1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UHusiano kati ya Ujerumani na Ufaransa Magazetini

Oumilkheir Hamidou
17 Oktoba 2019

Uhusiano kati ya Ujerumani na Ufaransa, Uvamizi wa Uturuki nchini Syria na maonyesho ya kimataifa ya vitabu mjini Frankfurt ni miongoni mwa mada magazetini.

Frankreich Toulouse | Emmanuel Macron & Angela Merkel
Picha: picture-alliance/AP Photo/F. Scheiber

Tunaanzia njia panda inayoiunganisha Ufaransa na Ujerumani. Uhusiano kati ya madola haya mawili makubwa ya Umoja wa Ulaya umepwaya. Misimamo ya viongozi wa nchi hizo mbili, kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Emmanuel Macron wa Ufaransa inatofautiana pia katika masuala kadhaa. Gazeti la "Rheinpfalz" linaandika: "Kwa jinsi gani viongozi hao wananuniana, jibu la suala hilo limebainika katika kuteuliwa mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa ulaya.

Kutokana na shinikizo la Macron, mjerumani Manfred Weber hakuteuliwa kuiongoza halmashauri hiyo. Macron alikuwa na lengo lake ambalo amelitekeleza kama alivyopanga. Na sasa Macron anahisi kama ni kisasi cha Ujerumani baada ya mgombea wake Sylvie Goulard kukosa imani ya wabunge wa Ulaya,kuweza kuchaguliwa kama kamisha wa Umoja wa ulaya. Ndo kusema watajirekebisha? Abadan! Ukweli ni kwamba Macron hajatekeleza bado hata lengo moja kati ya mengi anayodhamiria."

Kiburi cha rais wa Uturuki Erdogan

Uturuki inaendelea na opereshini zake kaskazini mwa Syria. Rais Recep Tayyip Erdogan anapuuza miito ya jumuia ya kimataifa ya kusitisha opereshini jizo. Gazeti la "Südwest Presse" linamulika hali namna ilivyo na kuandika: "Wanasiasa wa Ujerumani na Umoja wa Ulaya wamelaani kwa sauti moja uvamizi wa vikosi vya Uturuki nchini Syria. Laana hizo zimsaidia nini? Kelele za chura. Erdogan anatambua fika hakuna chochote kikubwa ambacho kingemsumbuwa. Ujerumani na Umoja wa Ulaya hawawezi kuvumilia mfarakano pamoja na Uturuki. Kwa miongo sasa hali imekuwa ikiendelea hivyo hivyo na watu wanafumba macho na kunyamaza kimya."

Maonyesho ya vitabu mjini Frankfurt ni nuru kataika enzi za digitali

Mada yetu ya mwisho magazetini inatufikisha Frankfurt yanayokoendelea maonyesho ya kimataifa ya vitabu. Gazeti la "Mittelbayerische Zeitung" linachambua umuhimu wa maonyesho kama hayo katika enzi hizi za digitali. Gazeti linaendelea kuandika: "Katika enzi hizi za sasa, maonyesho ya kimataifa ya vitabu mjini Frankfurt yanafungua upenu wa kudhihirisha umuhimu mkubwa wa maneno yaliyoandikwa. Neno linaendelea kupumbaza na halijapoteza uzito wake. Na hilo limedhihirika  katika maonyesho ya vitabu kutokana na ushahidi wa wanaohudhuria. Kusoma ni muhimu. Aliyebahatika kutumia wakati wake kusoma vitabu, hakosi kupata faida yake. Mwenye kusoma kwa bidii anatafakari na kutafakari ni jambo muhimu ili kutofautisha jema na baya."

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri:Yusuf Saumu

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW