1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhusiano kati ya Rwanda na Burundi unayumba zaidi

18 Januari 2024

Uhusiano kati ya Burundi na Rwanda umekuwa wa kuregarega kwa miaka mingi. Mpaka kati ya mataifa hayo mawili uliofunguliwa yapata miaka miwili iliyopita, umefungwa tena baada ya mvutano mpya kuibuka kati ya majirani hao.

Marais Evariste Ndayishimiye na Paul Kagame
Rais Evariste Ndayishimiye wa Burundi na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame

Burundi imesitisha uhusiano wa kidiplomasia na Rwanda na imeamua pia kuufunga kwa muda usiojulikana mpaka wake na jirani yake huyo. Uamuzi huo ulifanyika wiki iliyopita, huku serikali ya mjini Bujumbura ikiituhumu Rwanda kwa kuliunga mkono kundi la waasi la RED - Tabara.

Rwanda hata hivyo imekanusha kuliunga mkono kundi hilo ambalo linaaminika kuwa na makao makuu yake mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Kundi la RED - Tabara limekuwa likiishambulia Burundi, ambayo imeliorodhesha kundi hilo kuwa la kigaidi. RED - Tabara ilidai kuhusika na shambulio la mnamo Disemba 22 katika ardhi ya Burundi kwenye eneo moja lililoko umbali wa kilomita 20 kutoka mji mkuu wa Burundi. Kundi hilo lilidai kuwa, maafisa 10 wa usalama waliuawa katika shambulio hilo, huku serikali ya Burundi ikisema watu 20 walipoteza maisha- wengi wao wakiwa raia.

Msemaji wa serikali ya Rwanda Yolande Makolo alisema katika taarifa kuwa, uamuzi wa Burundi wa kusitisha uhusiano wake wa kidiplomasia na Kigali na pia kuufunga mpaka wake, sio uamuzi wa busara na kwamba unakiuka kanuni za Jumuiya ya Afrika Mashariki za ushirikiano mwema wa kikanda.

Phil Clark, profesa wa siasa za kimataifa katika chuo kikuu cha SOAS cha London Uingereza ameiambia DW kuwa, mpaka kati ya Rwanda na Burundi ulifungwa kwa muda mrefu - kati ya mwaka 2015 na 2022, na kwamba kulionekana kuwepo kwa nuru mwaka 2022 ya kuimarika kwa uhusiano kati ya nchi hizo wakati mpaka huo ulipofunguliwa.

Clark ameendelea kueleza kuwa, baada ya kufungwa tena kwa mpaka huo safari hii, ni dhihirisho ya kuwepo kwa chembechembe za kutoelewana kati ya serikali hizo mbili.

Profesa huyo wa siasa za kimataifa amesema huenda ikachukua muda mrefu, ikiwezekana hata miezi hadi pale mpaka huo utakapofunguliwa tena. Mvutano kati ya Rwanda na Burundi una mizizi ya kihistoria ambayo mara nyingi inahusisha masuala ya kisiasa, kikabila na hata kiuchumi. Msuguano kati ya nchi hizo mbili pia umechangia kuwepo kwa changamoto za hapa na pale za kidiplomasia na mizozo isiyotabirika.

Burundi inaituhumu Rwanda bila ya kuwepo ushahidi

Mipaka kati ya Burundi na Rwanda imefungwa tena baada ya kufunguliwa miaka kdhaa iliyopitaPicha: Stephanie Aglietti/AFP/Getty Images

Kulingana na Clark, Burundi haijatoa ushahidi wowote wa kuthibitisha madai waliyo nayo dhidi ya Rwanda.

Amesema na hapa namnukuu, "kuna ushahidi mdogo kuonyesha kuwa Rwanda inaliunga mkono kundi la waasi la RED - Tabara mashariki mwa Kongo. Kundi hilo kwa kiasi kikubwa linajumuisha wapiganaji wa Burundi. Wengi wao ni wanajeshi wa zamani wa Burundi ambao wana matatizo yao na serikali kwa muda mrefu," mwisho wa nukuu.

Mnamo mwaka 2015, Burundi ilifunga mpake wake na Rwanda wakati kulipozuka ghasia za baada ya uchaguzi kufuatia kuchaguliwa tena Rais Pierre Nkurunzinza. Wakati huo, mamlaka ya Burundi ilikinyooshea kidole cha lawama Rwanda kwa kuchochea maandamano na kuhimiza kufanyike mapinduzi ya serikali. Itakukumbukwa kwamba Rais Paul Kagame alikuwa mkosoaji mkubwa wa utawala wa Nkurunziza.

Hivi karibuni, uhusiano ulionekana kunawiri baada ya Rais Evariste Ndayishimiye kuingia madarakani mwaka 2020, na chini ya utawala wake aliufungua tena mpaka wa nchi hiyo na Rwanda mwaka 2022 na popole biashara kati ya nchi hizo mbili zikaanza kuimarika.

Hata hivyo, uhusiano uliingia doa baada ya Burundi kutuma wanajeshi wake mashariki mwa Kongo kuisaidia serikali ya Kinshasa kupambana na waasi wa M23. Kongo yenyewe, imekuwa ikiishtumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi hao, huku wataalamu wa Umoja wa Mataifa wakionekana kuipa nguvu kauli ya Kongo kwamba Rwanda ni kweli inawaunga mkono M23.

Serikali ya Rwanda hata hivyo, imekanusha kuwa na mafungamano ya aina yoyote na waasi hao wa M23.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW