1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
HistoriaAfrika

Uhusiano baina ya ugozi wa zama za ukoloni na unazi

28 Desemba 2023

Ukoloni uliiwezesha Ulaya kujipatia maeneo makubwa ya ardhi na udhibiti wa mamilioni ya raia, lakini pia uliyapatia tatizo la jinsi ya kuihalalisha, kimaadili na kisayansi, dunia ovu na ya kibaguzi waliyoiunda wenyewe.

 Mfululizo wa makala hizi za za Kivuli cha Ukoloni wa Ujerumani unatayarishwa na DW, shirika la kimataifa la utangazaji la Ujerumani, kwa ufadhili wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani (AA). Ushauri wa masuala ya historia umetolewa na Profesa Lily Mafela, Profesa Kwame Osei Kwarteng na Reginald Kirey.
 Mfululizo wa makala hizi za za Kivuli cha Ukoloni wa Ujerumani unatayarishwa na DW, shirika la kimataifa la utangazaji la Ujerumani, kwa ufadhili wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani (AA). Ushauri wa masuala ya historia umetolewa na Profesa Lily Mafela, Profesa Kwame Osei Kwarteng na Reginald Kirey.Picha: Comic Republic

Vipi machafuko yalichangia nadharia za ugozi kwenye makoloni ya Ujerumani?

Kufikia mwanzoni mwa miaka ya 1900, tayari vikosi vya jeshi la kikoloni la Ujerumani vilishaushinda upinzani nchini Tanzania, Kameruni, Togo na Namibia za sasa kwa kutumia ukatili na ugaidi usio kifani.

Kutoka mwaka 1905 hadi 1907, ukatili dhidi ya vuguvugu la Maji Maji na sera ya kuangamiza ardhi nchini Tanzania viliuwa zaidi ya watu 300,000.

Soma zaidi: Ukosefu wa imani kwa chanjo za Magharibi ulivyozalika wakati wa ukoloni

Mauaji ya kwanza ya kimbari katika karne ya 20 nchini Namibia yaliangamiza asilimia 80 ya watu wa jamii ya Ovaherero na asilimia 50 ya watu wa jamii ya Nama.

Kivuli cha ukoloni wa Ujerumani - Sehemu ya Kwanza

This browser does not support the audio element.

Ukoloni uliwafanya wakoloni na wasomi wakutane moja kwa moja na watu wasiokuwa Wazungu kama wao, na katika makutano hayo ukazaliwa ugozi uliotokana na ukandamizaji uliovikwa sura ya dharau na ya kisayansi.

Vipi Ujerumani ilijaribu kuhalalisha utawala wake kupitia nadharia ya ugozi?

Nadharia ya ugozi - fikra kwamba watu wenye rangi tafauti za ngozi wana tafauti pia za mambo mengine - ilikuwa nadharia iliyokubalika.

Tatizo ni kwamba ilikuwa shida kupata uthibitisho wa kisayansi kuunga mkono ugozi. Baada ya yote, vipi unaweza kusema kuwa tafauti ya rangi za ngozi ni jambo la msingi kwa tafauti nyengine, ikiwa watu walishachanganyika zama na zama?

Kivuli cha Ukoloni wa Ujerumani

02:47

This browser does not support the video element.

Kujaribu kutatua tatizo hili, mwaka 1908, mwanaanthropolojia Eugen Fisher aliwasili Ujerumani ya Afrika Kusini Magharibi kutafiti jamii iliyofahamika kama Rehoboth Basters. Jamii hii ipo hadi leo nchini Namibia. Imeundwa na kizazi cha mchanganyiko wa Wazungu na Waafrika katika Cape, kabla ya kuzagaa kaskazini hadi kati ya Namibia. Wanazungumza aina fulani ya lugha ya Kidachi, kwa kiasi kikubwa waliishi maisha ya Kizungu, walikuwa Wakristo na walikuwa machotara.

Soma zaidi: Quane Martin Dibobe: Kutoka maonesho hadi mwanaharakati dhidi ya ukoloni

Lakini lengo la Fischer lilikuwa ni kutafuta vinasaba na kuthibitisha urithi wa "tabia za rangi za ngozi" na hivyo kujenga hoja ya "ugozi" kwenye baiolojia.

Kwa sababu kama unaweza kuthibitisha kisayansi kwamba kuna tafauti baina ya watu wenye rangi tafauti za ngozi, basi unaweza kwa urahisi kuhalalisha kisayansi majukumu tafauti kwa watu wenye ngozi tafauti katika jamii ya kibinaadamu. Ama kwenye muktadha wa ukoloni, unaweza kuonesha kwa nini ni halali kwa wenye ngozi nyeupe kuwatawala "watu dhalili" wenye ngozi nyengine.

Kwa kuwachunguza watoto wa Baster, kupima mafuvu yao, kuzingatia rangi ya nywele na macho na mambo mengine, Fischer alithibitisha kwamba kulikuwa na tafauti za ugozi baina ya wanaadamu, na aliamini kuwa watu wenye asili mchanganyiko, yaani machotara, walikuwa bora zaidi mbele ya wenyeji lakini, hata hivyo, hata wao nao walikuwa watu wa chini mbele ya wakoloni wa Kizungu.

Soma zaidi: Togo "Koloni la Mfano"

Kwa hitimisho lake hilo, Fischer alipiga kampeni ya kuwapo kwa "utenganishaji watu kwa misingi ya rangi za ngozi" zao ndani ya jamii.

Matokeo yake, ndoa ama mahusiano ya kindoa baina ya watu weupe na weusi yalipigwa marufuku kote kwenye makoloni ya Kijerumani.

Vipi kwa wasomi kuukubali ugozi wa kisayansi kuliusaidia ukoloni? 

Nadharia za ugozi za Fischer zilikubalika kama sayansi ya kweli na kuchochea mabadiliko makubwa mno kwenye somo hilo kiasi cha kwamba mahitaji ya mafuvu na mifupa ya watu waliouawa nchini Tanzania na Namibia yalipanda juu, yote kwa jina la utafiti wa kusaka uthibitisho kwamba Wazungu walikuwa "bora zaidi" kuliko wenyeji kwenye mataifa waliyoyatawala.

Hii ilikuwa sababu kwa nini madaktari wa serikali ya kikoloni ya Ujerumani waliwatumilia Waafrika kwenye majaribio ya madawa yao na hata kuwalazimisha kuchomwa chanjo.

Soma zaidi: DW yazindua makala mpya za "Kivuli cha Ukoloni wa Ujerumani"

Nadharia hii ya ugozi iliwaondolea hisia ya ubinaadamu kwa Waafrika, kwa sababu mfumo kandamizi wa kikoloni uliwapa wataalamu hao wepesi kuiendea miili ya Waafrika kuipima, kuihisabu na kuichambua bila kujali kuwa ilikuwa ya wanaadamu kama wao.

Nadharia na mapendekezo ya Eugen Fischer kuhusiana na kile kilichoitwa "utoharifu wa kigozi" yalitekelezwa barani Afrika, na kupewa hadhi ya kuwa sehemu ya mfumo wa afya ya umma. 

Vipi nadharia za Fischer ziliuathiri Unazi?

Inaripotiwa kwamba Adolf Hitler alisoma kitabu cha Fischer kiitwacho The Principles of Human Heredity and Race Hygiene akiwa gerezani na fikra kuhusu utoharifu wa ugozi na daraja za ugozi ziliathiri sana kitabu chake, Mein Kampf.

Kivuli cha Ukoloni wa Ujerumani - Utwaaji wa ardhi

01:59

This browser does not support the video element.

Kitabu hicho cha Fischer kilikuja kuwa na athari kubwa kwenye sheria za kigozi na chuki dhidi ya Mayahudi za Nuremburg mwaka 1935, na ambazo ndizo zilizotengeneza mazingira kwa Wanazi kuwaangamiza Mayahudi na makundi mengine kutoka jamii ya Kijerumani.

Kuna mfanano upi baina ya sera za Unazi na ukoloni?

