1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Uholanzi yasaini makubaliano ya ulinzi na Ukraine

2 Machi 2024

Waziri Mkuu wa Uholanzi Mark Rutte Ijumaa alisaini mkataba wa ulinzi na Ukraine katika mji wa kaskazini mashariki wa nchi hiyo wa Kharkiv.

Ukraine Zelenskiy na Rutte makubaliano ya ulinzi
Waziri Mkuu wa Uholanzi Mark Rutte (kushoto) na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy (kulia)Picha: Ukrainian Presidential Press Service via REUTERS

Rutte alisema Uholanzi itasaidia kufadhili makombora laki nane kwa ajili ya kuzuia mashambulizi ya majeshi ya Urusi.

Rutte alikutana na Rais Volodymyr Zelenskiy katika ziara ya kushtukiza huko Kharkiv na amekuwa kiongozi wa saba wa nchi za Magharibi kusaini mkataba wa usalama wa miaka kumi na Ukraine katika kipindi cha miezi miwili iliyopita.

Tofauti za kisiasa na maelewano kuhusu Ukraine

Ukraine ina upungufu mkubwa wa silaha wakati ambapo majeshi yake yanajaribu kuwazuia majeshi ya Urusi amba wanafanya mashambulizi kwa mara nyengine mashariki mwa nchi hiyo, miaka miwili baada ya uvamizi kamili ya Urusi ulipoanza.

Rutte na Zelenskiy wakisaini mkataba wa ulinziPicha: Ukrainian Presidential Press Service via REUTERS

Hayo yakiarifiwa, Rais Joe Biden amempongeza Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni kwa uungaji mkono wake wa Ukraine. Biden ameyasema haya wakati wa mazungumzo kati yake na Meloni, mazungumzo yaliyotiliwa kiwingu na mustakabali wa msaada wa Marekani kwa Kyiv.

Licha ya tofauti zao za kisiasa, kiongozi huyo wa Italia anayefuata siasa za mrengo wa kulia na mkongwe huyo wa chama cha Democratic, wamekuwa na mahusiano mazuri, hasa kutokana na msimamo madhubuti alio nao Meloni kuhusu kuiunga mkono Ukraine katika vita vyake na Urusi.

Msaada wa Ukraine wakwamishwa na Warepublican bunge

"Nataka nikushukuru kwa kuiunga mkono pakubwa Ukraine" alisema Biden, mwenye umri wa miaka 81 alipokuwa akizungumza na Meloni mwenye miaka 47 katika afisi yake katika ikulu ya White House.

Rais Joe Biden (kulia) na Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni (kushoto)Picha: Saul Loeb/AFP

Biden alikuwa anataka kumhakikishia kwa mara nyenginetena meloni kwamba anawasukuma Warepublican wasiuzuie msaada wa dola bilioni 60 wa silaha muhimu za kijeshi kwa Ukraine.

Hii ilikuwa ziara ya pili ya Meloni katika White House baada ya kufanya ziara yake ya kwanza mwezi Julai mwaka jana 2023.

Vyanzo: DPA/AFP