Uhuru Kenyatta, atawazwa mshindi wa urais Kenya
30 Machi 2013Uamuzi huo umetolewa katika taifa hilo ambalo bado linakabiliwa na changamoto nyingi zilizosababishwa na machafuko ya baada ya uchaguzi miaka mitano iliyopita.
Kenyatta, anayekabiliwa na mashitaka ya uhalifu dhidi ya ubinaadamu katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifi ya ICC mjini The Hague nchini Uholanzi, kuhusiana na machafuko ya baada ya uchaguzi wa mwaka 2007, alitangazwa mshindi wa uchaguzi uliofanyiaka Machi 4 mwaka huu, hivyo kuepeuka duru ya pili kwa kura 8,000 tu.
Lakini matokeo hayo yalipingwa na mpinzani wake mkubwa, waziri mkuu anayeondoka madarakani, Raila Amolo Odinga, ambaye alisema uchaguzi huo ulikumbwa na mizengwe.
Hatma ya Odinga na Kenyatta mikononi mwa majaji 6
Kama Mahakama ya Juu itatangaza kwamba matokeo ya uchaguzi ni halali, mlango utakuwa wazi kwa Uhuru, mtoto wa rais wa kwanza wa Kenya na mmojawapo wa watu matajiri kabisa barani Afrika, kuapishwa Aprili 4 na kuwa rais wa nne wa Jamhuri ya Kenya. Mahakama ya Juu inaweza pia kumuunga mkono Odinga na kuamuru uchaguzi mpya.
Majaji sita wa mahakama hiyo wanaweza pia kuamua kwamba madai ya Odinga ya kuwepo udanganyifu na mapungufu katika uchaguzi huo yana msingi, lakini wanaweza kutangaza kuwa hayakufikia kiwango cha kuyatangaza matokeo ya uchaguzi huo kuwa si halali.
Hali ya wasiwasi imetanda kabla ya kutolewa kwa uamuzi huo. Uchaguzi wa mwaka 2007 ulikumbwa na malalamiko kama haya ya udanganyifu na kusababisha damu kumwagika, ambapo zaidi ya watu 1,100 waliuawa na kusababisha maelfu kuyakimbia makaaazi yao.
Polisi wametawanywa kuzunguka jengo la mahakama hiyo iliyopo katikatik mwa jiji la Nairobi, huku Mkuu wa Polisi nchini Kenya, David Kimaiyo akionya kuwa mikusanyiko kuzunguka mahakama hiyo haitakubalika.
Kenyatta aridhishwa na mahakama
Hadi sasa, Kenyatta anaonekana kuridhishwa na uamuzi utakaotolewa na mahakama hiyo, baada ya mwanzoni mwa wiki hii kuomba radhi kuhusu matamshi aliyoyatoa ya kuwashushia hadhi majaji kwa kusema ''watu sita'' wanatoa uamuzi. Jumanne iliyopita, mahakama ilikataa ombi moja la Odinga, kwamba Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka-IEBC kuweka wazi daftari la wapiga kura ililotumia kuhesabu kura, baada ya mfumo wa elektroniki kukwama.
Pia ilitupilia mbali ushahidi wa mamia ya kurasa uliowasilishwa na Odinga kuongeza uthibitisho wa tuhuma za kuwepo mapungufu, ingawa hiyo ilikuwa ni sehemu ya ushahidi uliowasilishwa. Jumatatu iliyopita, mahakama hiyo iliamuru kura zihesabiwe upya katika vituo 22, ikiwa ni sehemu ya jumla ya vituo 32,000 vya kupigia kura nchi nzima. Matokeo ya kura hizo bado hayajatolewa.
Matokeo rasmi yalionyesha kuwa rais aliyechaguliwa, Uhuru Kenyatta ameshinda kwa zaidi ya kura 8,000 na kupata asilimia 50.7 ya kura na hivyo kuepuka duru ya pili ya uchaguzi. Kenyatta, alitangazwa mshindi Machi 9 mwaka huu. Odinga amewasihi wafuasi wake kubakia watulivu wakati wanasubiri uamuzi huo wa mahakama, na ameahidi kuheshimu uamuzi huo.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE
Mhariri: Josehat Charo