1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSenegal

Uhuru waminywa Senegal kuelekea uchaguzi wa rais 2024

10 Machi 2023

Waziri mkuu wa zamani wa Senegal Cheikh Hadjibou Soumare amekamatwa baada ya kumuuliza Rais Macky Sall iwapo alikuwa amemfadhili mwansiasa wa Ufaransa kutoka chama kinachoeneza chuki na kuwakataa wengine.

Belgien EU-Afrika-Gipfel Präsident Macky Sall
Picha: John Thys, Pool Photo/AP/picture alliance

Afisa moja wa polisi amesema Soumare, ambaye alikuwa waziri wa bajeti na kisha waziri mkuu kutoka 2007 hadi 2009 chini ya rais wa zamani Abdoulaye Wade, aliitwa na polisi siku ya Alhamisi.

Katika barua ya wazi kwa Rais Sall mwishoni mwa wiki iliyopita, Soumare alimuuliza rais kama ametoa euro milioni 12 kwa mwanasiasa wa Ufaransa ambaye chama chake kinatambuliwa kuchochea chuki na kuwakataa wengine.

Serikali ya Senegal, katika taarifa yake siku ya Jumanne, ilikanusha kutoa mchango wowote wa kifedha kwa kiongozi wa chama cha National Rally, Marine Le Pen, ambaye alimtembelea Sall katika mji mkuu wa Dakar Januari 18.

Soma pia: Senegal yaitaka Ujerumani kubakisha majeshi yake Mali

Katika taarifa siku ya Jumanne, serikali ilisema "inakataa na kulaani vikali usingiziaji kama huo wa uoga usiyo na msingi." Hata hivyo watetezi wa haki na wapinzani wa Sall wanasema uhuru wa kiraia nchini Senegal unakabiliwa na shinikizo katika maandalizi ya uchaguzi wa Februari 2024.

Cheikh Hadjibou Soumare, kulia, akiteteta jambo na rais wa zamani wa Senegal Abdoulaye Wade. Soumare amekatwa kwa kumuuliza swali rais wa sasa Macky Sall.Picha: picture-alliance/ dpa / maxppp

Waandishi wa habari waandamwa

Baada ya mwandishi mashuhuri wa Kisenegal Pape Ale Niang kukamatwa Novemba mwaka jana kwa tuhuma za kueneza habari za uongo, mwanaharakati Beyna Gueye alifanya maandamano madogo, akidai kuachiliwa kwa mwandishi huyo kufuatia mkutano na waziri mkuu Amadou Ba.

Alikamatwa mara moja na kuhukumiwa kifungo cha miezi mwili gerezani. Na siku ya kuachiwa kwake wiki hii, mwandishi mwingine wa habari alikamatwa pia kwa tuhuma za "kueneza habari za uongo."

Soma pia: Senegal yapata Waziri Mkuu tangu kufutwa wadhfa huo mnamo 2019

Gueye mwenye umri wa miaka 24, alisema yeye na wanachama wengine wawili wa vuguvugu la kiraia, linaloongozwa na mwanamuzi wa miondoka ya kufokafoka Abdou Karim Gueye, walikamatwa Januari baada ya kushiriki katika mkutano na Waziri Mkuu kuhusu madai ya matumizi mabaya ya fedha za Uviko-19.

Walichukuliwa baada ya kutoka kwenye mkutano wakiimba, "Mwachieni Pape Ale Niang". Niang, ambaye ni mkuu wa tovuti ya habari ya Dakar Matin, pia anajulikana kuwa mkosoaji wa rais.

Kesi dhidi ya Niang iliibuka baada ya kuandika kuhusu mashtaka ya ubakaji yanayomkabili kiongozi mkuu wa upinzani nchini Senegal, Ousmane Sonko.

Kiongozi mkuu wa upinzani nchini Senegal Ousmane Sonko anaekabiliwa na kesi ya ubakaji, ambayo baadhi wanashuku imechochewa kisiasa.Picha: Seyllou/AFP/Getty Images

Ameshutumiwa, miongoni mwa mambo mengine, kufichua habari zinazoweza kuhatarisha usalama wa taifa na kueneza habari za uongo.

Je, Sall kuwania muhula wa tatu?

Wanaharakati wa haki wamekuwa wepesi kumkumbusha Rais Sall, ambaye alichaguliwa mwaka wa 2012 na tena 2019, kwamba aliahidi katika mahojiano ya 2015 kamwe hatamfunga jela mwandishi wa habari kwa kosa la vyombo vya habari.

Soma pia: Rais wa Senegal Kupunguza Muda wa Mhula

Lakini siku ya Jumanne, mwanahabari mwingine, Pape Ndiaye wa kituo cha habari cha Walf TV, alishtakiwa na kuzuiliwa baada ya kutilia shaka uhuru wa idara ya mahakama katika kesi ya Sonko.

Kesi hiyo na tishio lake dhidi ya mpango wake wa kuwania urais, vimekuwa chanzo cha mvutano nchini Senegal kwa miaka miwili.

Mpaka sasa Rais Sall hajathibitisha au kukanusha ikiwa ana nia ya kuibadili  katiba na kuwania muhula wa tatu wa urais mwaka 2024.

Chanzo: AFPE

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW