba Ujerumani ingeliweza kufungwa mabao mengi zaidi.
Kocha wa Ujerumani Joachim Löw amekiri hayo na amempongeza kocha mwenzake wa timu ya Uhispania kwa kusema kuwa hana budi akubali kwamba wachezaji wa Uhispania walikuwa hodari zaidi. Hatahivyo kocha huyo amewapongeza wachezaji wake kwa bidii kubwa waliyofanya kwenye mashindano yote ya wiki sita
Wachezaji wa Ujerumani hawakuwa na turufu wakati wote. Takwimu zimethibitisha kuwa waliweza kuenda sambamba na Uhispania kwa muda wa dakika kama 15 tu kwa wakati mmoja na baada ya hapo walidorora kama alivyosema nahodha wa timu ya Ujerumani Michael Ballack.
Ballack amesema timu yake ilikuwa na nia lakini haikuwa na uwezo.
Katika upande mwingine waziri mkuu wa Uhispania bwana Zapatero amesema ushindi wa timu yake umeashiria mafanikio ya kwanza chini ya demokrasia na amewataka wachezaji wa nchi yake washike uzi huo huo hadi kwenye mashindano ya kuwania kombe la dunia mnamo mwaka 2010 nchini Afrika Kusini. Bwana Zapatero amesema ni heshima kubwa kwake kwa uhispania kupata mafanikio hayo chini ya uongozi wake wa kidemokrasia .Amesema mafanikio makubwa zaidi yapo njiani.
►◄