1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uholanzi yawazuia mawaziri wa Uturuki kuhutubia

Caro Robi
12 Machi 2017

Uholanzi imewazuia mawaziri wa Uturuki kuhutubia katika mikutano ya hadhara katika mji wa Rotterdam katika mzozo wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili kuhusu Uturuki kufanya mikutano ya kisiasa.

Rotterdam Türkische Ministerin darf Konsulat nicht betreten


Rotterdam Türkische Ministerin darf Konsulat nicht betreten
Picha: Reuters/Y. Herman

Baada ya Rais Erdogan kuwaita Waholanzi Manazi na kuwa ni mabaki ya mafashisti kufuatia kunyimwa ruhusa ya kuingia nchini humo waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Mevlut Cavosoglu, mzozo wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili ulizidi kuzorota baada ya waziri wa masuala ya familia wa Uturuki naye kuzuiwa na polisi kuingia ubalozi mdogo wa Uturuki ulioko Rotterdam.

Mamia ya waandamanaji waliokuwa wanapeperusha bendera ya Uturuki walikusanyika nje ya ubalozi huo mdogo wakitaka kumuona balozi huyo. Polisi walitumia mbwa na magari ya kurusha maji mapema leo Jumapili kuwatawanya waaandamanaji hao ambao waliwarushia chupa na mawe.

Waziri wa masuala ya familia Fatma Betul Sayan Kaya ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa amesindikizwa kurejeshwa Ujerumani alikotokea kuingia Uholanzi. Kaya amesema ulimwengu sharti uchukue msimamo kwa ajili ya demokrasia dhidi ya kitendo cha kuzuiwa kuhutubia Uholanzi alichokitaja ufashisti. Meya wa mji wa Rotterdam amethibitisha kuwa waziri huyo anasindikizwa na polisi kuelekea mpaka wa Ujerumani.

Waandamanaji nje ya ubalozi wa Uholanzi nchini UturukiPicha: picture alliance/AP Photo

Uturuki na Uholanzi zalumbana

Serikali ya Uholanzi imesema inachukulia ziara hizo za mawaziri wa Uturuki kuwa zisizotakikana na  haitashiriki katika kampeini za kisiasa za mawaziri hao nchini humo. Serikali hiyo imesema mikutano hiyo ya kisiasa inaweza kusababisha migawanyiko miongoni mwa jamii ya waturuki nchini humo ambako kuna wanaomuunga mkono Erdogan na wanaompinga.

Uholanzi inafanya uchaguzi mkuu Jumatano ijayo. Wanasiasa wa Uholanzi wa pande zote wamesema wanaunga mkono uamuzi wa Waziri mkuu Mark Rutte kupiga marufuku mikutano ya mawaziri wa Uturuki.

Geert Wilders kiongozi wa chama kinachowapinga Waislamu Uholanzi ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa kwa Waturuki wote walioko Uholanzi wanaomuunga mkono Erdogan waende Uturuki na wasirejee kamwe nchini humo.

Wizara ya mambo ya nje ya Uturuki imesema haimtaki balozi wa Uholanzi nchini humo ambaye yuko likizoni kurejea nchini humo kwa muda, maafisa wameufunga ubalozi wa Uholanzi katika mji wa Ankara na ubalozi mdogo ulioko Istanbul na kutishia kuiwekea Uholanzi vikwazo vya kiuchumi na kisiasa.

Ujerumani na Austria pia zazuia mikutano

Erdogan anatafuta kuungwa mkono na idadi kubwa ya Waturuki walio katika mataifa ya Ulaya hasa Ujerumani na Uholanzi kumsaidia kupata ushindi katika kura ya maoni inayotarajiwa kufanyika mwezi ujao ambayo itampa madaraka makubwa zaidi.

Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Mevlut CavusogluPicha: picture-alliance/AA/A. Hudaverdi Yaman

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema atafanya kila awezalo kuepusha mzozo wa kisiasa wa Uturuki kusambaa Ujerumani. Mikutano minne iliyokuwa ifanyike Austria na Uswisi pia imefutiliwa mbali.

Licha ya kuzuiwa kuingia Uholanzi, Cavusoglu amesema atasafiri kuelekea nchini humo kwani ni waziri wa mambo ya nje na ana haki ya kusafiri kokote atakako, akisema Ulaya inapaswa kuachana na kasumba ya kuwa mwinyi na kuishutumu Uholanzi kwa kuwachukulia raia wa Uturuki walio nchini humo kama mateka.

Baada ya kuzuiwa kuingia Uholanzi, Cavusoglu alielekea Ufaransa ambako anatarajiwa kuhutubia mkutano wa hadhara katika mji wa Metz. Waziri mkuu wa Uturuki Binali Yildirim ameapa kutakuwa na hatua kali baada ya Kaya kuzuiwa kuingia ubalozi mdogo wa Uturuki mjini Rotterdam na kufurushwa nchini humo.

Yildirim amesema wanaojiita marafiki wao Ulaya ambao kila fursa wanayopata wanazungumzia demokrasia, uhuru wa kujieleza na haki za binadamu, kwa mara nyingine wameshindwa kuyadhihirisha wanayoyazungumzia na kuongeza matukio kama hayo yanawafanya kuwatambua marafiki wao wa kweli. Uturuki imewataka raia wao walioko Ujerumani na Uholanzi kuwa watulivu.

Mwandishi: Caro Robi/Reuters/afp/dpa

Mhariri: Sudi Mnette

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW