Uhuru wa vyombo vya habari
3 Juni 2020Picha za waandishi wa habari tofauti wanaoripoti kutoka Marekani kuhusiana na hali inayoendelea nchini humo kwa sasa zinavuruga akili. Maafisa wa polisi wanakabiliana na waandishi wa habari ambao wanastahili kuwa huru katika utenda kazi wao.
Lakini sisi kama waandishi wa habari, hatutatikiswa kivyovyote vile, kama alivyosema mwandishi wa DW Stefan Simons ambaye alionekana akikabiliwa na maafisa wa polisi na pia akapigwa risasi ya mpira. Alipatikana katika hali hiyo alipokuwa katikati ya kuripoti kuhusiana na maandamano yanayoendelea nchini humo.
Wanaowazuia waandishi wa habari kufanya kazi hawatofanikiwa
Katika siku chache zilizopita, shirika la utafiti la Bellingcat limeripoti kuwa zaidi ya waandishi mia moja wamekuwa wahanga wa ukatili wa polisi nchini Marekani. Kati yao, Linda Tirado ambaye ni mpiga picha alipoteza jicho baada ya kupigwa risasi ya mpira.
Wale wanaotuzuia waandishi wa habari kufanya kazi yetu, hawatofanikiwa kwasababu, kuripoti kwa njia huru ni sehemu ya demokrasia. Bila shaka hili ni wazi pia nchini Marekani, nchi ambayo inashikilia nafasi ya 45 duniani katika orodha ya Maripota Wasio na Mipaka. Waandishi wa habari nchini Marekani sasa wanafanya kazi katika mazingira mabaya sana ukizingatia pia wanakabiliwa na matusi ya mara kwa mara kutoka kwa Rais Donald Trump. Jambo hili ni lazima lifikie mwisho.
Lakini jaribio la kuwatisha na kuwachafulia jina waandishi halitofanikiwa. Ripoti kuhusu ukatili wa polisi, matumizi mabaya ya mamlaka au polisi kushindwa kutekeleza majukumu yao, ni masuala ambayo tunachukua tahadhari kuyaripoti kwasababu kila mtu ana haki ya kupata taarifa hata ikiwa wengine hawapendi.
Deutsche Welle imewasilisha malalamiko kwa Ubalozi wa Marekani
Kila tunaposhambuliwa waandishi wa habari, uhuru wa kupata taarifa ndio umeshambuliwa, kwa hiyo ni lazima tutetee kukandamizwa kwa uhuru wa kuripoti kwa njia zozote zile za kisheria.
Shirika la habari la Deutsche Welle, limeuandikia ubalozi wa Marekani kutoa malalamiko yake kuhusiana na kuhatarishwa kwa waandishi wake nchini Marekani. Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Heiko Maas ameitaka Marekani kuulinda uhuru wa wanahabari na ametaka pia uchunguzi ufanyike kuhusiana na mashambulizi hayo.
Ni vizuri kuwahamasisha watu baada ya mashambulizi haya dhidi ya waandishi wa habari kwa kuwa, waandishi wanapokandamizwa, basi haki zengine zitakuwa hatarini pia. Ndio maana tunastahili kuendelea kuwataarifu watu kuhusiana na kinachoendelea Marekani, Hong Kong, Urusi, Ujerumani na kote duniani. Hatutokubali kupokonywa uhuru huu.