Nadharia za kisomi za ugozi, kambi za mateso kwenye makoloni wakati wa Ubeberu wa Ujerumani, ukatili na mambo mengine yaliyojiri zama hizo, yamepelekea wasomi kadhaa kuhoji kwamba udhalilishaji wa ukoloni wa Kijerumani barani Afrika ndio ulioiunda sera ya Unazi hadi na wakati wa Vita vya Pili vya Dunia.

Sababu ni kwamba mifumo yote miwili ilitegemea ukatili na ilikuwa na itikadi kali kabisa ya ugozi.

Soma zaidi: Uporaji wa ardhi: Kuzaliwa kwa Himaya ya Ukoloni wa Ujerumani

Wengi kati ya waungaji mkono wakubwa wa sera ya utoharifu wa kigozi ya Ujerumani chini ya Wanazi walikuwa ndio hao hao waliokuwa wakifanya kazi kwenye makoloni, akiwemo Fischer mwenyewe.

Mwengine ni Ernst Rodenwaldt, ambaye pia alianza kazi kama daktari wa kikoloni nchini Togo na Kameruni ambako alitekeleza sera za utoharifu wa ugozi. Anatambuliwa kama muungaji mkono mkubwa wa "utenganishaji watu kwa misingi ya rangi za ngozi" zao, na mtetezi wa damu safi ya Kijerumani dhidi ya kuchanganyika na wale walioitwa "watu wa chini", ambao kwa wakati huo walijumuisha pia Mayahudi, Weusi, Waroma na Waulaya Mashariki. 

Wakati wa uzinduzi wa Mfululizo wa Makala za Kivuli cha Ukoloni wa Ujerumani tarehe 14 Disemba 2023 jijini Dar es Salaam.Picha: DW

Hata baada ya Vita vya Pili vya Dunia na licha ya mahusiano yao makubwa na utawala wa Kinazi, ushawishi wao kwenye nadharia ya ugozi na uhusika wao kwenye kuwatumia wanaadamu kwa majaribio, Fischer na Rodenwaldt walisalia kuwa wasomi wanaoheshimika, na hakuna mmoja kati yao aliyewajibishwa kwa kazi yao ambayo ndiyo iliyopelekea vifo vya mamilioni.

Vipi ugozi uliendelea Namibia baada ya Ujerumani kuondoka?

Afrika Kusini iliitawala Namibia kama amana tangu mwaka 1919 na ikaanza kutumia sheria ya ubaguzi wa rangi kuanzia miaka ya 1940. z

Juhudi za Fischer kwenye kukataza mahusiano baina ya Wazungu na wasiokuwa Wazungu ziliakisika kwenye sheria za ubaguzi wa rangi ambazo zilipiga marufuku ndoa baina ya watu wenye rangi tafauti za ngozi, kama ile iitwacho Sheria ya Ukosefu wa Maadili na Sheria ya Ndoa Mchanganyiko, ambazo zilidumu hadi mwaka 1990 wakati Namibia ilipopata uhuru wake kutoka Afrika Kusini.

Soma zaidi: Pambana! Jinsi Waafrika Mashariki walivyokabiliana na ukandamizaji wa kikoloni

Juu ya yote, nadharia ya ugozi ilitaka kuhalalisha nguvu na ukatili wa Wazungu na vizazi vyao dhidi ya watu waliowatawala, na haikuwa na uhusiano wowote na afya ya umma. Na ingawa maafisa wa kikoloni wa Ujerumani hawakuwa wa kwanza, pekee wala wa mwisho kutekeleza kiwango hiki cha nadharia ya ugozi, vivuli vilivyoletwa na sera hizi zisizo za kibinaadamu vinaifunika Ulaya na Afrika hadi hivi leo.

 Mfululizo wa makala hizi za za Kivuli cha Ukoloni wa Ujerumani unatayarishwa na DW, shirika la kimataifa la utangazaji la Ujerumani, kwa ufadhili wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani (AA). Ushauri wa masuala ya historia umetolewa na Profesa Lily Mafela, Profesa Kwame Osei Kwarteng na Reginald Kirey.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW