Uholanzi na Ujerumani kuumana
11 Juni 2012Timu zote mbili zinaorodheshwa na FIFA kuwa nne bora ulimwenguni. Zote mbili zilimaliza katika nafasi ya pili na tatu katika kinyang'anyiro kilichopita cha kombe la dunia. Uholanzi dhidi ya Ujerumani, mojawapo ya mechi kubwa zaidi za uhasimu katika kandanda na katika michezo yote kwa sababu hiyo.
Na kumalizia mambo, Uholanzi ni lazima ishinde mchuano huo wa Jumatano ili kurejea tena katika dimba hilo. Ikishindwa basi ni kama wataondolewa na kwa kuondolewa mikononi mwa Ujerumani basi litakuwa suala chungu zaidi kulimeza. Ujerumani iliishinda Ureno goli moja kwa sifuri Jumamosi katika mchuano uliokuwa mgumu zaidi. Huyu hapa kocha wa timu ya taifa Joachim Löw.
Shirikisho la soka barani Ulaya - UEFA limechukua hatua dhidi ya Ujerumani na Ureno kutokana na tabia ya mashabiki wao na timu. Kamati ya nidhamu ya UEFA itaishughulikia kesi hiyo Alhamisi kuhusiana na matukio ya mchuano wa kundi B Jumamosi mjini Lviv, Ukraine.
Shirikisho la soka Ujerumani DFV limeshtakiwa baada ya mashabiki wake kurusha fataki nalo shirikisho la Soka Ureno FPF likikabiliwa na kesi ya kucheleweshwa mchuano katika kipindi cha pili.
UFEA tayari inaendesha kesi dhidi ya Urusi baada ya mashabiki wan chi hiyo kuwasha baruti na kuwashambulia walinzi wa uwanjani. Wakuu wa soka wa Urusi wameapa kufayna kila wawezalo kuzia kurudiwa kwa ghasia kama hizo na wakawaonya rasmi mashabiki wao kuonyesha tabia nzuri.
Di Matteo kocha mpya wa Chelsea?
Klabu ya Chelsea inatarajiwa kutangaza wiki hii uteuzi wa Roberto Di Matteo kama meneja wake. Wawakilishi wa Mutaliano huyo walifanya mazungumzo na maafisa wa Chelsea mwishoni mwa wiki na Di Matteo mweny umri wa miaka 41 amehakikishiwa kuwa ndiye mtu anayetakiwa na mmiliki wa klabu hiyo Roman Abramovich.
Di Matteo amekubali mkataba huo kimsingi huku kanuni nyingine zikikamilishwa. Aliteuliwa kama kaimu kocha baada ya Andre Villas-Boas kupigwa kalamu. Aliiongoza Chelsea hadi ushindi wa kombe la Ligi ya Mabingwa Ulaya na lile la FA.
Majonzi Ufilipino
Wafilipino walielezea mshangao wao na wengine wakatokwa machozi ya huzuni Jumapili baada ya bondia wao Manny Pacquiao kushindwa mjini Las Vegas, na bondia wa Marekani Timothy Bradley. Manny alipokonywa taji lake la WBO weklterweight.
Pacquiao alishindwa kutokana na uamuzi wa pointi katika ukumbi wa MGM Grand Arena na hivyo kumaliza miaka saba ya taaluma yake ya bila kushindwa.
Idadi kubwa ya Wafilipino walikiga kelele wakiesema Manny alidanganywa baada ya kutazama mchuano huo kwenye televisheni kubwa zilizoezekwa kwenye maeneo ya umma nchini Ufilipino.
Pacquiao alisema alikuwa na uhakika asilimia mia kuwa alishinda pigano hilo na sasa anasubiri pigano la marudiano tarehe 10 Novemba ijapokuwa mahala litakakoandaliwa hapajaamuliwa.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/Reuters
Mhariri: Yusuf Saumu