Uhuru aapishwa kuwa rais wa nne wa Kenya
9 Aprili 2013Kenyatta mwenye umri wa miaka 51 ni mtoto wa rais wa kwanza wa Kenya, Jomo Kenyatta. Ushindi wake wa asilimia 50.07 katika uchaguzi wa tarehe 4 Machi ulihalalishwa na Mahakama ya Juu baada ya pingamizi lililowekwa na Waziri Mkuu anayemaliza muda wake, Raila Odinga, kutupiliwa mbali na mahakama hiyo.
Kenyatta anayekuwa rais wa nne wa taifa hilo la Afrika ya Mashariki tangu lilipopata uhuru wake kutoka Uingereza mwaka 1963, anakuwa rais wa pili barani Afrika kuwa madarakani hali anakabiliwa na mashitaka kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kwa tuhuma za kusaidia kuchochea ghasia za kikabila zilizoukumba uchaguzi wa urais wa Kenya wa mwaka 2007. Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa mwezi Julai, ambapo Kenyatta na naibu wake, William Ruto, wanakabiliwa na mashitaka ya aina moja.
Hata hivyo, uchaguzi wa mara hii ulikuwa wa amani na kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, Wakenya wengi wanatarajia kwamba Uhuru atatimiza ahadi yake ya kuwa kiongozi wa watu wote na hatakuwa rais wa kabila lake tu, jambo ambalo limekuwa kawaida kwa wanasiasa wa huko.
Utata unaoyakumba mataifa ya Magharibi
Kwa mataifa ya Magharibi, ambao ni wafadhili wakubwa wa nchi hiyo yenye uchumi mkubwa zaidi kwenye eneo la la mashariki mwa Afrika, Kenya ni mshirika muhimu katika mapambano dhidi ya makundi ya kidini yenye siasa kali kwenye eneo hilo.
Lakini sasa mataifa hayo yanakabiliwa na uchaguzi wa ama kuendelea kuimarisha mahusiano au kujitenga na kiongozi ambaye anakabiliwa na mashitaka kwenye mahakama ya ICC mjini The Hague.
Marekani na mataifa makubwa ya Ulaya yalisema yangelituma mabalozi wao kwenye sherehe za kuapishwa kwa Kenyatta, kiwango cha uwakilishi ambacho wanasema bado kinakwenda sambamba na msimamo wao wa kuwa na mahusiano ya lazima tu na watuhumiwa hao.
Mtaalamu wa masuala ya Kenya katika Chuo Kikuu cha Warwick, Daniel Branch, ameiambia Reuters kuwa mataifa ya Magharibi yamejikuta kwenye hali ngumu sana, lakini huenda kila nchi ikatafuta njia yake yenyewe na mahusiano na Kenya.
China huenda ikapata fursa mpya
Ikiwa mataifa ya Magharibi yatagawika kuhusu mahusiano yake na Kenya chini ya Uhuru Kenyatta, hali hiyo itafungua njia zaidi kwa China na mataifa mengine makubwa ya Asia ambayo yamekuwa yakijizolea ushawishi wa kisiasa na kibiashara barani Afrika kwa siku za hivi karibuni.
Wakati kwenye sherehe hizo, viongozi wakuu wa Afrika watajikuta wamewekwa pamoja na mabalozi tu wa nchi za Magharibi, Kenya na India - ambazo zote mbili hazijasaini Mkataba wa Rome ulioanzisha ICC - zimetuma maafisa wao wa ngazi za juu.
Hata hivyo, mabalozi wa Kimagharibi wataepuka matusi mengine, baada ya maafisa wa Kenya kusema kuwa Rais Omar Hassan al-Bashir wa Sudan asingelihudhuria sherehe hiyo.
Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AP
Mhariri: Josephat Charo