Uhusiano kati ya Uturuki na Jumuiya ya Ulaya
26 Machi 2018
Yafuatayo ni baadhi ya masuala ambayo huenda yakajitokeza:
Uanachama wa Uturuki katika EU
Kasi ya mchakato wa Uturuki kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Ulaya mara nyingi umekuwa wa pole pole. Moja ya sababu ni kujivuta kwa Ufaransa na Ujerumani kuhusu msimamo wa Uturuki kwa haki za binadamu.
Mashauriano kati ya Ubelgiji na Uturuki yamegonga mwamba tangu kushindwa kwa jaribio la mapinduzi mwaka 2016.
Mataifa wanachama wa Jumuiya ya Ulaya wameshindwa kusitisha msaada wa kifedha kwa Uturuki kwa muda huku bunge la Jumuiya ya Ulaya likiunga mkono hatua hiyo kwa maana kuwa Uturuki ingali inapokea msaada wa kifedha katika juhudi za kufikia viwango vya Jumuiya hiyo.
Uturuki ingali inashinikiza kujiunga kwenye Jumuiya ya Ulaya lakini waziri wa masuala ya nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu hivi karibuni alisema kuwa: " Hatuna matarajio ya uanachama kuhusu Jumuiya ya Ulaya."
Uhamiaji
Maafisa wa Jumuiya ya Ulaya mara kwa mara wanarejelea mkataba ulioafikiwa mwaka 2016 kama mfano wa pande mbili zinazoweza kufanya kazi pamoja.
Chini ya mkataba huo, Uturuki ilikubali kuwahifadhi wakimbizi wanaoelekea Ulaya wengi wao wakiwa wanaotoroka vita nchini Syria.
Kwa upande wake, Jumuiya ya Ulaya iliahidi msaada wa euro bilioni 6 kwa jumla sawa na dola bilioni 7.4. Ulaya inasema kuwa imeshatoa euro bilioni tatu katika awamu ya kwanza, ijapokuwa Uturuki inasema kuwa imepokea euro milioni 850 pekee.
Uturuki inataka kutoa fedha hizo moja kwa moja lakini Ubelgiji inasisitiza ufadhili wa miradi inayoendeshwa na Uturuki. Shirika moja la misaada ambalo lilikuwa linafanya kazi na mataifa ya Ulaya lilifungwa na serikali ya Uturuki kama hatua ya kukabili mashirika yasiyo ya serikali nchini humo.
Kurahisisha Upatikanaji wa Visa
Kama sehemu ya mkataba wa uhamiaji, Jumuiya ya Ulaya iliahidi kuondoa masharti yaliyohitajika kwa raia wa Uturuki waliokuwa wanazuru mataifa ya Jumuiya hiyo.
Pande hizo mbili sasa zinazozana kuhusu suala hilo, huku Uturuki ikitisha kufuta mkataba wa wakimbizi, baada ya Jumuiya ya Ulaya kushindwa kuondoa masharti ya visa.
Haki za Binadamu
Jumuiya ya Ulaya imekuwa mkosoaji mkubwa kwa vitendo vya Uturuki dhidi ya majaji, vyombo vya habari na kuzima sauti za upinzani tangu kufeli kwa kwa jaribio la mapinduzi mwaka 2016.
Makumi ya maelfu wakiwemo wanahabari na wafanyikazi wa vyombo vya habari walitimuliwa kutoka kwenye ajira za umma.
Hivi karibuni majaji waliwaachia baadhi ya waandishi habari maarufu, ijapokuwa wengine walihukumiwa vifungo vya maisha.
Syria
Jumuiya ya Ulaya imeyataka mataifa ya Uturuki, Urusi na Iran kupunguza ghasia nchini Syria baada ya Uturuki kuanza operesheni za kijeshi katika eneo la Afrin. Bunge la Jumuiya ya Ulaya limeitaka Uturuki kuondoa vikosi vyake katika nchi ya Syria. Uturuki imepuuza wito huo. Uturuki inaviona vikosi vya Wakurdi kuwa kitisho cha ugaidi wakiwa na ushirikiano na chama cha wafanyikazi cha Wakurdi (PKK) kilichopigwa marufuku:
Ugaidi
Uturuki imetoa wito kwa mataifa wanachama wa Jumuiya ya Ulaya kuchukua msimamo mkali dhidi ya wanaounga mkono vugu vugu la kitaifa la Wakurdi, ikihoji kuwa Ulaya inawahifadhi magaidi. Uturuki inasema kuwa magaidi hao ndio waliochangia jaribio la kutaka kuipindua serikali mwaka 2016.
Mwandishi: Shisia Wasilwa, dpa
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman